Watumishi 23 wa MOI wachunguzwa wizi dawa, vifaa tiba vya Bil 1.2

0

Na Mwandishi Wetu 

Watumishi 23 wa Idara ya Famasia katika Taasisi ya Mifupa (Moi) wanachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa madai ya wizi wa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh1.2 bilioni.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Januari 13, 2021 na mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Mbungo amesema watumishi hao wanadaiwa kufanya udanganyifu huo kati ya mwaka 2018 hadi 2020.

Akielezea namna ubadhirifu huo ulivyofanyika, Mbungo amesema, watuhumiwa hao walikuwa wanaandika taarifa za uongo katika mfumo unaofahamika kama MEDPRO4 kwa kuweka idadi kubwa ya vifaa vilivyotolewa tofauti na idadi halisi iliyotolewa na madaktari kwa wagonjwa na wateja.

“TAKUKURU kwa kushirikiana na MOI imedhibiti uchepushaji na ubadhirifu wa madawa ya zaidi ya Sh Bil. 1.2, ambazo zilihujumiwa kwa manufaa binafsi na watumishi wa kitengo cha famasia katika taasisi hiyo.

“Ubadhirifu huu umebainika kutokana na uwepo wa tofauti kati ya taarifa za dawa zilizoingizwa na wafamasia na zile zilizoandikwa na madaktari ikilinganishwa na fomu za wagonjwa zilizotoa maelekezo ya aina ya dawa.

“Mfano Daktari anaandika dawa 30 kwa ajili ya matumizi ya mgonjwa, Mfamasia anaongeza idadi ya dawa na kuingiza kwenye mfumo dawa 60 au 70, jambo ambalo kiuhalisia mgonjwa anakuwa hajapatiwa idadi hiyo ya dawa,” amesema Brig. Mbungo na kuongeza kuwa;

“Pia tumebaini wafamasia walikuwa wanasababisha upotevu wa dawa kwa kuingiza taarifa za uongo, njia nyingine ni ile ya Wafamasia kuingiza taarifa kwenye mfumo za kuonesha kuwa dawa zimetolewa huku wakijua kuwa hao ni wagonjwa hewa.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here