NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Boniface Gissima Nyamohanga, pamoja na dereva wake, Muhajiri Mohammed Haule, waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea usiku wa kuamkia jana katika eneo la Bunda, mkoani Mara.
Kupitia salamu zake, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo hivyo na kueleza kuwa ni pigo kubwa kwa taifa, hasa katika sekta ya nishati ambayo marehemu Mhandisi Nyamohanga alikuwa akiitumikia kwa bidii na weledi mkubwa.
ìNatoa pole kwa familia za marehemu, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, watumishi wa TANESCO, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu mzito,î alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amewaombea wafiwa wote wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ibada katika kipindi hiki kigumu, akimuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.
Mkurugenzi huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia leo Aprili 13, 2025 katika ajali iliyotokea wilayani Bunda mkoani Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo ameeleza kuwa limetokea kati ya saa 6 hadi 7 usiku wa kuamkia leo.
“Ni kweli tukio lipo na amefariki dunia ila wasiliana na RPC atakuwa na taarifa kwa kina,” amesema Mtambi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema ni baada ya gari la Mkurugenzi lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Bunda kugongana uso kwa uso na lori.
Amesema chanzo cha tukio hilo ni dereva wa gari lililokuwa limembeba Mkurugenzi aina ya Toyota Land Cruiser kumkwepa mwendesha baiskeli kisha kupoteza mwelekeo na kugongana na lori.
“Tukio limetokea Bunda saa 7.30 usiku baada ya dereva wa gari aina ya Toyota Land Cruiser iliyombeba mkurugenzi kumkwepa mwendesha baiskeli na kugongana uso kwa uso na lori kisha kupelekea vifo vya dereva na bosi wake,” amesema Kamanda Lutumo
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mara, Nickson Babu amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda huku wakisubiri taarifa zaidi kuhusu taratibu nyingine.
Wakati huohuo Jeshi la Polisi mkoani Mara, imetaja chanzo cha ajali ya Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamohanga, kuwa ni uzembe wa dereva wa kiongozi huyo akimkwepa mwendesha baiskeli.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda huyo amesema gari la Mkurugenzi huyo lilikuwa linaendeshwa na Muhajir Haule (61).
Akielezea tukio hilo amesema limetokea majira ya 07:30 usiku wa kuamkia Aprili 13, 2025 kwa magari kugongana uso kwa uso.
ìMagari Toyota Land Cruiser yenye namba T.385 EHM na lori aina ya SCANIA lenye namba za usajili T.396 EHR likiwa na tela lenye namba za usajili T.833 ACD na kusababisha vifo vya watu wawili,” amesema Lutumo.
Kamanda Lutumo amesema gari na T385 EHM Toyota Land Cruiser ilikuwa ikitokea Mwanza kwenda Bunda iligongana uso kwa uso na lori lenye namba za usajili T.396 EHR Scania likiwa na tela lenye namba za usajili T.833ACD
“Waliofariki dunia katika ajali hiyo ni Mhandisi Gissima Nyamo-Hunga (56) Mkurugenzi wa TANESCO nchini, na Dereva wake Haule wakazi wa Dar es Salaam,” amesema.
Aidha, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari dogo kumkwepa mwendesha baiskeli na kushindwa kulimudu gari lake na hivyo kugongana uso kwa uso na lori alilokuwa anapishana nalo.
Aidha, Kamanda Lutumo amesema baada ya ajali hiyo kutokea dereva wa lori alikimbilia kusikojulikana na kwamba miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari) katika hospitali ya DDH wilayani Bunda.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi licha ya kukiri kutokea kwa ajali hiyo ametoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki juu ya marehemu waliotokana na ajali hiyo.