- Wafanyakazi wa mmoja wa mnufaika aliyekopa na kukataa kulipa wasambaza kimkakati kwa nguvu video yake mitandaoni, magazetini
- Ni ile akizungumzia uhuru wa mahakama kimuundo na kimfumo kuonyesha kuwa haiwezi kuingiliwa
- Inasemekana video iliyosambazwa ilitolewa na Jaji Mkuu baada ya Mfanyabiashara Rostam Aziz kuwatuhumu baadhi ya majaji wa Mahakama za Tanzania
- Wadau wawashangaa ukimya wa mahakama kiongozi wao mkuu akitumika kusafisha makando kando ya watu binafsi
NUKUU
‘’Mfano Jaji mmoja kati ya waliohukumu hizo kesi, kabla alikuwa wakili, Mwaka 2015 aligogembea ubunge kura za maoni CCM akashindwa, mwaka 2016 akateuliwa kuwa DED(Mkurugenzi wa Halmashauri) katika moja ya wilaya za mkoa wa Shinyanga, mwaka 2018 akateuliwa kuwa Jaji na baadae akapewa ahukumu kesi ya mabilioni ya pesa huku yeye mwenyewe kabla alishawahi kukopa Benki moja mkoani Mwanza mkopo ukamshinda nusura apigiwe mnada mali zake. Ana tuhuma kibao za kupiga madili kabla hajawa jaji unategemea nini kitatokea hapo, hii nayo inahitaji maelekezo kutoka kwa jaji mkuu kujua kuwa Uadilifu kwa mtu wa namna hii ni mdogo?’’. Aliongeza Nyange
Na. Mwandishi wetu
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mtumishi mmoja wa Serikali ambaye kwa sasa ni afisa Tarafa katika moja ya Tarafa za mkoa wa pwani aliyepata kuwa meneja katika moja ya vituo vya mafuta vya mmoja wa wafanyabiashara wanaolalamikiwa kukopa mabilioni ya fedha katika benki na kisha kukataa kulipa na kukimbilia mahakamani na mahakama kubariki kutokulipa kwao kwa kilichoitwa Ushahidi wa taarifa ya Benki kuu kuwaambia wasilipe mikopo ambayo haijasajiliwa (jina na tarafa anayofanyia kazi tunaihifadhi kwa sasa), amejikuta akisambaza video ya Jaji Mkuu nchini Profesa Ibrahim Hamis Juma kama sehemu ya utetezi kwa aliyekuwa bosi wake ambaye amekataa kulipa mkopo
Katika video inayoonekana kuhaririwa kimkakati ionekane kuwa Jji Prof. Juma alizungumzia suala la kutuhumiwa kwa baadhi ya majaji wa mahakama ya Biashara kushirikiana na wafanyabiashara kupindisha haki na kutoa hukumu zilizozua vichekesho kwa wataalam wa sheria na wafuatiliaji wa mambo ya mikopo
Video halisi na siku halisi ambayo Jaji mkuu alizungumza ni kuhusu uhuru wa mahakama na huku akionyesha ni namna gani mahakama yake ipo huru na kwamba hakuna kiongozi anayeweza kuiingilia kwa kutoa maagizo nani ashinde kesi gani na kwa nini jambo ambalo sio lililolalamikiwa
Taarifa zinasema kuwa jambo lililolalamikiwa ni tabia zisizo za kinidhamu na zisizo za kijaji za baadhi ya majaji walioamua kutoa hukumu zilizoliaibisha Taifa huku wenyewe wakiona wameyakomesha mabeki
Ni katika video hiyo iliyosambazwa kwa nguvu mitandaoni na kesho yake kuandikwa katika magazeti ya mtandaoni ya ukurasa wa mbele na nyuma tu yanayomilikiwa na waliokuwa wafanyakazi wa gazeti hili inaonyesha dhahili kuna njama na nguvu kubwa inayotumika kuficha ukweli kiasi cha kumtumia jaji mkuu ambaye kimsingi wala kauli yake haihusiani na kinachoelendelea kuandikwa na gazeti hili kuhusiana na mikopo chechefu
‘’unajua hawa jamaa ni bora wangetafuta mshauri mtaalam awape mbinu nini cha kufanya, Gazeti lenu limeandika mabenki na wakopaji kibao, tumeona benki kadhaa zikitajwa kama Azania, NBC, TADB, EXIM, CRDB, NMB, Stanbic na nyingine, na gazeti limetaja zaidi ya watu 20 kama sikosei kwenye orodha yake. Lakini wakamkurupusha yule wakili akaenda kuongea na waandishi akaharibu kabisa, bora angekaa tu kimya, wakaona haitoshi wakaisambaza video ya jaji mkuu akimjibu Rostam Aziz, napo ndipo wanaonyesha wazi nkuwa kuna kitu ndani yake sio bure’’. Ananukuliwa Ibrahim Nyange mtaalam wa mawasiliano mtandao
Anaongeza kuwa kama suala ni halali na wao wameshinda kihalali basi hakukuwa na haja ya wao kujitokeza na kugeuka watetezi wa mahakama na majaji ambao wengine miongoni mwao upatikanaji wao tu unatia mashaka
‘’wakili anayegeuka kuwa mtetezi wa jaji na kumsifia kuwa amefanya uamuzi bora tena wenye kurasa nyingi huu ni upungufu mkubwa wa kiueledi, kama ambavyo hawa vijana wamejikuta wakisambaza video ya jaji mkuu akizungumzia mambo mengine kabisa’’. Aliongeza
‘’hakuna sehemu watu wamelalamika kuwa mahakama haiku huru kimuundo, watu wanalalamika na matendo ya majaji, na watu wanawataja baadhi ya majaji kuwa ni tatizo kuanzia kupatikana kwako kuwa majaji, sasa kumuingiza jaji mkuu pale na mahakama kukaa kimya ni kama kwamba mahakama na waliosambaza video ile walikuwa nalao moja’’. Alisisitiza
Utafiti wa gazeti hili unaonyesha kuwa jaji huyo aliyetajwa nan Nyange kuwa tangu atoe hukumu tata zilizoifedhehesha nchi na mahakama ameshahamishwa vituo vya kazgi kadhaa akipelekwa mkoani Kigoma, kisha manyara na sasa amehamishiwa mkoani Morogoro ndani ya muda mfupi
Hayo yanajiri wakati Alhamis gazeti hili liliripoti kuwa Wakili mtetezi wa mikopo chechefu, Frank Mwalongo amewatia kitanzini wateja wake wa makampuni sita aliyoyataja kuwa anawatetea kwa kutumia utetezi unaovunja sheria za nchi katika udhibiti wa fedha za kigeni nchini unaowalazimu watu wote, taasisi zote wanaokopa pesa, mali, bidhaa au huduma kutoka nje ya nchi kusajili mikopo hiyo kwa Benki kuu ya Tanzania mara tu baada ya kukopeshwa na kutokufanya hivyo kunapelekea kutendwa kwa kosa la kisheria linalopelekea adhabu kali.
Kanuni ya fedha za kigeni nchini inayosimamiwa na sheria ya fedha za kigeni CAP 271 iliyotolewa na Gazeti la serikali kwa tangazo namba 294 na kuchapishwa tarehe 13 mwezi mei 2022 na marekebisho yake yaliyotolewa kwa tangazo la serikali nam,ba 622 lililochapishwa septemba mosi 2023 inakataza vikali wapokeaji kupokea mikopo kutoka nje ya nchi na kukwepa kuisajili na adhabu ya kufanya kosa hilo ni kulipa faini ya kiasi cha shilingi milioni nne kwa kilasiku ambayo mkopo huo umeishi bila kusajiliwa benki kuu au kufungwa jela kwa kipindi kisichozidi miaka 14 ama vyote kwa pamoja
Taarifa za zinasema kuwa kitendo cha watumiaji wa fedha zinazotoka nje kuzipokea na kutozisajili BOT, kinaashiria walakini wa matumizi ya fedha hizo kama zimetumika kwa matumizi gani kwa kuwa taarifa zake hazipo kwenye kumbukumbu za Taifa
Kwa mantiki hiyo basi, wakati wakili mwalongo anatamba na kufurahia wateja wake kukatazwa na BOT kulipa madeni waliyokopa kwa sababu mikopo yao haijasajiliwa BOT, licha ya kwamba kutokusajiliwa mikopo hakuzuii wakopaji kutimiza wajibu wa mkopaji wa ‘DAWA YA DENI NI KULIPA’ bali kumewaingiza matatani na kutakiwa kuweka wazi matumizi ya hayo mabilioni waliyopokea kutoka nchi za nje na kwanini walikwenpa kusajili mikopo hiyo BOT
Aidha kitendo cha wakili huyo kusema hadharani kuwa mikopo hiyo haijasajiliwa BOT ni kana kwamba amevivua nguo vyombo vya ulinzi na usalama vinavyojihusisha na udhibiti wa fedha zinazoingia na kutoka nchini ambavyo vina wajibu wa kisheria na kikanuni kufuatilia na kuzuia miamala yote inayowekewa mashaka na kutokusajili muamala BOT ni chanzo namba moja cha kutiliwa Mashaka kwa mpokeaji wa mualama huo
Bado haijafahamika ni kwa kiasi gani kitengo cha intelijensia ya Fedha cha serikali (Financial Intelligence Unit – FIU) kama kilifahamu juu ya kuingia na kutumika kwa miamala hii nchini ambapo wakili amethibitishia umma katika video yake ya dakika 13 aliyorekodiwa akizungumza na wanahabari kwamba mikopo ya wateja wake wote sita anaowatetea haijasajiliwa BOT
Ni kwa mashaka hayo pia ndipo Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini ‘TAKUKURU’ haijaweka wazi bado kama nayo imejiridhisha kuwa matendo ya wafanyabiashara kukwepa kusajili mikopo waliyoingiza kutoka nje ya nchi na kutumia mchezo huo kama kigezo halali cha kushinda kesi na Jaji wa mahakama ya biashara akijua kuwa kufanywa hivyo ni uvunjifu wa sheria nab ado akawapa ushindi watu waliotakiwa kuelekezwa kufuata na kuheshimu sheria za nchi, kuwa hakuna harufu ama dalili za rushwa ama njama za kutakatisha fedha
Katika kufahamu kanuni hizi, tunaarifiwa kuwa Nchini Tanzania, Benki Kuu ya Tanzania imepewa jukumu la kufuatilia pamoja na mambo mengine madeni ya nje ya sekta binafsi madeni ya nje yanafuatiliwa kwa uangalifu ili kuhakikisha kuwa uchumi una uwezo wa kutimiza majukumu yake ya deni.
Kanuni za Fedha za Kigeni 2022 zinatoa sharti la mkopo wowote wa kigeni kwa mkazi wa Tanzania unaozidi siku 365 usajiliwe na BoT na kupewa Nambari ya Usajili wa Deni (Debt Registration Nnumber)kwa kifupi DRN.
DRN ni alama ya kipekee ya utambulisho unaotolewa ili kutambua mikopo ya nje iliyosajiliwa katika hifadhidata ya mikopo ya nje katika BOT, zaidi ya hayo DRN itakuwa rejeleo la malipo, huduma ya deni na muamala mwingine wowote unaohusiana na mkopo huo.
Taarifa zinaeleza kuwa kwa kuwa mikopo yote ya makampuni yanayodai kushinda kesi kwa kigezo cha mikopo kutokusajiliwa BOT ilikuwa inaingia kwenye kanuni hii na inapaswa kusajiliwa tofauti na ilivyofanywa
Kanuni zinataka mara tu baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya mkopo, kampuni iliyokopa inapaswa kuwasilisha nakala iliyoidhinishwa ya makubaliano ya mkopo na hati nyingine zozote husika kwa benki yako ndani ya siku 14 kwa madhumuni ya usajili huku Benki yake ikitakiwa kuwasilisha hati hizo kwa BoT ndani ya siku 7 baada ya kuzipokea kutoka kwa kampuni yako kwa ajili ya kutoa Nambari ya Usajili wa Deni.
Kwa hivyo, kwa kuzingatia hali aliyoitaja wakili mwalongo na kuzingatia mahitaji ya kanuni ni wazi kuwa yeye na benki za wateja wake wamekiuka Sheria ya Fedha za Kigeni na Kanuni na hivyo kustahili kutozwa kwa adhabu na BOT.
Utaratibu huo sio tu kwa kampuni kama mkopaji bali pia sheria inatoa adhabu kwa benki husika kwa kupokea mapato ya mkopo na kushindwa kuwasilisha nyaraka zinazohitajika BoT kwa usajili kwa mujibu wa matakwa ya sheria.
Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa kanuni za Fedha za Kigeni za 2022 zimerekebishwa tena mwaka 2023 ambapo awali, adhabu ya TZS 1M ingetozwa kwa kampuni husika kwa kila siku mkopo ambayo mkopo unakaa bila kusajiliwa hata hivyo, kwa marekebisho ya sasa, adhabu imepanda na kuwa TZS 4M au kifungo kisichozidi miaka 14 au vyote kwa pamoja.
Mbali na hayopo wakati wa kusajili mkopo na BoT, mambo kadhaa yanapaswa kuzingatiwa ;kwamba Kanuni zinataka mkataba wa mkopo usiwe na masharti na masharti yasiyofaa ikiwa ni pamoja na, lakini sio tu, kwamba kiwango cha riba na malipo mengine ya mkopo wa nje lazima. kuakisi hali ya soko iliyopo kwa sarafu husika ya kukopa. Pia ni sharti kwamba mkataba wa mkopo usijumuishe masharti ambayo yanamtaka mkopaji kufungua akaunti ya fedha za kigeni nje ya Jamhuri ya Muungano. Endapo mkataba wa mkopo una masharti hayo, BoT haitasajili mkopo huo.
Aidha, kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na BoT mkataba wa mkopo unapaswa kuwa na angalau taarifa zifuatazo: Jina la mkopeshaji na mkopaji; Maelezo ya mawasiliano kama vile anwani ya posta, nambari ya faksi, nambari ya simu na anwani halisi ya mkopeshaji na mkopaji; Kiasi cha mkopo na sarafu ya manunuzi; Madhumuni ya mkopo; Kiwango cha riba kinachotumika; Kipindi cha ukomavu wa mkopo; Ratiba ya marejesho ya mkopo yenye tarehe zilizoonyeshwa wazi; Vifungu vya matukio ya kasoro na matokeo yake; Kifungu kinachoonyesha sheria inayotumika Malipo yanayoonyesha kiasi, tarehe ya malipo na sarafu; Malipo ya huduma ya deni yanayoonyesha mtaji na riba iliyolipwa na tarehe za thamani; Malipo mengine yanayolipwa, yaani, ada ya ahadi, ada za usimamizi n.k; Maelezo juu ya uboreshaji wa mkopo au kughairiwa; na Maelezo juu ya urekebishaji au ufadhili wa mkopo.
Juzi katika utetezi wake kwa waandishi wa Habari wakili wa wafanyabiashara 6 waliofungua kesi za aina moja kwenye mahaka wote wakigoma kulipa mikopo waliyokopeshwa na mabenki kwa kisingizio cha kuwa ni mikopo ya kimataifa, alisema kuwa wateja wake hawakulipa mikopo hiyo kutokana na kupewa barua na Benki kuu ya Tanzania ikiwaelekeza kuwa Mikopo ambayo haikusajiliwa nchini haipaswi kulipwa
Kauli ya wakili huyo aliyejizolea umaarufu kama Mzee wa Mikopo chechefu, imeibua mshangao kwa watu wengi kwani haikutarajiwa mtu anayeaminika kuwa mweledi kama yeye kutoa utetezi mwepesi namna hii
Utetezi wake umeibuka baada ya siku moja kabla gazeti hili kuripoti kuwa Jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kukaribisha na kuhamasisha uwekezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza nchini unaelezwa kutiwa kigingi na tabia chafu inayozidi kuota mizizi ya baadhi ya wafanyabiashara wakubwa kushirikiana na baadhi ya majaji wa mahakama kuu wasio waaminifu kuyatapeli mabenki ya ndani na nje ya nchi kwa na hivyo kuwanyima fursa wafanyabiashara wadogo na wakati kushindwa kuaminiwa na kupata mikopo.
Orodha ya wafanyabiashara wanaotumia mahakama kutapeli na kudhulumu mabenki iliyofanyiwa uchunguzi na kuthibitishwa na gazeti hili, inaonyesha kuwa wengi kati ya wafanyabiashara hao wanajihusisha na biashara za Mafuta na ushafirishaji ambapo wastani wa shilingi za kitanzania Trilioni 1.3 wamekopa katika benki mbalimbali za ndani nan je ya nchi na kukataa kulipa kisha kukimbilia mahakamani ambako pia wanadaiwa kupata ushindi kwa njia zisizo za kawaida
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wafanyabiashara hao wanaoheshimika nchini wakionekana machoni mwa watu kuwa ni matajiri na wengine wakijionyesha kama wacha Mungu na wenye kumuogopa Mungu huku wengine wakijinasibu kama wana michezo na wawekezaji wakubwa wanaitumia mahakama hasa mahakama ya biashara kama kichaka chao cha kufanyia uhalifu huo wa kimkakati
‘’hebu fikiria, mtu amekwenda TADP amekopa bilioni 40, akaenda Azania benki akakopa bilioni 70, hajaishia hapo akaenda Equity benki akakopa bilioni 110, halafu akapanda ndege hadi ujerumani akavidanganya baadhi ya viwanda vya huko kuwa anaenda kuwekeza mafuta Kahama, nako wakamkopesha mali na mtaji wa zaidi ya bilioni 220, halafu anakataa kulipa mkopo makusudi kwa kukimbilia Mahakamani na Jaji anampa ushindi bila kuzingatia Ushahidi na ukweli kuwa hizo bilioni 220 za ndani na bilioni 220 alizochukua ujerumani zote kwa pamoja zinaingia kwenye deni la Taifa na kukataa kwake kulipa mkopo kunatunyima fursa sisi wafanyabiashara wadogo kuaminiwa’’. Anasema Christopher Kabison mfanyabiashara wa vifaa vya simu Kariakoo
Kabison anaongeza kuwa kama Serikali haitachukua hatua za haraka kuingilia kati hali hii basi jitihada za Rais kutaka mabenki yakopeshe wafanyabiashara kwa riba nafuu zitabaki kuwa ndoto kwani hakuna benki itakayokuwa tayari kuendelea kupoteza mitaji yake huku mahakama zinazotarajiwa kuwa ni sehemu ya haki zikitumika kuhalalisha uchafu huo
‘’juzi nilikuwa napitia hukumu za mahakama, nimeshuhudia jaji mmoja amempa ushindi Stati oili ambaye alikopa dola milioini 26 equiti benki halafu akakataa kulipa, ukizipitia hizi hukumu unaweza ukajiuliza kama jaji wakati anatoa hukumu alikuwa sawa sawa ama ameonja kidogo..na jaji huyo huyo akahukumu hukumu kama hiyo kwa kampuni ya derina ambayo ilikopa zaidi ya bilioni 40 na kukataa kulipa. Sasa hapa tukisema mahakama inatumika kuhalalisha ujambazi dhidi ya watanzania tutakuwa tumeionea’’. Aliongeza Kobisoni
Kwa mujibu wa taarifa na nyaraka ambazo gazeti hili linazo zinaonyesha kuwa miongoni mwa makampuni yanayoongoza kufilisi mabenki huku wakitumia mahaka ni pamoja na KOM GROUP ambayo imeweka kibindoni zaidi ya bilioni 440 na kukataa kulipa na kuziacha solemba benki za TADB,AZANIA pamoja na EQUITY sambamba na ujerumani
Wengine wanaoongoza genge la kukwamisha jitihada za Rais Dkt. Samia katika kukuza mitaji ya wafanyabiashara wadogo na wa kati kwa kukataa kulipa mikopo na kisha kukimbilia mahakamani na mahakama kuwapa hukumu za ushindi ni pamoja na kampuni ya TSN iliyozidhulumu benki za NMB na Equity, Derina Group iliyozidhulumu benki za CRDB na KCB huku BIG BON ikitajwa kuidhulumu benki ya NBC kama ambavyo Masasi construction inavyopambana kuidhulumu benki ya Equity kwa kutumia mahakama
Sambamba na kampuni hizo, nyingine ni Global Agency, State Oil inayomilikwa na Nilesh Suchak kama ilivyo kwa NAS HAULIERS na Continental reliable zinazotamba kuwadhulumu CRDB, NMB, NBC,EQUITY, KCB na nyinginezo
Ikiwa kitendo hiki cha wafanyabiashara hawa wakubwa kukopa na kuacha kulipa madeni kisha kukimbilia mahakamani na mahakama kuwapa ushindi kitaachwa kuendelee kuota mizizi kitapelekea Taifa kuwa na kikundi ‘GANG’ cha wafanyabiashara wanaoutawala Uchumi wa nchi na hivyo kuhatarisha amani ya Taifa
Kuwepo nje ya mzunguko wa benki hizi mabilioni hayo ya shilingi ni kiashiria kibaya katika ukuzaji wa Uchumi huku Gavana wa benki kuu akiombwa kuchukua hatua za haraka kuingilia sintofahamu hii inayozidi kushika kasi
‘’kama BOT hawatakuwa serious na kuingilia kati kunusuru hili jambo, benki zitafungwa hizi, ama zisipofungwa basi Uchumi utahama kutoka kuwa rasmi na kuwa Uchumi wa kihuni unaondeshwa na wahuni, lazima benki kuu iingilie kati haraka’’. Alisema Juma Hamad mchambuzi wa masuala ya kiuchumi
Aliongeza kuwa katika Taifa lolote ambalo linaheshimu utawala wa sheria, ni nadra kwa wafanyabiashara kukopa halafu kukataa kulipa makusudi kisa tu kuna mahakama, hali hii inaweza kushawishi na wafanyabiashara wadogo nao kukataa kulipa na ikiwa wakashindwa mahakamani basi itasababisha hali ya sintofahamu
Gazeti hili linaendelea na jitihada za kuwatafuta wote waliotajwa kukapua mabilioni hayo na kukataa kulipa huku simu zao za mkononi zikiita bila kupokelewa.