Serikali imesema kiasi cha shilingi Bilioni 12 kitatumika katika utekelezaji
wa mradi wa kukijanisha jjiji la Dodoma ikiwemo kupanda miti na maua
katika hifadhi za Barabara ili kutunza mazingira na kupendezesha
mandhari ya jiji hilo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa Juni 11, 2024
jijini Dodoma katika kikao cha pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo ambapo Mradi huo
wa Green Solution Project (GSP) unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo
Afrika (AfDB) ambayo inafadhili mradi wa ujenzi wa Barabara ya Mzunguko
wa Jiji la Dodoma (km 112.3).
“Naamini Timu za Wataalam wa Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya
Ujenzi na Taasisi zake zikishirikiana na kujadili suala la utunzaji wa
mazingira hususan katika jiji la Dodoma watakuja na mikakati bora ya
utekelezaji wa mradi huu”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo katika jiji
la Dodoma utafungua mawanda mapana kwa Serikali kutafuta wadau wa
maendeleo watakaoshirikiana na Serikali kukijanisha maeneo mbalimbali
nchini.
Aidha, Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,kuisimamia
TANROADS kuandaa usanifu na upembuzi yakinifu ambao hautaathiriwa
na mabadiliko na uboreshaji wa miundombinu ya barabara ikiwemo
upanuzi wa barabara ambao umekuwa ukisababisa ukataji wa miti ambayo
imepandwa hivi karibuni.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo ameipongeza Wizara ya Ujenzi kupitia
TANROADS kwa zoezi la upandaji miti na kuitunza hususan katika
barabara Chimwanga- Ihumwa Jct jijini Dodoma.
Dkt. Jafo amesema Serikali ina mpango wa kukutana na wamiliki na
wawekezaji wa maeneo yaliyo pembezoni mwa barabara ili kuweka
mkakati wa pamoja wa upandaji miti na bustani za maua ili kuendelea
kukijanisha nchi.
Naye, Afisa Mazingira Mwandamizi kutoka TANROADS, Julius Luhuro,
amesema kuwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) itaendelea
kukijanisha hifadhi za Barabara kwa barabara zilizopo na zinazojengwa
katika maeneo mengi nchini hususan Dodoma na kusisitiza kuwa mkakati
huo ni zoezi endelevu lengo ni kuhifadhi mazingira.