Watanzania waanza kupiga kura, wanaamua hatima ya miaka mitano ijayo

0

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 

Watanzania milioni 29.75 waanza kupiga kura leo Jumatano Oktoba 28, 2020 kuchagua Rais, wabunge na madiwani watakaoongoza kwa miaka mitano ijayo.

Hatua hiyo inakuja baada ya kumalizika kwa siku 63 za kampeni zilizovuta maelfu ya watu katika mikutano ya wagombea urais.

Lakini mikutano ya wagombea ubunge na udiwani ilivuta wananchi wachache na hivyo kuwalazimisha kutumia mbinu mbadala ya kujinadi, ambayo ilikuwa ni kuwafuata vijiweni, majumbani na katika sehemu zao za shughuli za kiuchumi.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage alisema jana Jumanne Oktoba 27, kuwa kati ya wapigakura hao, milioni 29.188 wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la NEC na 566,352 wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kaijage alisema katika uchaguzi, Tume itatumia jumla ya vituo vya kupiga Kura 81,567 vikiwemo vituo 80,155  vinavyotokana na daftari la NEC na vituo 1,412 vya ZEC.

Vyama 15 vimesimamisha wagombea urais.

“Vyama vyote 19 vyenye usajili wa kudumu vinashiriki uchaguzi huu kwa kusimamisha wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Kwa mujibu wa takwimu, kuna jumla ya wagombea 1,257 katika nafasi za ubunge na jumla ya wagombea 9,237 katika udiwani,” alisema Kaijage.

Alisema Tume imechambua takwimu kwa kuangalia uwiano wa jinsia katika nafasi zote za uongozi zinazogombewa. Wanawake wanaowania urais ni wawili kati ya 15, sawa na asilimia 13. Na wagombea wenza wanawake ni asilimia 33.

Kaijage alisema wagombea wanawake kwa nafasi ya ubunge ni 294, sawa na asilimia 23 na madiwani wanawake walioteulowa ni 669, sawa na asilimia 7.2 ya wagombea.

 “Tume imekamilisha maandalizi yote muhimu, vikiwemo vifaa vya uchaguzi hadi kufikia leo vifaa vyote vimefikishwa kwenye halmashauri na kata mbalimbali na hivi sasa zoezi la kusambazwa vifaa hivyo kwenye vituo vya kupiga kura linaendelea,” alisema Kaijage.

Pia aliwataka wananchi waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi ili kutimiza haki yao ya kikatiba bila hofu ili kuchagua viongozi kwenye nafasi za uongozi.

Kaijage alisema Tume inategemea kuanza  upigaji kura saa 1:00 asubuhi  na wanategea  kumalizika  saa 10:00 jioni na kwamba askari mwenye sare  atasimama nyuma ya mtu wa mwisho kituoni.

Alisema mambo ambayo hayaruhusiwi siku ya uchaguzi, ikiwemo kuvaa sare za chama cha siasa katika vituo vya kupiga kura na kuendesha kampeni

Aidha alisema taratibu za utangazaji wa matokeo akinukuu ibara ya 41 kifungu kidogo cha saba cha katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inasema mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani ni ya NEC, wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wa uchaguzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here