Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameendelea na ziara ya kukagua vyanzo mbalimbali vya uzalishaji umeme nchini ambapo leo amekagua Bwala la kuzalisha umeme la Kidatu ( 204 MW)
na Kihansi ( 180 MW) mkoani Morogoro.
Lengo la ziara hiyo ni kujihakikisha hali halisi ya uwepo wa maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme nchini pamoja kukagua mitambo ya kuzalisha umeme.
Baada ya kukagua Bwawa la Kidatu na Kihansi pamoja na mitambo ya kuzalisha umeme, Dkt. Biteko amesema kuwa, mabwawa ya Mtera, Kihansi na Kidatu yana maji ya kutosha kuweza kuzalisha umeme huku tumaini jingine kubwa likiwa ni umeme kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao muda wowote unatarajia kuingiza megawati 235 katika Gridi ya Taifa.
“Nafurahi kuwaambia kwamba changamoto tuliyonayo ya umeme imefika mwishoni sana hivyo Watendaji wa TANESCO ni wakati pia wa kushughulikia changamoto nyingine ambazo baadhi ya wananchi wanazipata ikiwemo ya kutotoa huduma kwa wakati na pia ukarabati wa mitambo ufanyike kwa wakati.” Amesema Dkt. Biteko
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amekataza Watendaji wa TANESCO kwenda likizo kipindi cha changamoto za umeme na badala yake wajikite katika kutatua changamoto hizo na katika hilo ameagiza Uongozi wa juu wa TANESCO kumchukulia hatua za kinidhamu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro ambaye amechukua likizo katika kipindi hiki ambacho Serikali inapambana kutatua changamoto za umeme.
” Niliposema TANESCO hamtolala kipindi cha mgawo wa umeme nilimaanisha kuwa kila mtu awepo kwenye kituo chake cha kazi, sisi wenyewe tunahangaika kutatua changamoto za umeme halafu baada ya kufika hapa nimeshangazwa kuona Meneja wa Mkoa ambaye alipaswa kuwepo kituoni wakati wa changamoto amechukua likizo, hivyo nimewaelekeza watendaji wa TANESCO hakuna kwenda likizo kuanzia sasa.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kila rasilimali kwa ajili ya kuwapatia watanzania umeme hivyo viongozi na watendaji wa Wizara hawatakuwa kikwazo cha kumkwamisha.