Watu 10 kizimbani wizi, unyanganyi wa silaha

0

NA DEVOTHA FULUGUNGE, DAR ES SALAAM

WATU 10 wamefikishwa katika Mahakama ya Kinondoni katika kesi mbili tofauti wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali yakiwemo ya wizi, kumiliki mali za wizi na unyanganyi wa kumia silaha.

Katika kesi ya kwanza watu saba wakazi wa jijini Dar-es-Salaam walifikishwa katika Mahakama hiyo wakikabiliwa na mashitaka matano likiwemo la wizi wa Sh. milioni 10.2.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Lilian Silayo.

Waliyofikishwa mahakamani ni pamoja na Alex Joel (35) Mkazi wa Msasani Macho, Heriel Kimario (31) Mkazi wa Goba mtaa wa Ulugwini, Deodati Kimario (38) Mkazi wa Goba, Denis Tarimo (34) Mkazi wa Goba.

Wengine ni Winfrida Mwita (36) Mkazi wa Goba, Chikaka Raobi (45) Mkazi wa Goba mtaa wa Muungano na Gerald Mshanga (29) Mkazi wa Tegeta “A”.

Awali Wakili Mwendesha mashitaka wa umma ASP Hamisi Said kupitia hati ya mashitaka alidai, Agosti 6, 2020 eneo la Goba mtambani wilaya ja Ubungo jijini Dar-es-Salaam mshtakiwa Joel, Kimaro, Daud na Mwita walikula njama kwa nia ya kutenda kosa la wizi.

Katika shitaka la pili Said alidai, Agosti 6, 2020 eneo la Goba Mtambani jijini Dar-es-Salaam mshitakiwa wa 1, 2,3 na 4 waliiba mali za mtu aliyejulikana kwa jina la Marcelina Dallas zenye thamani ya Sh. 10,266,000.

Shitaka la tatu, ni kukutwa na mali zilizodhaniwa kuwa zilipatikana kwa njia ambayo siyo halali ambalo  lilimuhusu mshtakiwa wa 6 Ambaye ni Chikaka Raobi ambapo Septemba 23,2020 eneo la Goba mshtakiwa huyo alikutwa na seti nne za viti na meza vyenye thamani ya Sh. 1,500,000 vilivodhaniwa kupatikana kwa njia ambayo siyo halali.

Katika shitaka la nne, ilidaiwa Septemba 14, 2020 mshtakiwa Mwita alikutwa akimiliki mali ambayo ilidhaniwa kupatikana kwa njia ambayo siyo halali, mali hiyo ni friji na capte vyenye thamani ya sh. 2,050,000.

Said aliendelea kudai kuwa shtaka la tano, Septemba 15, 2020 mshitakiwa Aloyce alikutwa na oven ya kupikia (cooking oven ) yenye thamani ya sh. 300,000 ambayo iliibwa au ilipatikana kwa njia ambayo siyo halali.

Mwendesha mashitaka alidai upelelezi bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo.

Mbali na hapo, mshitakiwa wa 1 mpaka wa 6 walikana kutenda makosa hayo na mshitakiwa wa 7 alikiri kutenda kosa.

Hakimu Silayo alisema dhamana iko wazi na kutaja masharti ya dhamana kwa makundi.

Mshitakiwa wa 5,6 na 7 wao walitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya milioni tatu kila mmoja sambamba na barua za utambulisho.

Aliendelea kutaja masharti ya dhamana kwa mshtakiwa wa 1,2,3 na 4 ambapo wao  walitakiwa kuweka pesa taslimu kwenye akaunti kiasi cha shilingi milioni kumi kila mmoja na kama ingeshindikana wawe na wadhamini wawili kila mmoja ambapo wadhamini walitakiwa kuleta hati ya kitu kisichohamishika chenye thamani ya Sh milioni tano na kuendelea.

Waliyokidhi masharti ya dhamana ni mshitakiwa wa 5 (Winfrida Mwita) na mshitakiwa wa 6 (Chikaka Raobi).

Kwa upande wa mshitakiwa wa 1, 2,3,4 na 7 wao walirudishwa rumande baada ya kutotimiza masharti ya dhamana na Hakimu Silayo alihairisha kesi hiyo hadi Januari 18 kwa ajili ya hoja za awali.

Wakati huo huo watu watatu wamefikishwa katika Mahakama hiyo wakikabiliwa na Shitaka la unyan’ganyi wa kutumia silaha aina ya panga.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Siffa Jacob.

Waliyofikishwa ni Peter maduhu(22) Mkazi wa Kimara, Daudi Elias maarufu kama Dangote (24) Mkazi wa Kimara na Goodluck Mkoma (32) ambaye ni Mkazi wa Kimara Stop Over.

Kupitia hati ya mashitaka Wakili wa Serikali Veronica Mtafya alidai, Novemba 28, 2020 eneo la Mbweni Mpiji wilayani Kinondoni jijini Dar-es-Salaam washitakiwa waliiba simu mbili, runinga, laptop, pesa taslimu na Dola za Marekani 100.

Wakili Mtafya aliendelea kudai kuwa, washtakiwa hao waliiba simu mbili aina ya iPhone 11 PRO MAX yenye thamani ya Sh. 3,200,000, Samsung note 7 Edge Sh.420,000, runinga moja yenye thamani ya Sh. 3,620,000, laptop aina ya HP yenye thamani ya Sh. 1,000,000, pesa taslimu sh. 160,000 na Dola za Marekani 100 ambazo ni mali za Noela Yusuph Abas.

Mbali na hapo wakili alidai baada na kabla washtakiwa hao walimtishia Abas kwa panga kwa nia ya kujimilikisha mali hizo.

Washitakiwa walikana kutenda kosa na wakili alidai upelelezi bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri.

Hakimu Jacob alisema shitaka linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria na kesi kuhahirishwa hadi Januari 18, 2021 kwa kutajwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here