Yanga yatuma salaam kwa wapinzani wao

0

NA KELVI SHOO, TUDARCO

UONGOZI wa Yanga umesema kuwa ushindi wao dhidi ya Ruvu Shooting ni mwendelezo wa yale waliyojiwekea kwenye mpango kazi wao hivyo wataendelea kushusha dozi taratibu ndani ya uwanja.

Yanga ikiwa imecheza jumla ya mechi 14 haijapoteza kwa msimu wa 2020/21 hata mchezo zaidi ya kuambulia sare nne na kushinda mechi 10.

Ipo nafasi ya kwanza ikiwa na jumla ya pointi 34 kibindoni inafuatiwa na Azam FC nafasi ya pili yenye pointi 27 nayo pia imecheza mechi 14.

Kibarua chake kinachofuata ni dhidi ya Mwadui FC mchezo utakaochezwa Uwanja wa Kambarage, Desemba 12.

Ofisa Uhamasishaji wa Yanga Antonio Nugaz, aliyasema hayo mara baada ya kumalizika mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting, juzi Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa matokeo ya mchezo huo yalikuwa ni salamu kwa wapinzani wao ambao wanapaswa kujiandae kisaikolojia kwa kuwa wamejipanga kuendelea kutoa dozi.

“Huu ni mwendelezo wa yale ambayo tumeyapanga kuyafanya ndani ya ligi na katika mashindano mengine ambayo tutashiriki kwani tupo vizuri.

“Tunawaambia kwamba kazi ndo kwanza inaanza hivyo wale wengine nawaambia kwamba, wape salamu tupo imara na tunapambana mwanzo mwisho.

“Kila mchezo kwetu tunahitaji pointi tatu muhimu hakuna jambo jingine zaidi ya hilo na furaha yetu ni kuona kwamba kila mmoja anatimiza majukumu yake ndani ya uwanja, mashabiki waendelee kutupa sapoti,” alisema Nugaz.

Aidha, Nugaz, alijigamba kwa kuwataka mashabiki wa timu hiyo kuanza kugeukiana na kupigana vifua ikiwa ni ishara ya kupongezana kuelekea ubingwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here