Waziri Mkuu awasimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha, Meneja wa Matumizi wa TPA

0
Mkurugenzi wa Fedha wa TPA,Nuru Mhando

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha, Nuru Mhando pamoja na Meneja wa Matumizi ya Fedha wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),Witness Mahela ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha zinazowakabili.

Majaliwa amechukua hatua hiyo baada kupokea ripoti ya Ukaguzi Maalum uliofanywa na CAG katika hesabu ya Bandari ya Kigoma kwa mwaka 2017/2018 na 2018/2019. Lengo la ukaguzi huo lilikuwa kujiridhisha kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (umapili, Disemba 27, 2020 katika kikao chake na Waziri na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania na Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kilichofanyika katika ofisi za TPA jijini Dar es Salaam. Amesema taasisi hiyo imebeba taswira ya uchumi wa Taifa, lazima kazi ifanyike vizuri.

Majaliwa ameitaka Bodi ya Bandari Tanzania ihakikishe kwamba mamlaka hiyo inafanyakazi kwa weledi na isisite kuchukua hatua kwa mtumishi atakayebainika kutenda makosa na isimbebe kwa namna yoyote.

“Miongoni mwa mambo yasiyoridhisha yanayofanywa na mamlaka hiyo ambayo yanaikosesha Serikali mapato ni pamoja na msamaha wa kodi ya zaidi ya sh. bilioni mbili iliyoutoa kwa kiwanda cha saruji cha Mbeya licha ya kukataliwa na kamati ya misamaha.

“Licha ya kuongezeka kwa makusanyo lakini kati ya fedha inayokusanywa asilimia 70 tu ndiyo inayoongia Serikalini na kiasi kilichobaki kinaishia mifukoni jambo ambalo halikubaliki,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here