Zanzibar ni JPM na Dk. Mwinyi

0

  >> Wananchi watoa maoni na kueleza bayana walivyo na imani nao

 >>Kishindo cha Magufuli kuleta nidhamu serikalini kinawavutia wapiga kura

 >> Dk. Mwinyi ‘CV’ ya kuiongoza Wizara ya Ulinzi kwa weledi yageuka gumzo

Na Hafidh Kido, Zanzibar

TOFAUTI na miaka yote ya uchaguzi tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, visiwa vya Zanzibar vimekuwa na utulivu wa hali ya juu huku wananchi wakiimba majina mawili ya wagombea.

Ni Dk. John Magufuli mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Dk. Hussein Mwinyi nyegombea upande wa Zanzibar kwa chama hicho.

Jamvi la Habari lilipata nafasi ya kusikia maoni ya wananchi juu ya hali halisi ya uchaguzi, ambapo wengi waliweka wazi kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kwa utendaji wao mkubwa kuhudumia wananchi kwa miaka mitano iliyopita.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema Dk. Mwinyi amekuwa mgombea wa kipekee katika miaka 25 iliyopita kwa kuwa ni kijana aliyezaliwa baada ya mapinduzi ya mwaka 1964.

Vuai Nassor Suleiman, alisema imani kubwa ya Wazanzibari ni namna Dk. Shein alivyovibadili visiwa hivyo kwa kufanya miradi mikubwa ya kimaendeleo bila kupiga kelel.

“Mimi ninavyomfahamu Dk. Shein kwanza mambo yake alikuwa akifanya kimya kimya, lakini yote aliyofanya yalituridhisha hata mtu asiye na akili anafahamu alichofanya, jinsi alivyotujengea barabara, shule za ghorofa na kutuletea maji,” alisema Suleiman na kuongeza:

“Kwa kweli tulikuwa tuko nyuma kwa sasa tuko mbele, Dk. Hussein Mwinyi kwa kuwa ni kijana tunaamini atafanya makubwa zaidi, ndiyo maana kura zetu zote tutampigia yeye ili atuvushe kutoka hapa.”

Kwa upande wa Dk. Magufuli alisema:  “Dk. Magufuli naona ushindi wake ni mnono mno, tukiacha mambo aliyoyafanya wazi hata sisi Wazanzibari tunauona utendaji wake ameifanikisha Tanzania, sisi Wazanzibari tunamkubali sana na hata hadi zake za kutujengea mandari kubwa zinatuongezea imani kwake.

“Ni mkweli na zaidi kilichotufurahisha katika corona alijiamini, hatuwezi kumpata rais kama huyu na anayemchukia Dk. Magufuli alegee tu hana uwezo, hakuna wa kushindana naye watu wanajidanganya tu nafsi zao.”

Naye, Mauled Hassan kutoka Bububu visiwani humo alisema atamchagua Dk. Mwinyi kwa kuwa anaamini ni mchapakazi hodari.

“Kwa namna alivyotuambia kazi zake katika Wizara ya Ulinzi huenda wengi hawaufahamu, lakini tunaamini tukimpa fursa atafanya zaidi kama asemavyo kwenye kaulimbiu yake ‘Yajayo ni neema tupu.’ Tunaamini itakuwa neema kweli kwa kuwa ukweli wake na uthubutu umejidhihirisha kwenye wizara alizozisimamia kwa mika 20,” alisema Hassan.

Aidha, akizungumzia utendaji kazi wa Dk. Magufuli alisema: “Kila Mtanzania anafahamu utendaji wake wa kazi na maboa aliyoyafanya kukuza uchumi na miradi mikubwa ambayo itachukua muda mrefu kuyazungumza hapa. Watu wajipange tumchague tena Dk,. Magufuli na tumchague Dk. Mwinyi tuwe na imani nao kwa miaka mitano ijayo.”

Kwa upande wake Fatma Mussa Abdallah alisema: “Kiufupi Zanzibar imepiga hatua kubwa ukilinganisha na nyuma, maendeleo yapo wazi majumba makubwa yamejengwa, tunategemea ajaye aendeleze palipoishia.

“Uwezo wa Dk. Mwinyi ni mzuri hatujawahi kusikia kashfa zake, kuongoza ni weledi tangu alipoanza chini na nina uhakika yeye anaweza kuendesha nchi,” alisema Fatma.

Katika hatua nyingine alizungumzia shutuma anazotupiwa Dk. Mwinyi kuwa baba yake Mzee Ali Hassan Mwinyi alikuwa rais wa Zanzibar na sasa mwanaye anagombea urais huo ni kama usultani.

Alisema, hawezi kuzungumzia shutuma hizo kwa kuwa hazina maana yoyote, kinachotazamwa ni uwezo wa mgombea na si historia yake. Kwa kuwa hata kama babu yake na baba yake walikuwa viongozi kinachoangaliwa ni sifa za kuwa rais ambazo anazo kikatiba.

“Dk. Mwinyi hata kama baba na babu zake waliongoza nchi yeye anatosha kwa kuwa anao uwezo, kama angekuwa hana uwezo hapo sawa. Kuhusu Dk. Magufuli kama kuna kura 100 zote ningempa yeye ni mtu makini, si mwoga ameondoa mafisadi, maendeleo yapo wazi kila kitu amekifanya kwa uwazi na kwa kujiamini.”

Naye, Sauda Mussa Chama alisema Dk. Shein ameifanya Zanzibar imen’gara hata kipofu akipapasa akiambiwa aonyeshe aliyoyafanya Dk. Shein ataonyesha hata kwa macho na kupapasa.

“Tumeona amefanya mambo makubwa kuimarisha barabra, kujenga hospitali na shule, zamani wanafunzi walikuwa wanakaa darasa moja hata 200, kwa sasa wanafunzi wanasoma kwa raha.

“Wazee Zanzibar kwa sasa wanaishi vizuri zamani Sh 100 ya dagaa wanaitafuta, kwa sasa wazee wamepewa kipaumbele wanapewa fedha zao za kila mwenzi. Michenzani yetu mtu akija Zanzibar anaweza kudhani yupo Ulaya hayo ni matunda mazuri ya Dk. Shein.

“Kwa Dk. Mwinyi mtazamo wangu ni mtu atakayetufaa, ameelezea atawajali kinamama wajane na vijana, kwa mtazamo wangu atatufaa sana ni rais atakayeifanya Zanzibar ingare zaidi ya hapa. Atavaa viatu vya Dk. Shein atafanya na kumalizia yale mazuri anayofanywa na Dk. Magufuli.”

Aidha, kuhusu uwezo wa Dk. Magufuli alisema ni rais ambaye hakinaishi wala hachushi: “Tutampa kura nyingi za ndio na tuna hakika atafanya mazuri zaidi, Tanzania inavutia kwa sasa hata majirani wanaitamani Tanzania, ukienda Dar es Salaam kama uko China, ukipiga picha baadhi ya maeneo ukimwambia mtu uko China atakuamini.”

Mwanaidi Aboubakar Abdulrazak, alisema kwa Dk. Mwinyi wanategemea kupata kiongozi mahiri watahakikisha ushindi wa CCM ili kumpata kiongozi atakayewavusha. Na hata kwa uande wa Dk. Magufuli hawatakubali kumkosa kwa kuwa wanaamini ushindi upo kwa asilimia zaidi ya 75, atashinda kwa kishindo huu ni mwaka wa CCM kwa kuwa wamefanya mambo makubwa yanayoonekana pande zote mbili za muungano.

“Kwa kweli Dk. Shein amefanya mambo mengi amejenga shule nyingi, tulikuwa na shule kama mabanda ya ng’ombe lakini sasa shule zinatazamika amejitahidi kwa kweli tunaamini Dk. Mwinyi atafanya mengi zaidi, tuna imani Dk. Mwinyi atafuata nyendo za Dk. Magufuli na hata vijana wanampenda wanamuita ‘brother kaka’ hii ni ishara ya ushindi,” alisema na kusisitiza kwa upande wa Tanzania Bara kuwa:

“Dk. Magufuli ni jembe yule anapotoa amri anasikizwa, zamani ilikuwa ukienda kupata huduma unadharauliwa lakini kwa sasa watumishi wanatuheshimu. Wapinzani wanajua Dk. Magufuli anaweza lakini wameingia kwenye kinyang’anyiri kwa sababu demokrasia ya vyama vingi inawataka kufanya hivyo.”

Aidha, kipindi hiki kinaelezwa kuwa na kampeni za kistaarabu hasa baada ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao wamegaiwa mafungu mawili wengine wamekwenda ACT Wazalendo kwa amri ya Maalim Seif Shariff Hamad ambaye kwa mara ya tano mfululizo anagombea urais wa visiwa hivyo na wengine wamebaki chama hicho.

Hii ni fursa kwa vyama vingine ikiwemo CCM kupata wafuasi wapya ambao watabaki katikati, kwa kuwa wananchi wanavutiwa na mtaji wa maendeleo aliyofanya mgombea yeyote katika nafasi ya urais, ubunge au uwakilishi.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here