- Benki zinazomilikiwa na Serikali zawekwa pabaya kwa mabilioni ya fedha zake kutafunwa na wajanja
- Kufikia disemba 31 2023, benki ya maendeleo TIB ilikuwa na mikopo chechefu kwa asilimia 21.5 huku Azania benki wakiwa na asilimia 7.4 kinyume kabisa na maelekezo ya BOT yanayotaka mikopo hiyo isivuke asilimia 5
-Ni sawa na zaidi ya Shilingi Bilioni 206 za watanzania zimebebwa kama mkopo chechefu katika benki hizo mbili pekee - Serikali yashauriwa ichukue hatua za haraka kuzinusuru benki hizi, ikiwa ni pamoja na kuongeza mtaji kwa , kuboresha udhibiti wa gharama na kupunguza uwiano wa mikopo chechefu hadi kufikia kiwango kinachokubalika cha asilimia 5
NUKUU
‘’Benki ya Maendeleo ya TIB na Benki ya Azania kwa pamoja zilikuwa na mikopo chechefu ipatayo shilingi bilioni 206.04 (2022 mikopo chechefu shilingi bilioni 262.72) ikiwa imepungua kwa shilingi bilioni 56.68 huku sababu ikiwa ni kutozwa kwa mikopo chechefu ‘’ Taarifa ya CAG
Na. Mwandishi wetu,
Mikopo isiyolipika maarufu kama MIKOPO CHECHEFU inaelezwa kuwa moja ya kikwazo kikubwa cha ufanisi wa benki nyingi nchini na kichocheo kikubwa cha kurudisha nyuma uwiano wa kiasi cha fedha katika mzunguko wa jamii kutokana na kiasi kikubwa cha fedha kuwa mikononi mwa watu wachache hasa wafanyabiashara wakubwa na matajiri ambao wameibua mchezo mpya wa kukopa mabilioni ya shilingi na kukataa kulipa
Taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali kuhusiana na mikopo chechefu aliyoitoa mwezi machi mwaka huu inaonyesha ni kwa namna gazi benki zinazomilikiwa na serikali zinavyojikongoja kwa kukosa mtaji kutokana na sehemu kubwa ya mtaji wake kuwa mikononi mwa wakopaji waliokataa kulipa na hivyo kuifanya serikali kuunganisha baadhi ya benki ili kuunsda benki nyingine zenye mtaji mkubvwa
Katika taarifa hiyo CAG anaeleza kuwa alikagua utendaji wa benki zinazomilikiwa na Serikali, mifuko ya hifadhi ya jamii, Shirika la Bima la Taifa, na taasisi zinazohusika na usimamizi wa masoko ya mitaji na dhamana nchini Tanzania.
‘’Nilibainisha maeneo kadhaa ambayo taasisi hizi zina mapungufu ya kiutendaji na zinahitaji maboresho ili kuhakikisha utendaji wao unakuwa bora.Kwa benki tatu zinazomilikiwa na Serikali ambazo ni, Benki ya Maendeleo ya TIB, Benki ya Azania na Benki ya Biashara Tanzania nimebaini mapungufu kadhaa kama vile kutosimamia ipasavyo kwa mikopo, na kutokidhi matakwa ya udhibiti.’’. Inasema taarifa hiyo ya CAG
Mikopo chechefu, na Benki zinazopata hasara
‘’Ukaguzi wangu ulibaini Benki ya Maendeleo ya TIB iliendelea kupatahasara kabla ya kodi, mwaka 2023 hasara ilifikia shilingi bilioni 5.92(2022: hasara kabla ya kodi ilikuwa shilingi bilioni 131.97). Wakati Benki ya Biashara Tanzania ilipata hasara kabla ya kodi ya shilingi bilioni 41.40 (2022 faida kabla ya kodi shilingi bilioni 6.87),ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 48.27 sawa na asilimia 703. Hasara hii ilichangiwa zaidina kufutwa kwa mikopo chechefu iliyorithiwa kutoka iliyokuwa Benki ya TIB Corporate’’.inaongeza taarifa hiyo ya CAG
Taarifa hiyo inasisitiza kuwa katika mapitio ya mikopo chechefu ilibaini kuwa Benki ya Maendeleo ya TIB ilikuwa na mikopo chechefu ya asilimia 21.50 kufikia tarehe 31 Desemba 2023 (2022: mikopo chechefu asilimia 20.28), wakati Benki ya Azania ilikuwa na mikopo chechefu asilimia 7.44 hadi kufikia 31 Desemba 2023 ( 2022: mikopo chechefu asilimia 18.25). kinyume kabisa na matakwa ya kanuni inayosimamia ukomo wa mikopo ya BOT
‘’Pamoja na kupungua kwa uwiano wa mikopo chechefu kutoka mwaka uliopita kwa Benki ya Azania, ni vyema kutambua kuwa benki zote mbili bado zilivuka kiwango kinachokubalika na kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania cha asilimia 5. Pia, Benki ya Maendeleo ya TIB na Benki ya Azania kwa pamoja zilikuwa na mikopo chechefu ipatayo shilingi bilioni 206.04 (2022 mikopo chechefu shilingi bilioni 262.72) ikiwa imepungua kwa shilingi bilioni 56.68 huku sababu ikiwa ni kutozwa kwa mikopo chechefu ‘’ Imeongeza
CAG amebainisha kuwa Kuna uwezekano wa kuzorota kwa ubora wa mtaji wa mkopo kunaharibu mtaji mkuu wa Benki na unaathiri uwiano wa utoshelevu wa mtaji na utendaji wa benki hizo.
Ambapo katika hoja hizo amependekeza Serikali ichukue hatua za haraka kushughulikia masuala yanayozikabili benki hizi, ikiwa ni pamoja na kuongeza mtaji kwa Benki ya Maendeleo ya TIB, kuboresha udhibiti wa gharama na kupunguza uwiano wa mikopo chechefu hadi kufikia kiwango kinachokubalika cha asilimia 5.
Hayo yanajiri wakati mdhibiti na mkaguzi huo akionyesha wasiwasi juu ya ufanisi wa benki za Serikali kwenye Usimamizi duni wa dhamana zilizowekwa na wakopaji wa Benki ya Biashara Tanzania na Benki ya Azania kwa mikopo iliyotolewa ya shilingi bilioni 403.62
Soma hapa sehemu ya taarifa hiyo ya CAG
Benki ya Biashara Tanzania ilitoa mkopo wa shilingi bilioni 6.56 kwa wateja sita ambao hawakuweka dhamana kama inavyotakiwa na vipengele vya mikataba ya mikopo yao.
Pia, Benki ilitoa mikopo mingine ya shilingi bilioni 5.50 kwa wateja wawili bila kuhuisha dhamana zao za awali kabla ya kupata mkopo mwingine. Vilevile, nilibaini kutokuwapo kwa ripoti za uthamini za dhamana zilizoahidiwa za wateja sita zilizohusisha shilingi bilioni 8.34 kinyume na Muongozo wa ukopeshaji.
Pia, mapitio yangu yalibaini kuwa taarifa za dhamana za Benki ya Azania zilizotumika katika kukokotoa makadilio ya matarajio ya hasara inayotokana na kutokukusanya madai, zilibaini kutokuwepo kwa nyaraka kama vile ripoti za uthamini na bima za mikopo zinazohusisha
mikopo ya shilingi bilioni 383.22 iliyotolewa kwa wakopaji wapatao 60.
Hati za dhamana zisizotosheleza zinaweza kusababisha hatari ya benki kushindwa kurejesha mkopo kwa kunadi dhamana zilizowekwa endepo wakopaji watashindwa kurejesha mikopo yao.
Ninapendekeza Benki ya Azania na Benki ya Biashara Tanzania kuhakikisha mikopo iliyotolewa ina dhaminiwa na dhamana ya kutosha na yenye ubora pamoja na kuimarisha udhibiti wa usimamizi wa mikopo iliyotolewa ikiwa ni pamoja na kufuatilia mikopo iliyotolewa ikuungwa mkono na dhamana.
ii. Mikopo iliyotolewa na Benki ya Biashara Tanzania ya shilingi bilioni 734.28 ikiwa imezidi ukomo wa mikopo na bila kupata kibali cha Bodi ya Wakurugenzi
Aya ya 6.3 (i) ya Mwongozo wa Utoaji wa Mikopo wa Benki ya Biashara ya Tanzania wa mwaka 2022 inaeleza kuwa, ili kufikia na kudumisha amana ya mikopo yenye mfumo wa usalama wa sekta mbalimbali,menejimenti itaendelea kufuatilia utendaji wa sekta na kupendekeza mabadiliko kwenye Bodi ya Wakurugenzi kwa mapitio ya mipaka ya kiasi.
Benki ya Biashara Tanzania ilitoa mikopo ya shilingi bilioni 728.07 kwa sekta tano, ambazo ni sekta binafsi, sekta ya uchukuzi na mawasiliano,hoteli, migahawa na utalii, majengo na ujenzi, pamoja na elimu.
Mikopo hiyo ilikuwa juu ya ukomo ulioidhinishwa katika Sera ya Benki.
Pia, ilitolewa bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi.
Vilevile, Benki ilitoa mikopo yenye jumla ya shilingi bilioni 6.21 kwa sekta ambazo ni maghala na kuhifadhi, maji, umeme, uvuvi na afya ambazo hazikuidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi na pia sekta hizo haziko kwenye Mwongozo wa Ukopeshaji uliopo kwa sasa. Benki ilieleza
kuwa sekta zilizokuwa zimewekewa viwango ziliboreshwa katika Mwongozo wa Utoaji Mikopo wa mwaka 2023 ili kuendana na maelekezo ya Mdhibiti.
Muongozo huo tayari umeidhinishwa ndani ya Benki na unasubiri kuidhinishwa na Mdhibiti.
Aidha, Benki iliendelea kusisitiza kuwa sekta zilizojumuishwa katika muongozo ni pamoja na zile zilizobainishwa na mkaguzi.
Kuna hatari ya kuongezeka kwa hasara kutokana na kiasi kikubwa cha mikopo iliyotolewa zaidi ya kikomo na mikopo ambayo imetolewa kwenye sekta ambazo hazijaidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi.
Ninapendekeza Benki ya Biashara Tanzania kuimarisha udhibiti wa usimamizi wa mikopo iliyotolewa ikiwa ni pamoja na kufuatilia mikopo iliyotolewa na kuhakikisha mikopo inatolewa baada ya kupata kibali kinachostahili cha Bodi ya Wakurugenzi na iendane na
kikomo kilichoainishwa katika Sera.