Wanaodaiwa NDC Bil. 7.5 mikononi mwa TAKUKURU

0

NA MWANDISHI WETU, MANYARA

SHIRIKA la maendeleo la Taifa (NDC) limeipa jukumu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU Mkoa wa Manyara la kukusanya Sh. bilioni 7.5 kwa wakulima waliokopa matrekta tangu mwaka 2018.

Akizungumza mjini Babati, Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu alisema Serikali kupitia shirika lake la NDC iliwakopesha wakulima matrekta katika mipango yake ya kuhakikisha wanaondokana na jembe la mkono.

Makungu alisema katika mkoa wa Manyara, wakulima wa wilaya za Babati, Mbulu, Kiteto na Simanjiro walihamasishwa na kukopa matrekta hayo yenye thamani ya shilingi bilioni 7.5.

Amewapongeza wakulima wa wilaya za Babati na Mbulu waliochukua mikopo hiyo kwani wengi wao wameonyesha ushirikiano kwa maofisa wetu na wanaendelea kulipa madeni wanayodaiwa kulingana na mikataba yao.

“Katika wilaya ya Kiteto kumejitokeza baadhi ya walaghai wanaowahamasisha wakulima waliokopa matrekta hayo kutofanya marejesho kwa maelezo kuwa mikopo ya serikali huwa hairejeshwi,” amesema Makungu.

Amedai kuwa anapendana kuwajulisha umma wa Manyara kuwa uhamasishaji huo ni haramu na wakulima waliochukua mikopo wawapuuze na kuendelea kuirejesha.

Amesema wameanzisha uchunguzi wa wahusika wanaohusika na ulaghai huo na watakaobainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria bila kujali hadhi zao katika jamii.

Ametoa rai kwa wawakilishi wa wananchi wabunge na madiwani washirikiane kuwahamasisha waliochukua mikopo warejeshe ili wengine wakopeshwe matrekta.

“Nia ya serikali ni kuwawezesha wakulima wengi zaidi kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija,” amesema Makungu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here