Waziri Ummy atoa miezi mitatu vifungashio visivyo na ubora

0

Na Dotto Kwilasa, Dodoma 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu ametoa muda  wa miezi mitatu kuondolewa sokoni kwa vifungashio visivyokidhi vigezo vya Shirika la Viwango nchini (TBS) .

Mwalimu ametoa agizo hilo leo Januari 8 alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma ambapo amesema kumeibuka wimbi la mifuko ya plastiki kwa kisingizio cha vifungashio wakati vingi havikidhi vigezo kwa mujibu wa sheria za nchi.

amesema licha ya serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki lakini siku za hivi karibuni kumejitokeza changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki aina ya ‘tubings’ visivyokuwa na sifa na hivyo kutokidhi matakwa yaliyowekwa na TBS .

Amesema vifungashio hivi kwa sasa vinazalishwa kwa wingi na kwa ukubwa mbalimbali na vimekuwa vikitumika kama mifuko ya kubebea bidhaa sokoni na kuleta dhana kuwa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku imerudi kivingine.

“Mifuko hiyo imeanza kuzagaa kwenye mazingira ya mitaa  yetu na vijijini vyetu kwa kasi kubwa na hivyo kurudisha nyuma mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi chote cha kupambana na changamoto ya mifuko hiyo.” amesema Mwalimu na kuongeza kuwa;

“Vifungashio vinapaswa viwe na unene usiopungua microns 30 upande mmoja au microns 60 pande mbili,kilichofungashiwa bidhaa ili kukuza kabla ya kwenda sokoni,viwe na alama ya mzalishaji au anayepakia bidhaalakini pia viwe na alama ya ubora inayotolewa na TBS. “

Mwalimu amewataka wasambazaji, wazalishaji na waagizaji wa vifungashio hivyo kuacha mara moja kufanya hivyo vinginevyo wajiandae kukutana na mkono wa sheria.

Hata hiyo amesema ametoa muda huo wa kuondoka sokoni vifungashio hivyo kutokana na wafanyabiashara wadogo kuonekana bado wana shehena ya mzigo huo .

“Kwa kuzingatia maombi ya wafanyabiashara wadogo ambao bado wana shehena ya vifungashio hivi na kwa kuwa Serikali ya awamu ya tano inathamini mchango wa wafanyabiashara wadogo katika juhudi za kujiongezea kipato katika kupambana na umasikini natoa kipindi cha miezi mitatu kuanzia siku ya tangazo hili kuhakikisha kwamba vifungashio visivyokidhi viwango vya TBS havipo sokoni.” amesisitiza

Kwa mujibu wa Waziri huyo baada ya kipindi hicho Serikali haitatoa tangazo jingine lolote kuhusiana na katazo la matumizi ya vifungashio hivyo na badala yake itaendesha operesheni maalum kuwabaini wanaozalisha na kuvisbaza na kuwachukulia hatua Kali kwa mujibu wa sheria .

Aidha ametumia fursa hiyo kuwatoa hofu wananchi kwamba hakutakuwa na uhaba wa vingashio vinavyokidhi viwango baada ya kipindi hicho cha miezi mitatu kwa kuwa kwa mujibu wa TBS wapo wazalishaji wa kutosha kukidhi mahitaji yaliyopo nchini.

Amewaasa wazalishaji na wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa hiyo kwa kuzalisha vifungashio vyenye ubora unaotakiwa.

Ikumbukwe kuwa mnamo Juni Mosi , 2019 Serikali ilipiga marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini ambapo tangazo hilo lilihusu kuzuia uzalishaji, uingizaji nchini, uuzaji, uhifadhi, usambazaji, matumizi ya mifuko ya plastiki na umiliki wa mifuko hiyo kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote.

Lengo Kuu la marufuku hiyo pamoja na mambo mengine ni kulinda mazingira ,afya ya binadamu na mifugo dhidi ya athari za matumizi ya mifuko hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here