NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt. Mohamed Said Dimwa, amesema chama hicho kinaridhishwa na juhudi za Serikali zote mbili katika kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema muungano huo unaendelea kuvunja rekodi ya kudumu kwa miaka mingi zaidi ya miungano ya nchi nyingine barani Afrika na duniani kwa ujumla, kutokana na dhamira ya dhati ya kuasisiwa kwake.
Dkt Dimwa aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu, ambapo amesema juhudi hizo zimeleta Mapinduzi ya kiuchumi,kiuchumi,kijamii na kuimarisha diplomasia ya kikanda na kimataifa.
Alifafanua kuwa Muungano huo ulioasisiwa Aprili 26, 1964 na hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Amani Karuma, umetimiza miaka 60 ukiwa na mafanikio ya wazi yanayozinufaisha nchi zote mbili Zanzibar na Tanzania Bara.
Alisema kuimarika kwa Muungano huo ni kutokana na mchango wa Viongozi wa awamu mbalimbali katika Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kusimamia, kudumisha na kuimarisha umoja, amani na mshikamano.
Dkt. Dimwa aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa ushirikiano mzuri na kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha Muungano huo unaendelea kuwa na tija kwa nchi zote mbili.
“Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 ibara ya 246 (b), Chama Cha Mapinduzi kimeelekezwa kudumisha Muungano hivyo hiki ni kipaumbele kwetu na lazima tusimamie kwa vitendo na gharama yoyote.”
“Hakuna mwananchi wa Zanzibar na Tanzania bara asiyenufaika na Muungano huu kwani umegusa kila sehemu kuanzia katika asili zetu, maisha yetu ya kila siku ya kutafuta riziki, fursa za kiuchumi na kijamii pamoja na ukuaji wa demokrasia inayotegemea utashi wa kisiasa.”, alisema Dkt. Dimwa
Alisema wapo baadhi ya wanasiasa na wasomi wanaoukosoa Muungano huo kutokana na utashi wa itikadi za vyama vyao, bila kuridhia hoja ya kutafusa suluhu ya kumaliza kasoro ndogondogo zilizopo katika Muungano huo.
Pamoja na hayo, alisema watu wanaoukosoa Muungano huo wajue kwamba haukuundwa kwa msukumo wa kisiasa bali ni kutokana na maslahi mapana ya kiuchumi na kijamii, yaliyolenga kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.
Alisema Zanzibar imeendelea kuimarika kutokana na uwepo wa taasisi za Muungano zinazotoa huduma bora kwa wananchi wote bila ubaguzi.
Dkt. Dimwa alisema Chama Cha Mapinduzi kinaamini kuwa uimara wa uchumi na maendeleo endelevu ya kuivusha Zanzibar kufikia katika hadhi ya nchi za visiwa zilizoendelea kiuchumi, ni kuimarika kwa tunu ya Muungano huo.
Katika hatua nyingine Dkt. Dimwa aliwataka wananchi bila kujali tofauti zao za kisiasa waendelee kuunga mkono mambo mema yanayotekelezwa chini ya Muungano huo, ambao ndio chimbuko la uwepo wa sera nzuri za kuimarisha uchumi wa nchi.
Alichambua baadhi ya mafanikio, changamoto, dhamira ya CCM Zanzibar na muelekeo wa muungano kwa miaka ijayo chini ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi katika nyanja za uchumi, kijamii na kisiasa.
Mafanikio
Alisema tangu kuasisiwa kwa Muungano huo mwaka 1964 Zanzibar iliendelea kubaki kama nchi inayojitawala na kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa baadhi ya mambo waliokubaliana Kikatiba.
Dkt.Dimwa, alieleza kuwa wananchi wa pande zote mbili wamekuwa huru katika kutembea na kuishi sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatua ambayo ni fursa kubwa kwa wananchi wa Zanzibar.
Alisema kuimarika kwa undugu, amani, utulivu, mshikamano baina ya wananchi wa pande zote mbili ni hatua kubwa ya mafanikio kwani hakuna kiashiria chochote cha uwepo wa migogoro ya kijamii inayoweza kuingiza nchi katika machafuko.
Pamoja na hayo Dkt.Dimwa, alisema kuimarika kwa fursa za ajira na biashara ni sehemu ya mafanikio ya uwepo wa Muungano huo.
Mafanikio mengine ni utatuzi wa changamoto za Muungano ambazo kwa miaka mingi zilikuwa zikilalamikiwa ambapo kwa sasa zimebaki chache na muda wowote zitatatuliwa zote.
Dhamira ya CCM Zanzibar.
Dkt.Dimwa, alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kitaendelea kusimamia misingi yake ya kuendeleza utawala wa haki, sheria,uwajibikaji na utawala bora ili wananchi waendelee kunufaika na matunda ya Muungano.
Alisema ndani ya Muungano huo CCM Zanzibar itahakikisha inasimamia kwa vitendo sera zake ili ziwe chachu ya kunufaisha wananchi wa visiwa vya hivyo vya kihistoria.
Aliweka msisitizo kuwa ataendelea kusimamia kikamilifu Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 pamoja na dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 kwa kuhakikisha zinakuwa ni vipaumbele vya kuchochea maendeleo ya nchi.
Muelekeo wa muungano kwa miaka ijayo
Dkt.Dimwa, alisema kutokana na juhudi za Serikali katika kusimamia masuala yote ya Muungano upo muelekeo mzuri na matumaini yanayodhibitisha dhamira.
CAPTION
Picha no.005- Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, akizungumza katika moja ya Mkutano wa CCM Zanzibar.
Inbox