Waziri China atoa siri uchumi wa viwanda

0
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi akiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako wakifunua pazia kuashiria kufungua rasmi Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Chato mkoani Kagera mara tu baada ta kuwasili nchini kwa ziara ya siku mbili jan Jumatano Januari 7, 2021

NA JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi amesema ili Tanzania ifikie uchumi wa viwanda ni lazima kuwa na vijana wengi wenye ujuzi wa ufundi stadi.

Waziri Yi aliyasema hayo jana katika hotuba yake mara baada ya kuzindua Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wialayani Chato ambako alianzia ziara yake nchini.

Yi yupo hapa nchi kwa ziara ya siku mbili ambayo inaishia leo ikiwa ni matunda  ya mazunguzmo ya Rais John Magufuli na Rais wa China Xi Jingpin hivi karibuni kuhusiana na kushirikiana kuboresha mahusiano na maslahi ya kiuchumi kwa mataifa yote mawili.

Waziri Yi alisema kutokana na umuhimu wa kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi wa ufundi stadi China imeamua kushirikiana na Serikali katika kuboresha vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ikiwemo kujenga chuo kimoja mkoani Kagera chenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,000.

Waziri Yi alimpongeza Rais Magufuli kwa maono na uzalendo wake kwa kujenga vyuo vingi vya ufundi kikiwemo Chuo cha Ufundi Chato kwaajili ya wananchi wa wilaya hiyo.

Alisema China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha chuo cha VETA Chato na kwamba kama kuna mahitaji yeyote basi yafikishwe kwa balozi wa China hapa nchini.

Waziri Yi alitoa msaada wa Sh milioni 350 kwa chuo hicho kwaajili ya kuboresha miundombinu ya kujifunzia kwa programu ya uvuvi.

Akitoa shukrani kwa Serikali ya China kwa msaada huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alisema utatumika kununulia vifaa vya mafunzo ya uvuvi kwani wananchi wengi wa eneo hilo wanajishughulisha na uvuvi.

 Awali katika hotuba yake Profesa Ndalichako alisema Serikali imelenga kuwa na kituo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi katika kila wilaya na kuomba China ishirikiane na Serikali katika kufikia lengo hilo.

“Najua ni malengo makubwa lakini tutayafanikisha kwa kutumia mapato yetu ya ndani pamoja na misaada ya wadau kama Serikali ya China,” alisema Ndalichako.

Pia alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya China kwa msaada ya kujenga kituo kimoja cha Kagera ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000.

Alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika uendelezaji wa vyuo vya ufundi kwani ndiyo njia ya uhakika ya kujenga maendeleo ya kujitegemea.

Leo katika kuhitimisha ziara yake Waziri Yi atakuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli na atatembelea mwalo wa Chato ili kuona shughuli za uvuvi, ikizingatiwa kuwa ziwa Victoria ni ziwa la pili kwa ukubwa duniani.

 Pia Kabudi alisema yeye na wajumbe wake kutika Tanzania atakuwa na mazungumzo rasmi na Waziri Yi pamoja na ujumbe wake .

Kati ya masuala ambayo Waziri Yi atazungumza na ujumbe wa Tanzania ni pamoja na kupanua wigo wa biashara za Tanzania nchini China, kushiriki maonesho ya biashara ili kukuza bidhaa zetu pamoja uwekezaji katika sekta ya madini.

 Pia kuhusu utoaji wa mikopo pamoja na uzalishaji wa umeme wa maji katika baadhi ya maeneo nchini kwani nchi ya China imepiga hatua kubwa katika suala la teknololojia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here