Yanga ikimsajili Chama atawasaidia-Kashasha

0

NA MWANDISHI WETU

MTANGAZAJI na mchambuzi maarufu wa masuala ya michezo nchini, Alex Kashasha ‘Mwalimu Kashasha’, amekiri kuwa kama Yanga itafanikiwa kumsajili kiungo nyota wa Klabu ya Simba, Clatous Chama,basi atawasaidia Yanga kutokana na ubora alionao.

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa zinazomhusisha kiungo huyo wa Simba kuwa kwenye mazungumzo na uongozi wa Yanga ili kujiunga na timu hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maluum ya +255 Global radio yaliyoruka mubashara kupitia Global TV Online, Kashasha amesema: “Kama ni kweli Yanga watafanikisha usajili wa Chama kama ambavyo tetesi zimekuwa zikieleza, basi utakuwa usajili bora, na naamini atakuwa msaada mkubwa kwao.

“Miongoni mwa wachezaji bora na wenye nidhamu ni Chama, uwezo wake ndani ya uwanja umekuwa ukionekana hivyo nguvu zake zikiongezwa ndani ya Yanga basi timu hiyo itafanya vizuri kwenye mashindano itakayoshiriki,”alisema Kashashs.

Wakati huo huo, uongozi wa Simba ulisema kuwa kwa sasa nyota wao Clatous Chama ataendelea kuwa ndani ya kikosi hicho kwa kuwa ni mali yao.

Chama mwenye mabao mawili ndani ya Ligi Kuu Bara na pasi tano kwa msimu wa 2020/21 kati ya mabao 22 yaliyofungwa na Simba anatajwa kuingia kwenye rada za watani wa jadi Yanga.

Kwenye wakati wa usajili wa dirisha kubwa msimu uliopita, Fredrick Mwakalebela ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga alisema kuwa wamefanya mazungumzo na kiungo huyo.

Baadaye alikanusha taarifa hizo baada ya uongozi wa Simba kumjibu na kupeleka malalamiko Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) kwa kuwa Yanga ilikiuka vigezo vya usajili wa mchezaji kwa mujibu wa Fifa kwa kuzungumza na mchezaji ambaye bado ana mkataba.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Haji Manara, Chama ni mali ya timu hiyo na hakuna mpango wa yeye kuibukia timu nyingine kwa sasa.

“Hizo ni habari tu ambazo zinaeleza kwamba Chama anaondoka anakwenda sijui wapi, lakini ukweli ni kwamba mwamba bado yupo ndani ya Simba na suala la kuondoka bado sana.

“Kwa sasa akili zetu tumeziwekeza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kisha mambo hayo mengine yatafuata,”alisema Manara.

Simba inawakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa ambapo ina kazi ya kusaka ushindi mbele ya Plateu United ya Nigeria.

Mchezo wa kwanza kwa Simba unatarajiwa kuwa nchini Nigeria Uwanja wa Jos kati ya Novemba 27-29 na ule wa marudio unatarajiwa kuchezwa kati ya Desemba 4-6 mwaka huu, Uwanja wa Mkapa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here