Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) amewataja bodaboda kama kundi linaloongoza kukiuka sheria barabarani huku wakijichukulia sheria mkononi akihusisha na tukio lilotokea siku ya jana Februari 27, 2024 Wilayani Korogwe Mkoani Tanga walivyochoma basi la abiria.
Akizungumza leo Februari 28, 2024 kwenye Ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa katika Kijiji cha Komuge Wilayani Rorya Mhe. Sagini alisema kuwa, bodaboda wengi wao wamekuwa barabani wakiendesha vyombo vyao kwa mwendo mkali na pia hawafuati sheria za barabarani hali inayopelekea kusababisha ajali zinazowaumiza wenyewe na watu wengine.
“Bodaboda ni ajira lakini hawajihurumii wanaendesha mwendo mkali wakiwa wametumia vilevi wakiingia barabarani wanaona mwendo wa kawaida kumbe ni hatari ukienda Dar es Salaam pale MOI wengi wamekatwa miguu na chanzo chake ni mwendo mkali na jana kule Korogwe wamejichukulia sheria mkononi naomba waache hii tabia mara moja” Alisema Sagini.
Aidha, Mhe. Sagini aliwataka wananchi wa Rorya kuendelea kufanya shughuli za uzalishaji mali bila uoga kwani Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaelekeza vyema kupitia Jeshi lake la Polisi limeimarisha doria ziwani na nchi kavu Wilayani Rorya pamoja na kudhibiti uhalifu uliokuwepo hapo awali ambao ulikwamisha shughuli mbalimbali.
Hata hivyo, Mhe. Sagini ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusikia ombi la Mbunge wa Jimbo la Rorya Mhe. Japhari Chege na kuridhia kutoa fedha kwa ajili ya Ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wanamaji ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandishi Hamad Masauni pia alimulekeza IGP Camillus Wambura na hatimaye utekelezaji umeanza.