Zanzibar,
11 Juni, 2024
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa rai kwa Wasomi, wanazuoni wenye taaluma, maarifa na uzoefu wa masuala mbalimbali ya taaluma, kujadili fursa na changamotozilizopatikana ndani ya kipindi cha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanziabar na Muungano wa Tanzania hasa kwenye utekelezaji wa Sera na Mipango ya Serikali.
Rais Dk. Mwinyi pia aliwasihi wasomi hao kutumia fursa za majukwaa na makongamano ya taaluma kuzungumzia Sera zinazopewa kipaumbelee na Serikali zote mbili za Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika utekelezaji wa Mipango mikuu ya nchi ikiwemo Uchumi wa
Buluu, Uwekezaji, Diplomasia ya Uchumi pamoja na kutoa mapendekezo yenye kuboresha ustawi wa Taifa.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo kwenye ukumbi wa Dk. Ali Muhammed Shein, Tunguu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja alipofungua Kongamano la kitaaluma la kumbukumbu ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, liliandaliwa na Baraza la Uongozi na Menejimenti ya
Chuo cha Utumishi wa Umma – Zanzibar (IPA) na Baraza la Uongozi na Menejimenti ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kutoka Kurasini – Dar es Salaam
Alisema, miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania, ni chachu ya maendeleo mengi yaliyopatikana kutoka sekta mbalimbali za Uchumi, Jamii, Siasa na Diplomasia.
Pia Rais Dk. Mwinyi alieleza imani yake kwa wataalamu wabobezi wakiwemowasomi na wanzuoni kwenye Kongfamno hilo, kuendelea kuelezea faida na matunda ya Mapinduzi, Muungano na Umoja wa Watanzania sambamba na kutoa hoja madhubuti, takwimu na maelezo ya kina yatakayolitambulisha vyema taifa hasa kwa nyakati zilizopita wakati uliopo na unaokuja.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alivipongeza vyuo vya Utumishi wa Umma, Zanzibar (IPA) na Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kwa mpango wa kuendesha shindano la uandishi wa insha lenye lengo la kuimarisha kumbukumbu ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Mapinduzi Matukufu za Zanzibar kwa wanafunzi wa Skuli zote za Msingi na Sekondari nchi nzima.
Halkadhalika, Rais Dk. Mwinyi aliwanasihi washiriki wa Kongamano hilo, kuitumia vizuri fursa hiyo kwa kujadili umuhimu wa kudumisha Mapinduzi ya Zanzibar na kuuenzi Muungano wa Tanzania kwa dhamira ile ile ya Waasisi wa Taifa, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Vile vile, Dk. Mwinyi alitoa wito kwa washiriki wa Kongamano hilo, kutumia vyema Jukwaa hilo kwa kuchangia na kutoa maoni yenye lengo la kuimarisha na kujenga manufaa zaidi yanayotokana na tunu za Mapinduzi na Muungano kwa Taifa kwani ndio msingi wa kuendelea kuwepo kwa hali ya amani, usalama na Umoja wa Kitaifa.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman pia aliwataka washiriki wa Kongamano hilo kuendelea kuhubiri juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na viongozi waliopo madarakani, Dk. Samia Suluhu Hassan an DK . Husssein Ali Mwinyi ya kuendelea kuhubiri amani, utulivu na ushirikiano baina ya Wa Tanzania.
Naye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Januari Yussuf Makamba amewapongeza Wanzibari na Wanatnzania kwa ujumla hasa kwa ushiriki wao wa moja kwa moja kwa kujadili Sera mpya ya Mambo ya nje ambayo pia imejumiya masuala ya Uchumi wa Buluu yenye tija kubwa kwa ustawi na maendeleo ya utalii nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi na Menejimenti ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kutoka Dar es Salaam,
Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi amesema wameamua kushirikiana na IPA kuandaa Kongamano hilo kwa lengo la kuwaweka pamoja Watanzania ili kujadili mchango wa Diplomasia na Sekta ya Umma kwenye maisha yao ya elimu na kuongeza uelewa kwa wananchi hasa kwa masuala mbalimbali ya uchumi na mandeeo kwa ustawi wa taifa lao la Tanzania
Sambamba naye, Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma – Zanzibar (IPA), Dr. Shaaban Mwinchum Suleiman, ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukiboresha chuo hicho na kukiongeza hadhi kwa kuwajengea jengo jipya litakaloimarisha huduma zao, Ombi lililokubaliwa na Serikali.
Kongamano la kitaaluma la kumbukumbu ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibarna Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lenye kauli mbiu isemayo “Miaka 60 ya Muungano katika diplomasia na Maendeleo Endelevu ya Uchumi wa Buluu”.
WAKATI huo huo Rais Dk. Mwinyi amekitembelea Chuo cha Ufundi cha Al Mubarak Mazrui cha Taasisi ya Al Mazrui Charitable Oganization ya Abu Dhabi, kilichopo Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi kinachotoa elimu zaufundi na kazi za amali.
Katika ziara yake kituoni hapo Rais Dk. Mwinyi aliwaka wanafunzi wanapokea maarifa ya ufundi kituoni hapo kuendeleza jitihada na kujifunza kwa bidii.
Rais Dk. Mwinyi pia alisifu mchango mkubwa wanaoutoa vijana wanaojifunza kituoni hapo kwa Mashirika ya mbalimbali ya Umma ikiwemo Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA).
Amesema tayari Serikali imetoa kibali cha kuajiri vijana hao wakiwemo waliojitolea muda mrefu kwa taasisi za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Maji ZAWA na Mashirika mengine ya Umma. Pia, amewasihi vijana wengine wanaoendelea kujifunza hapo kuendeleza utamaduni huo ili fursa zikitokea kwa Serikali na taasisi binafsi kuzichangamkia.
Sambamba na hilo, Rais Dk. Mwinyi ameishukuru Taasisi ya Al Mazrui Charitable Oganization ya Abu Dhabi kwa kutoa jengo lililokuwa kituo cha zamani cha kulelea watoto Yatima na kulitumia kwa kutua huduma za Afya.
Alisema Taasisi ya Al Mazrui Charitable Oganization ya Abu Dhabi ipo nchini tokea mwaka 1990 na imefanya maendeleo makubwa kwa jamii ikiwemo kulea na
kuwahudumia watoto yatima, kujenga misikiti, kujenga kituo cha kazi za amali kinachowahudumia wananchi wengi wa Zanzibar.
Kwa upande wake mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Jawwan Mubarak Mazrui, aliishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua kubwa ya maendeleo hasa kukuza huduma za jamii.
Aliahidi Serikali kuendeleza ushirikiano ulipo baina ya taasisi yake na Serikali kwa kuendeleza kuboresha huduma za jamii. Alisema, taasisi yao imefanikiwa kusambaza huduma nyingi za jamii Unguja na Pemba pamoja na Mikoa mengine ya Tanzania, ikiwemo Arusha, Morogoro na Dar es Salaam.