Yanga ni moto lakini isibweteke

0

NA MWANDISHI WETU

YANGA imemaliza duru la kwanza la Ligi Kuu Bara kibabe kwa kucheza mechi zao zote 17 bila kupoteza hata moja, lakini pia ikizidi kuwasha taa ya kijani kwa wapinzani wao kwamba msimu huu wana jambo lao, hasa kwa moto walionao kwa sasa, huku nyota wao wakitisha zaidi.

Wababe hao waliandikisha ushindi wao wa 13 msimu huu kwa kuinyoa Ihefu SC nyumbani kwao jijini Mbeya na kufanya wafikishe jumla ya pointi 43 katika mechi zao 17, zikiwamo sare nne ilizopata mpaka sasa.

Ushindi wao wa pili mfululizo wa mabao 3-0 kwa kuinyoa Ihefu, ulichangiwa kwa kiwango kikubwa na umahiri wa nyota wake mpya, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ ndiye habari itakayowatisha zaidi wapinzani wao huku mashabiki wao wakiwa na shangwe lisilotamatika.

Awali iliinyoa Dodoma Jiji kwa mabao 3-0, siku chache tu ikiitoka kuifumua Mwadui 5-0 na kuwafanya wale waliokuwa wakiibeza kwamba msimu huu wamekuwa wazee moja moja, kufunga midomo kutokana na dozi nono inayotoa kwa sasa.

Katika mechi hizi mbili mfululizo, ukitaka kuisifia Yanga hutaacha kumtaja Saido ambaye katika mechi zake mbili tangu aanze kuitumikia timu hiyo amefanikiwa kufunga bao moja lakini akiasisti mara tatu na mara mbili kati ya asisti hizo amezipiga juzi kibabe kisha akatoka.

Mchezaji huyo tangu atue kikosini ameongeza kitu na kuirahisishia kazi safu ya ushambuliaji, huku washambuliaji, Deus Kaseke na Yacouba Songne wakizidi kunoga na kuwafanya mashabiki wa Yanga sasa kutembea kifua mbele.

Namna Yanga iliyoimarika eneo hilo na muunganiko wa idara nyingine ikiwamo beki na kiungo, imeifanya timu yao iwe tishio na kuonyesha wazi msimu wana jambo lao na wapinzani wao katika Ligi Kuu wajipange kwelikweli kama wanataka kula nao sahani moja kwenye ubingwa.

Ihefu licha ya kipigo hicho kutoka kwa Yanga, lakini bado imeonekana kuwa na mabadiliko makubwa kiuchezaji chini ya Kocha Zubery Katwila na hasa ingizo la nyota wapya waliosajili kwenye dirisha dogo akiwa kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ na wale waliotua kwa mkopo.

Pamoja na kuonekana kufanya vizuri Yanga haitakiwi kubweteka kwani wapinzani wao wanawafuatia nyuma kwa kupishana alama chache sana hivyo meza inaweza kupinduka muda wowote kwa Yanga kuharibu mchezo mmoja tu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here