Katika Kukuza Sekta ya Utalii nchini Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imepokea wageni 10 maarufu kutoka nchini Oman (Dream Team Explorers) ambao watatembelea, kuona na kutangaza vivutio vinavyopatikana mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana tar. 16 Apr 2024 , Jijini Dar es Salaam Meneja Habari na Uhusiano kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ndg. Samuel Nsyuka amesema kuwa “ugeni huu ni zao jipya la utalii ambapo wapo Takribani wageni 10 kutoka nchini Oman, watakuwa na magari yao yenye Plate namba za Nchini kwao hivyo watazunguka kwenye vivutio vyote ambavyo vinapatika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo hifadhi ya Taifa ya Kitulo, Ziwa Ngosi na Hifadhi ya Msitu Asili wa Mlima Rungwe”
Hata hivyo Meneja Habari na Uhusiano kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ndg. Samuel Nsyuka ameendelea kuwasisitiza Watanzania kujumuika nao pamoja kwani hayo ni matokeo ya filamu ya The Tanzania Royal Tour ndiyo imeweza kuwavutia wageni hao 10 maarufu katika sekta ya utalii katika nchi za Kiarabu kuja kujionea fursa mbalimbali katika zao la utalii nchini.
Naye Mwakilishi wa Wageni hao maarufu kutoka nchini Oman (Dream Team Explorers) Ndg, Abdullah AL Rabii ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan katika uwekezaji sekta ya Utalii sambamba na Wao kama Wadau wa Utalii Duniani wamepanga kumpatia Tuzo ya Heshima Kama Mdau Namba Mmoja wa Utalii Afrika.