Wawekezaji karibuni Zanzibar-Dk. Mwinyi

0
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Mmiliki wa Hoteli ya Park Hyatt kutoka Nchini Dubai, Ali Saeed Juma Albwardy na (kulia kwake), Yakoub Osman Sadiq, alipowasili katika ukumbi wa Ikulu kwa ajili ya mazungumzo na ujumbe huo (Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  imewahakikishia wawekezaji wanaotaka kuja kuekeza Zanzibar kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itawawekea mazingira mazuri.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Mmiliki wa Hoteli ya Park Hyatt Ali Saeed Juma Albwardy kutoka nchini Dubai akiwa amefuatana na Nicolas Cedro, Meneja Mkuu wa Hoteli ya Park Hyatt, Nicolas Kong, Meneja Mkuu wa Melia, Zanzibar pamoja na Yakoub Osman Sidik.

Katika maelezo yake Dk. Mwinyi alimueleza muwekezaji huyo kwamba Serikali anayoiongoza itahakikisha inafanya kazi vizuri na wawekezaji sambamba na kuwawekea mazingira bora ya uekezaji.

Alieleza kuwa kwa upande wa sekta ya utalii ambayo ndio inayochangia zaidi katika pato la Taifa, Serikali ya Awamu ya Nane itahakikisha sekta hiyo inawekewa mazingira bora pamoja na wawekezaji wake.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba Serikali yake imekusudia kufanya kazi na sekta binafsi kwani inatambua umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi na kuinua pato la Taifa.

Aliongeza kuwa Serikali anayoiongoza itahakikisha inashirikiana vyema na sekta binafsi katika kuinua uchumi wa Zanzibar.

Alisisitiza kwamba sekta binafsi ndio injini ya uchumi, hivyo Serikali ya Awamu ya Nane taweka mikakati maalum ya kuhakikisha sekta hiyo inaimarika ili kuleta tija kwa nchi na wananachi wake kwani kuimarika kwake kutaongeza soko la ajira sambamba na pato la Taifa.

Aidha,Dk. Mwinyi alieleza umuhimu wa kuimarisha bandari na viwanja vya ndege ili sekta ya utalii, biashara na uwekezaji zizidi kuimarika na kusisitiza kwamba hio ndio azma ya Serikali ya Awamu ya Nane.

Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi i alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji, wafanyabishara na wenye viwanda wa ndani na nje ya Zanzibar waje kuwekeza kutokana na kuwepo fursa nyingi hapa nchini.

Alisisitiza kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa na Serikali yake katika kuhakikisha inaweka miundombinu rafiki ili wawekezaji, wafanyabiashara na wenye viwanda waje Zanzibar kufanya shughuli zao hizo.

Pamoja na hayo, Dk. Mwinyi alikiri kwamba Zanzibar ina vivutio vingi vya kitalii sambamba na ukarimu wa watu wake na utamaduni walionao ambavyo vyote hivyo ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya kitalii na kuahidi kwamba vyote hivyo vitaimarishwa katika kufikia lengo lililokusudiwa.

Mapema Mmiliki wa Hoteli ya Park Hyatt Ali Saeed Juma Albwardy alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kuchaguliwa na Wananchi wengi wa Zanzibar na kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi hatua ambayo inatokana na imani ya wananchi hao kwake.

Albwardy alimueleza Dk. Mwinyi azama ya Kampuni Park Hyatt ya kuongeza uwekezaji hapa Zanzibar kutokana na kuwepo kwa vivutio kadhaa sambamba na ukarimu na utamaduni wa watu wake.

Aliongeza kuwa Kampuni yake yenye Makao Makuu yake nchini Dubai lakini ina hoteli kadhaa katika nchi mbali mbali duniani inavutiwa zaidi na Zanzibar kutokana na mazingira yake mazuri ya kitalii ukiwemo Mji Mkongwe.

Mmiliki huyo wa Hoteli ya Park Hyatt amesifu mashirikiano mazuri aliyoyapata na anayoendelea kuyapa kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuahidi kwamba
atahakikisha anaendelea kuitangaza zaidi Zanzibar Kimataifa.

Aidha, Albwardy alimueleza Dk. Mwiny azma yake ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Nane ya kuimarisha sekta za biashara na viwanda, vikiwemo viwanda vya nguo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here