Zimebaki siku tatu, kila Mtanzania mwenye sifa nenda kapige kura

0

Na Mwandishi Wetu

Zoezi la kampeni  linaelekea ukingoni zikiwa zimebaki siku tatu kufikia siku ya kupiga kura, huku wagombea kutoka vyama mbalimbali vya siasa wakizunguka kwa ajili ya kutangaza Ilani  na Sera za vyama vyao sambamba na kuomba ridhaa kwa wananchi ili waweze kuchaguliwa katika uchaguzi Mkuu Jumatano.

Sisi Jamvi la Habari tunapenda kuwakumbusha wananchi kuwa suala la kupiga kura ni wajibu wa kila mtanzania mwenye sifa kwa mujibu wa sheria na Katiba.

Katika kipindi hiki cha  kampeni tumeona kiu ya Watanzania katika kushiriki kampeni za uchaguzi, ambapo wamekuwa  wakijitokeza kwa wingi katika kampeni za wagombea mbalimbali, hii inaonyesha jinsi gani Watanzania walivyo na hamu ya  kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo, japokuwa  historia ya ushiriki katika upigaji kura katika miaka ya nyuma imeonesha mwamko mdogo sana.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2010 idadi ya wapiga kura waliojiandikisha ilikuwa 20,137,303, lakini waliopiga kura mwaka huo walikuwa 8,626,283 sawa na asilimia 42.84 . Mwaka 2015 zaidi ya  Watanzania milioni 23 walijiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, huku Watanzania 15,589,639  pekee ndio waliopiga kura ambayo ni sawa na asilimia 67.34. Hii inaonyesha jinsi gani watu wanavyopuuzia suala la upigaji kura na kupoteza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka. Tatizo hili la watu kutojitokeza kwa wingi kupiga kura linatokana na kukosa elimu ya uraia  na elimu ya mpiga kura.

Hivyo basi tunahimiza wananchi kuhudhuria na kuzingatia mafunzo ya uraia pamoja na elimu ya mpiga kura ambayo hutolewa na asasi za kiraia na NEC ili waweze kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongizi wanaotaka wawaongoze katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Tunawahimiza pia kuwachagua viongozi kwa kuangalia ubora wa sera za chama pamoja na uwezo binafsi wa mtu katika kusimamia mambo ya jamii kuliko mambo yake binafsi. Hii itasaidia kupata viongozi wanaowajibika kwa jamii zaidi kuliko kutumikia matumbo yao na kuwasahau kuwa wametumwa na wananchi kufanya kazi.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here