Waziri Mkuu ashuhudia MV Kilindoni ikiingia majini kwa mara ya kwanza

0

Na Bethsheba Wambura Dar es Salaam

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Jumanne Disemba 15, 2020 ameshuhudia  kwa mara ya kwanza meli ya MV Kilindoni Hapa Kazi ikiingia majini. Meli hiyo itakayokuwa inafanya safari zake kati ya Mafia na Nyamisati mkoani Pwani imegharimu Sh Bil. 5.2 na itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 500, abiria 200 na magari 10

Akizindua safari za meli hiyo Jijini Dar es Salaam Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuanza kwa Safari ya meli ya MV Kilindoni ni muendelezo wa Serikali kuboresha sekta ya usafiri na usafirishaji nchini.

Majaliwa amesema katika sekta ya usafiri na usafirishaji kuanzia barabara, reli, anga na majini Serikali imefanya kazi na bado inaendelea kuboresha maeneo hayo.

“Serikali imejizatiti kuhakikisha kwamba tunajizatiti katika sekta ya usafirishaji inayohusisha barabara, anga, reli na maji. Katika barabara tumejenga za kuunganisha mikoa na hata nchi jirani tayari zipo na sasa tunaenda kujenga za kuunganisha Wilaya na Wilaya.

“Kwa upande wa anga, tumeshanunua Ndege nane na bado nyingine zitakuja Ili kuona kwamba kila mkoa uliopo nchini ndege zinatua na viwanja vya ndege vinajengwa huko mikoani Ili ndege hizo zitue.

“Upande wa reli kuna ufufuaji wa reli ya Kati na kaskazini, Ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme (SGR), na hadi Aprili, 2021 tunatarajia treni hiyo itaanza safari kutoka Moro kuja hadi Dar es Salaam.


“Kwa upande wa usafirishaji wa majini kuna ujenzi wa meli na vivuko. Na meli zetu tunazijenga kisasa sana ili watu wanaposagiri wafurahie safari zao, tunatambua pia kwamba tuna visiwa, Serikali inajenga meli  na vivuko ambapo katika visiwa vinavyozunguka Ziwa victoria tumejenga vivuko kama MV Ukara kwa gharama ya Sh bil 4.4, mizigo tani 100, abiria 300 na magari 10, MV Chato kwa Bil. 3.4 mizigo tani 100, abiria na magari 10 na MV Ilemela kwa Bil. 3.7 mizigo tani 100, abiria 300 na magari 10,” amesema na kuongeza kuwa;

“Kwasasa inajengwa meli itakayofanya safari zake kutoka Bandari ya Mtwara hadi Tanga na Zanzibar na kwenda Hadi visiwa vya Comoro.”

Aidha Majaliwa amesema yote hayo yanatendeka kutokana utendaji thabiti QA Rais Dk. John Magufuli.

“Utekelezaji wa haya unatokana na Mhe Rais Magufuli utashi wake kwamba ahadi zilizotolewa kwa Wananchi zinatekelezwa, chama hiki (CCM) kina benki ya watendaji kuhakikisha yote yaliyoahidiwa yanatekelezwa,”  amesema

Akiizungumzia kampuni ya Songoro Marine ambao ndiyo wametengeneza meli hiyo amesema; “Meli hii imetengenezwa na kampuni ya Songoro marine ambayo ni kampuni ya wazawa wajenzi. Sasa hivi tukitaka meli za ukubwa huo na kubwa zaidi hatuna haja ya kuagiza kutoka nje tuna tengeneza hapa hapa. Tunaposema tunafungua fursa za ajira tunamaanisha, katika kampuni hiiwameajiriwa watu 15, 00 ambao pengine wangekuwepo tu mtaani.”


Naye Mbunge wa Mafia, Juma Kipanga  amemshukuru Majaliwa kwa kwenda kuwazindulia meli hiyo

“Natoa Shukrani zangu kwako Waziri Mkuu kwa maana umekuwa ukifatilia mwenendo wa meli hii  kwa zaidi ya mara nne, hatimaye leo inaanza safari sisi Wakazi wa Mafia tunashukuru sana

“Pia nikishukuru Chama changu vha CCM kwani kivuko hiki kilikuwa katika ilani iliyopita ya (2015-2020) lakini pia katika ilani hii ya mwaka huu (2020-2025) pia kuna kivuko kingine cha pili ambacho kitajengwa.

“Lakini tunamshuru pia Rais Magufuli Kwa kutuheshimisha na kupatia kivuko hiki tunaahidi kukitunza na kuyaenzi Mapato yatakayotokana na kivuko hiki Ili yakafanye kazi nyingine,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine, Saleh Songoro amesema wao wanatengeneza meli na vivuko hapa nchini na nchi jirani na vivuko vya ni vya kisasa kabisa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here