Kituo cha Jamii Partners Group (JPG) POLYCLINIC kilichopo Chang’ombe mtaa wa keko bora ambacho kuwepo kwake ni kutokana uwezeshaji wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia mpango wa mikopo ya 10% ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa wakina mama, vijana na watu wenye ulemavu leo Machi 21, 2024 kimetoa huduma bure kwa wazee ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na serikali kwa ujumla.
Akizungumza wakati alipotembelea kituo hicho na kushuhudia namna gani wazee wakipatiwa huduma Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Temeke amesema kuwa wajibu wa serikali ni kuhakikisha inalinda afya za wananchi wake.
“Vijana hawa walimaliza chuo cha Muhimbili wakaandika andiko lao kuomba kuwezeshwa na halmashauri kupitia mikopo ya 10% iliwawezesha vijana hawa Shilingi Milioni 200 na hii imekuwa mchango mkubwa katika yote myaonayo hapa, na kila baada ya miezi mitatu wameona watoe huduma hii bure kwa kundi muhimu la wazee kama sehemu ya shukrani wanayotoa vijana hawa kwa Mheshimiwa Rais na jamii”. Alisema Ndg. Mabelya
Nae Daktari Thomas Ngerera, mwenyekiti wa kikundi cha Jamii partners group ametoa shukrani zake kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na uongozi wa Manispaa ya Temeke kwa kuwawezesha kufungua kituo hicho huku akiwakaribisha wananchi kujitokeza katika kituo hicho kwa kuwa wana vifaa vya kisasa na wanatoa huduma bora za kibingwa.
Kwa upande wa Bw. Edward Mwainyakule, mmoja wa wazee aliepatiwa huduma kituoni hapo amesema jambo hilo kwao limekuwa jema na limegusa maisha yao.
“Mkurugenzi sisi hatuwezi kumfikia Mheshimiwa Rais ila tunaomba utupelekeee shukrani kwa mheshimiwa na tunamuombea Mungu amjalie afya njema azidi kuwawezesha wananchi wake hasa vijana ambao moja kwa moja wanakwenda kuokoa maisha yetu sisi wazee” Alisema Bw. Edward.
Kwa siku hiyo kituo hicho kiliweza kuhudumia takribani wazee 100 ikiwa pamoja na kuwapatia matibabu yaani vipimo na dawa bila malipo yoyote.