Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa siku nne kwa Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) nchi nzima kufanya tathmini na ukaguzi wa madaraja, makalvati na barabara kuu zote ambazo zimekuwa zikifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara na kuwasilisha taarifa hizo kwa wakuu wa Mikoa ili ziweze kuchukuliwa hatua ya haraka.
Agizo hilo amelitoa mkoani Lindi Machi 5, 2024 kutokana na taarifa ya Mamlaka ya hali ya hewa kuhusu maoteo ya mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali na kuathiri miundombinu ya barabara, madaraja na makalvati kwa baadhi ya maeneo.
“Nielekeze hadi kufika Machi 9 Mwaka huu kila Meneja wa Mkoa wa TANROADS na timu yake wakabidhi taarifa ya hali ya barabara na maeneo ya hatari yanayoweza kujitokeza katika madaraja na makalvati ili Serikali iweze kuchukua hatua za haraka”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa amewapongeza Wakuu wa Mikoa yote nchini kwa kuendelea kusimamia Sekta ya Ujenzi katika mikoa yao na kuwaomba kuimarisha ushirikiano katika kipindi hiki cha changamoto za Mvua za El-Nino.
Bashungwa ameiomba Wizara ya Fedha kuendelea kupeleka fedha za dharura katika mikoa yote ili Mameneja wa TANROADS waweze kuendelea kuchukua hatua pale ambapo changamoto za Mvua za El – Nino na mawasiliano ya barabara yanapokatika.
Aidha, Bashungwa ametoa pole kwa wananchi waliokwama katika eneo la Nangao ambapo sehemu ya daraja na makalvati katika barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi zimekatika na kufunga mawasiliano ya barabara kwa wananchi wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kwa saa kadhaa.
Bashungwa amewasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika maeneo yao kama walivyotangaziwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa pindi wanapoona maji mengi yanakatiza juu ya barabara na madaraja ili kulinda usalama wao na vyombo wanavyovitumia.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack, ameomba fedha za dharura za matengenezo ya barabara kufika kwa haraka ili ziweze kunusuru barabara zilizoathiriwa na mvua na zile zilizofunga hasa kwa wananchi wa Wilaya ya Liwale ambao wamekuwa kisiwani hawawezi kutoka wala kuingia.