Yametimia: Mkataba ujenzi wa SGR Mwanza- Isaka wasainiwa

0

NA JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

Tanzania na China zimetiliana saini ya mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) katoka Mwanza hadi Isaka yenye urefu wa kilometa 341 ambayo itajengwa na kampuni kutoka China.

Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo ilifanyika jana wilayani Chato mkoani Geita na kuhudhuriwa na Rais wa Tanzania Dk John Magufuli na Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi. 

Akizungumzia kuhusu mradi huo Rais Magufuli aliwataka wakandarasi wa China kuujenga kwa haraka na kuiomba Serikali ya China kutoa mkopo nafuu kwaajili ya kipande cha Isaka-Makutupora.

Ujenzi SGR kipande cha Mwanza hadi Isaka utatekelezwa kwa miezi 36 kwa gharama ya shilingi trilioni 3.0617. Kwa  kusainiwa kwa mkataba huu, Serikali itakua inatekeleza mradi wa SGR katika eneo lenye urefu wa KM 1,063.

Kwa upande wake Waziri Yi alisema uwepo wa Rais Magufuli katika tukio hili la utiaji saini wa mkataba huo unaonesha umuhimu mkubwa ambao Rais anaupa ushirikiano na urafiki uliopo kati ya nchi hizi mbili.

“Nachukua fursa hii kuyaagiza makampuni ya China yanayotekeleza miradi hapa nchini Tanzania kutekeleza miradi hiyo kwa kuzingatia kwanza maslahi ya Tanzania,” alisema Yi.

Awali akielezea kuhusu mradi huo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho, alisema Serikali  inatekeleza kipande cha tatu cha ujenzi wa reli  ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza .

Chamuriho alisema  mkataba huu utatekeleza kwa muda wa miezi 36 kwa gharama ya Sh trilioni 3.06 ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/25 na mpango wa maendeleo ya Taifa wa miaka mitano.

“Ni jambo la faraja kwamba utiaji saini huu unafanyika ikiwa kuna ugeni wa Waziri wa Mambo ya Nje ya China.

“Huu ni ushahidi mwingine wa mahusiano ya kiuchumi kati yetu na China tunawakaribisha kampuni zao kushiriki katika ujenzi wa vipabde viwili vilivyobaki vya reli ya kisasa vya Makutopora hadi Tabora na Tabora hadi Isaka,” alisema Chamuriho.

Pia aliiomba Serikali ya China kuunga mkono katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuridhia taasisi za Serikali ya China kutoa mkopo nafuu ili reli nzima kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza iweze kufanya kazi mapema.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania, (TRC), Masanja Kadogosa, alisema makampuni ya kimataifa yaliyojitokeza kwa ajili ya kujenga reli ya kisasa kipande cha Mwanza – Isaka ni 108, baada ya kufanya mchakato kampuni za CCECC zilishinda zabuni.

 “Tulitangaza kipande hiki cha tano mwezi Agosti 25 na  Novemba 25 na kampuni za kimataifa zaidi ya 108 ziliomba tenda. Bada ya kufanya mchakato kwa mujibu wa sheria za nchi yetu kuna kampuni mbili zilishinda,” alisema Kadogosa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CCECC, Mhandisi Jiang Yigao alisema; “Kampuni hii imekua Tanzania kwa zaidi ya miaka 50, kwa miaka 10 iliyopita tumetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo daraja la Busisi- Kigongo, Ubungo interchange na ujenzi wa reli ya Tazara.

“Kama tulivyofanya ujenzi wa TAZARA tutafanya hivyo hivyo kwa kujenga reli hii ya kisasa tukitumia raslimali zilizopo na kujenga mradi huu kwa wakati na kwa viwango vya kimataifa.”

WALIYOZUNGUMZA RAIS MAGUFULI NA WANG YI

Kabla ya utiliaji saini wa Mkatba wa ujenzi wa Reli Rais Magufuli alifanya mazungumzo na Waziri Wang Yi kuhusu mambo mablimbali ya kimahusiano na uchumi baina ya TANZNAIA NA China.

Katika hotuba yake Rais magufuli alidokeza mambo makubwa matatu waliyozungumza ikiwemo kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa miradi.

“Nimemuomba atusaidie miradi mitatu mikubwa ya umeme ukiwemo wa maji ya mkoani Njombe, Lumakali na Luhuji pamoja na ujenzi wa KM 148 za barabara kwa kiwango cha lami Zanzibar,” alisema Rais Magufuli.

Pia alisema ameiomba Serikali ya China kutoa msamaha wa madeni mbalimbali yakiwemo ya muda mrefu ambayo China iliikopesha Tanzania.

“ Nimewaomba watusamehe madeni yetu tuliyokuwa tumekopa ikiwemo la Dola za Marekani Mil. 15.7 za ujenzi wa reli ya TAZARA, deni la Dola za Marekani Mil.137 la nyumba za askari pamoja na deni la kiwanda cha Urafiki la Dola za Marekani Mil.15,” alisema Rais Magufuli.

Alibainisha kuwa China imejipatia fedha nyingi kupitia utekelezaji wa miradi hapa nchi ambapo kwa miaka 10 wamevuna zaidi ya Trilioni 21 sawa na Dola za Marekani Bilioni 10 ambazo ni fedha za walipa kodi wetu; “Ndiyo maana kwenye maombi yangu niliomba mtusamehe maana na nyie mmevuna mengi kwetu.”

Alisema walizungumzia pia suala la fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania na fursa ya soko la China kwa bidhaa za kitanzania.

“China ni nchi tajiri duniani na sisi Tanzania tuna mazao mengi ambayo tunaweza kuyapeleka nchini humo hivyo natoa wito kwa Watanzania kuwa huu ndio wakati wa kulishika soko la China kwa kuwapelekea mazao yetu.

“Nimemuhakikishia Waziri Wang Yi kuwa kufanya biashara na Tanzania kuna faida kwani kupitia nchi yetu watakuwa na uwezo kufanya biashara na nchi zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye watu milioni 165 na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi zilizo Kusini mwa Afrika yenye watu milioni 500 kwa sababu  Tanzania  ni mwanachama wa Jumuiya hizo.

“Mazungumzo  tuliyofanya yalikuwa mazuri na nimemuhakikishia Waziri Wang Yi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na China kwa sababu  ni ndugu zetu,” alisema Rais Magufuli.

Pamoja na ushirikiano uliopo kwenye sekta nyingine ikiwemo sekta ya miundombinu, uhusiano baina ya Tanzania na China umezidi kuimarika zaidi katika sekta ya TEHAMA.  Kupitia kampuni ya Huawei, China imekuwa  ikishirikiana na Tanzania katika kufanikisha miradi mbalimbali inayolenga kuboresha sekta ya TEHAMA sambamba  na kukuza na kuibua vipaji vya sekta hiyo muhimu hapa nchini.

Matunda ya ushirikiano huo yalijidhihirisha hivi karibuni ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikabidhi  tuzo kwa washindi wa shindano la TEHAMA duniani lililoandaliwa na kampuni ya Huawei ambapo wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walishika nafasi ya pili Ulimwenguni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here