Yanga kuimarisha safu ya ushambuliaji Dirisha Dogo

0

NA MWANDISHI WETU

KOCHA Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, amefunguka kuwa anahitaji kuona kikosi chake kinafunga mabao mengi kwenye michezo yao ya mzunguko wa pili, ili kuwe na uwiano mzuri wa mabao, ndiyo maana wameazimia kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji kwa kumshusha straika. 

Yanga inatajwa kuwa kwenye hatua za mwisho kumalizana na straika Mkongomani, Fereboy Dore, ili kubusti safu yao ya ushambuliaji, inayoonekana kukosa makali ambapo washambuliaji wote wanne wamefunga mabao tisa tu kwenye michezo 18.

Kaze alisema: “Baada ya kuwa na mafanikio makubwa katika eneo la ulinzi kwenye mzunguko wa kwanza, kwa sasa tunataka kuhakikisha tunaongeza makali zaidi katika eneo la ushambuliaji na ndiyo maana tupo kwenye mpango wa kusajili straika mwingine ambaye atakuja kuwaongezea nguvu wale waliopo.

“Tunataka kuona timu yetu inapata mabao mengi, ili kuwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa kama tunataka kumaliza katika nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo.”

Yanga inaongoza msimamo na pointi zao 44 ilizokusanya baada ya kucheza michezo 18, imeshinda mechi 13 na kutoa sare kwenye michezo mitano.

Kikosi cha Yanga kwa sasa kipo Zanzibar kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambapo leo kitakuwa na kibarua cha kusaka ushindi mbele ya Jamhuri, Uwanja wa Amaan.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here