– Ni mikopo inayozidi kushamiri kila kona nchini kila siku
– Inaongoza kuwafilisi wananchi hasa wa vipato vya chini ikiwemo watumishi wa serikali na binafsi kutokana na riba kuwa kubwa
– Inatajwa kutolewa kirahisi bila ya masharti mengi hivyo kuvutia watu wengi kuikimbilia
– Unaweza ukakopa milioni moja ukalipa milioni kumi kama utani
– Watoaji wa mikopo hiyo sasa waanza kujikita mitandaoni
– Wachambuzi wa Uchumi wahoji ilipo Benki kuu na hatua wanazochukua kuunusuru Uchumi wa wananchi
– Mjadala mzito wa ibuka wa nini hasa chanzo cha mikopo hiyo
NUKUU
‘’Urahisi wa upatikanaji wa mikopo hii ndio unatuponza, mfano mimi nilijaza fomu saa nane mchana, dakika chache baadae nikakopeshwa, na waliniambia riba ni ndogo kumbe kila milioni moja niliyochukua ina riba yake, kufika siku natakiwa kulipa kuangalia najikuta siwezi kulipa deni lote, ikaanza kupanda riba aisee, kila mwezi inaongezeka tu. Ilibidi jamaa achukue tu kigari chenyewe nilichoweka dhamana’’. Chikawe Chiganga, mmoja wa waathirika
Na. Mwandishi wetu
Utekelezaji wa tangazo la Gavana wa Benki kuu ya Tanzania la tarehe 13, mei mwaka huu la kuwataka watanzania kutoa taarifa kwa benki hiyo juu ya wafanyabiashara wanaojihusisha na kutoa mikopo bila kuwa na leseni za kufanya hivyo kama wanavyotakiwa na kifungu cha 17 cha sheria za huduma ndogo za fedha 2018 umekuwa mgumu kutokana na ukweli kuwa uwezo wa wananchi kuifikia benki hiyo na kuchambua kwa kutambua kama anayewakopesha ni taasisi iliyosajiliwa ama haijasajiliwa ni mdogo sana
Aidha, hali ya wananchi wengi wanaojikuta wanaingia na kuangukia kwenye taasisi zinazokopesha mikopo kwa riba kubwa haziwaruhusu hata kufikiria mara mbili kipindi wanataka kukopa kwani wengi wao hukimbilia kukopa kama chaguo la mwisho baada ya kukwama kwa majaribio yao mengi hasa kushindwa kukopeshwa benki
Taarifa za uchunguzi zinaonyesha kuwa sio wananchi wasio wafanya kazi tu ndio wanateseka na aina hii ya mikopo lakini pia hata watumishi wa serikali hasa wafanyakazi wapya wanaoanza maisha mapya kazini hukutana na aina hii ya mikopo kutokana kuwa na uhitaji mkubwa wa kupata fedha za kujikimu na kuanzishia maisha kabla ya kupokea mshahara na hivyo kujikuta wanaangukia mikononi mwa wakopeshaji hawa
Idadi ya vijana walioanza kazi na wanaoshuhudia kishahara yao inapita Kwenda kulipa mikopo hii ni kubwa na inasikitisha kwani kutokana na kukithiri kwa mikopo hii kunawafanya watumishi hao kukosa hamu ya kufanya kazi
‘’hata sisi wafanyakazi wa serikali tunapambana nayo mikopo ya namna hiyo, vijana wengi sana wanaoanza kazi wanateseka na mikopo hiyo, yupo kijana mmoja alikopa milioni 8, mpaka sasa amerejesha milioni 21 na bado mkopo haujaisha. Kwa kifupi ni hatari’’. Anasema mmoja wa wakopaji aliyeomba jina lake lihifadhiwe
‘’tamko tu la benki kuu ama Waziri kuwa watu watoe taarifa juu ya uwepo wa mikopo ama taaisi za hivi wala halitoshi, wakopaji hukimbilia huko baada ya kubanwa sana, serikali kupitia BOT lazima watafute suluhu ya uhakika hasa kupitia mabenki’’. Ameongeza
‘’lazima tujue ni kwanini kuna ugumu kwa mabenki kutoa mikopo yenye unafuu wa masharti kiasi cha watu kukimbilia KAUSHA DAMU, maana kama benki zingekuwa zinatoa mikopo bila shida nina hakika hii kausha damu isingekuwepo’’. Amesisitiza
Uzoefu unaonyesha kuwa mikopo ya KAUSHA DAMU ipo ya aina mbalimbali mingineyo ikihusisha hadi taasisi zilizosajiliwa kisheria lakini wanaweka vipengele vigumu katika mikataba yao hasa utata wa uchakataji wa rib ana hivyo kuwatesa wakopaji kulipa
Vile vile watu binafsi wasio taasisi za fedha wala kusajiliwa wamekuwa wakijihusisha na shughuli hizo za kukopesha wengine kwa kuweka dhamana moja kwa moja hasa magari, vyombo vya majumbani na thamani nyingine na asilimia kubwa ya wakopaji hushindwa kulipa na kujikuta wananyang’anywa dhamana walizoweka
Hivi karibuni Serikali imetoa wito kwa watoa huduma za kifedha nchini kufuata sheria na taratibu za huduma za Fedha ikiwemo kupata leseni ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa ufanisi bila kuwaumiza na kuwadhalilisha wanufaika na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa waratibu wa Biashara ya Huduma ndogo za Fedha na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, Afisa Mkuu Mwandamizi, Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Deogratias Mnyamani alisema kuwa, Benki Kuu chini ya Wizara ya Fedha na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa mikakati kupitia sheria ya huduma ndogo ya Fedha ya mwaka 2018, ili kukomesha udhalilishaji unaofanywa na baadhi ya watoa huduma ndogo za fedha kupitia mitandao ya simu.
Benki hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha imeona umuhimu wa kutoa elimu ya fedha nchi nzima ili kuwapa uelewa wananchi kuhusu namna bora ya kukopa fedha na kuweza kurejesha mkopo bila kudhalilishwa.
Bw. Mnyamani alisema mikopo inayotolewa kwa njia ya mitandao ya simu imekuwa changamoto kubwa hasa katika ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wakopaji jambo linalopelekea watoa huduma hao kuvunja sheria ya usiri inayotakiwa katika kupata huduma ya fedha kwa kuwadhalilisha wakopaji hao kwa kutuma ujumbe mfupi kwa ndugu na jamaa waliochukua mikopo hiyo.
‘’Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania tunahitaji kushirikisha, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Makampuni ya simu na Polisi ili kuona namna ambayo tunaweza kulitatua suala hili la udhalilishaji linalofanywa na watoa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu’’ alisema Bw. Mnyamani.
Bw. Mnyamani aliongeza kuwa Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania hivi karibuni itaendesha kampeni kupitia vyombo vya habari na njia mbali mbali za kutoa elimu kwa umma ili kujenga uelewa kwa wananchi na watoa huduma ndogo za fedha kuhusu masuala muhimu ya kuzingatia katika utoaji na upatikanaji wa huduma ndogo za fedha nchini.
Awali, akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro alisema ni wajibu wa watoa huduma ya fedha kutoa elimu kwa wananchi wanaoomba mikopo ili kuwawezesha kutumia mikopo hiyo kuzalisha faida na kuweza kurejesha kwa wakati.
Bw. Kimaro alisisitiza kuwa ni lazima mkopaji apewe elimu ya kutosha ili apate uelewa kuhusu masharti yaliyoanishwa kwenye mkataba kwa kupewa nafasi ya kusoma na kuuelewa mkataba wa mkopo kabla ya kuchukua mkopo husika.
“Ni lazima mkopaji apewe elimu ya kutosha ili apate uelewa, na apewe nafasi ya kusoma na kuelewa mkataba wa mkopo kabla ya kuchukua mkopo’’ alisema Bw. Kimaro.
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha, kutoka Mkoa wa Ruvuma, Bernard Evarist Ndikaniki, alisema mafunzo waliyopata yataikomboa jamii dhidi ya watoa huduma wasiokuwa waaminifu na kuchangia maendeleo ya nchi.
Bw. Ndikaniki aliongeza kuwa mafunzo hayo hayataishia tu kutoa faida kwa washiriki, lakini pia yanaenda kugusa jamii na ngazi ya chini kabisa ya wananchi yakiwa na lengo la kufikisha elimu hiyo kwa jamii ambayo ndio walaji wa mwisho wa huduma ndogo za fedha.
Mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma ndogo za fedha na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri hufanyika kila mwaka, lengo likiwa ni kuimarisha huduma jumuishi za kifedha ili kuleta ufanisi wa utoaji huduma kwenye Sekta ndogo ya fedha nchini kwa wananchi wenye kipato cha chini ili kuwakwamua kiuchumi.
Kadharika Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, Kanal Anthony Mwakisu amewataka Wananchi kukopa kwenye taasisi za fedha zilizosajiliwa na Serikali na kutambulika kwa kuwa itasaidia kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kwa mkopaji kwa kuwa taasisi hizo zinaendeshwa kwa mujibu wa Sheria.
Kanalı Mwakisu alitoa rai hiyo baada ya kukutana na wataalam wa Wizara ya Fedha, TAMISEMI, Benki Kuu na wataalam wengine kutoka Taasisi za Serikali waliofika Wilayani mwake kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali. Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza kuwa wananchi wanatakiwa kwenda kukopa Fedha kwenye benki na Taasisi nyingine za fedha zilizosajiliwa na zinazotambulika kisheria na siyo kwenda kukopa Fedha kwenye vikundi ambavyo havijasajiliwa na serikali. “Matumizi ya Fedha ni muhimu sana, hivyo wananchi wasikope tu kwenye vikundi ambavyo havijasajiliwa”. Amesisitiza Kanali Mwakisu Aidha, Kanali Mwakisu alisema kuwa Serikali imekusudia kuhakikisha wananchi wengi wanapata uelewa wa masuala ya fedha ili kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika huduma rasmi za fedha. “wakulima msifanye matumizi mabaya ya Fedha zenu mnapo vuna mazao yenu bali fedha hizo zitumieni Kwenye matumizi sahihi ikiwemo kupeleka watoto shule”. Aliongeza Kanali Mwakisu Kwa upande wake Bw. Stanley Kibakaya ambaye ni Afisa Usimamizi wa Fedha, Wizara ya Fedha, aliwataka wananchi wanapokopa waangalie viwango vya riba ndipo wakope na wanapokopa wahakikishe wanabaki na nakala ya mkataba ili panapotokea changamoto mkataba huo uwalimde.
Kwa upande wake, Bw. Abonaventula Frederick, mkaazi wa Kasulu aliishukuru Wizara ya Fedha kwa Kutoa Elimu hiyo ambapo aliiomba Serikali kuendelea kutoa Elimu katika maeneo mengine kwani asilimia kubwa ya wananchi hawajui wapi wanatakiwa kuhifadhi fedha zao na wapi wanatakiwa wakope.
“Wananchi wengi hawajui wapi pakuhifadhi fedha zao na wengi wamekopa sehemu ambazo siyo sahihi hali ambayo imesababisha wauze mali zao ikiwemo mashamba ili walipe mikopo wanayodaiwa, hivyo wengi wakipata elimu hii wataelimika’. Alisema Bw. Frederick.
Naye Bi. Stephanie Fulmasi alisema kuwa wamepata elimu kupitia filamu ambayo imeandaliwa na Wizara hiyo na kupitia filamu hiyo wamejifunza namna gani wakina mama wanatakiwa kwenda kukopa sehemu sahihi na siyo kukopa sehemu yenye riba kubwa”. Amesema Bi. Stephanie.