Wanaochochea vurugu uchaguzi: Viongozi wa dini wacharuka kila kona

0

NA WAANDISHI WETU, SIMIYU, SHINYANGA

Viongozi wa dini katika maeneo tofauti nchini wametahadharishwa wananchi kutokuunga mkono vitendo vyovyote vinavyoweza kutokea na kusababisha  uvunjifu wa hali ya amani na utulivu uliopo hivi sasa hapa nchini.

Miongoni mwao ni Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga ambapo jana iliwataka wananchi wote wenye kuthamini amani kutokubali kutumiwa na wanasiasa wakati huu wa kipindi cha uchaguzi hasa siku ya upigaji kura Oktoba 28, mwaka huu.

Akitoa taarifa mbele ya waandishi wa habari, Kaimu mwenyekiti wa Kamati ya Amani mkoani Shinyanga, Sheikh Khalfan Ally, alisema kila mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha anailinda amani iliyopo hivi sasa hapa nchini kwa vile iwapo itatoweka haitokuwa na mbadala.

Sheikh Ally alisema iwapo amani itatoweka wahanga wakubwa watakuwa ni wanawake, wazee na watoto hasa wale wenye mahitaji maalumu miongoni mwa jamii na pia hapatakuwepo shughuli yoyote ya kimaendeleo inayoweza kufanyika.

“Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga inatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla kutokubali kutumiwa na wanasiasa wakati huu wa kipindi cha uchaguzi hasa siku ya upigaji kura Oktoba 28, mwaka huu,”

“Tunawaasa wazazi na walezi wa familia nchini kujiepusha na kushawishiwa kushiriki maandamano, fujo, na vurugu zozote wakati wa uchaguzi kwa kuwa matokeo yake watakabiliana na mkono wa sheria wakati wahamasishaji wa vurugu wakiikimbia nchi na kuwaacha wachache wakihangaika,” alieleza Sheikh Ally.

Katika hatua nyingine Kamati hiyo imetoa rai kwa baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kidini hapa nchini wanaojitokeza kuungana na watu wanaohamasisha vijana kujitokeza barabarani kuandamana ikiwemo kukaa kwenye vituo vya kupigia kura waache tabia hiyo mara moja.

Sheikh Ally alisema kiongozi ye yote wa kidini anayeungana na kundi, watu ama Chama cha Siasa kuhamasisha vurugu ni kwenda kinyume na misingi ya dini yake na kwamba wakumbuke upigaji wa kura hauendeshwi kwa misingi ya kidini.

“Sisi Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga, tunatoa wito na kuwaomba viongozi wote wa madhehebu ya kidini mkoani hapa na nchini kote kwa ujumla wajiepushe kushiriki ama kuunga mkono vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uvunjifu wa amani,” alieleza Sheikh Ally.

Kaimu Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa wakazi wote wa mkoa wa Shinyanga waliojiandikisha kupiga kura wajitokeze kwa wingi Oktoba 28, mwaka huu kwenda vituoni kupiga kura na wawachague viongozi wanaowapenda wao na siyo wale wanaopendwa na watu wengine.

Kwa upande wao viongozi wa dini wa Mkoa wa Simiyu walikutana na kupitisha maazimio likiwemo la kuhakikisha wanahimiza waamini wao kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Uchaguzi zinazotolewa na Tume ya Uchaguzi siku ya Uchaguzi.

Pia waliazimia kuwa ni jukumu la viongozi wa dini kuomba kwaajili ya amani na uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano huo Fuleule Kija kutoka Busega kata ya Lamadi alisema wameshajionea machafuko katika nchi nyingi za bara la Afrika ambapo wananchi huteseka kwasababu ya uchu wa madaraka wa baadhi ya watu.

Aliwataka watanzania kupuuza wito wa kuandamana na kusema kuwa mwisho wa siku wanaoteseka ni watoto, akinamama na wazee.

Naye Sheikhe wa Wilaya ya Meatu, Issa Bin Mussa maarufu Nyangenyange alisema wananchi wanapaswa kuwapuuza viongozi wa dini wanaosimama kwenyemajukwaa na kupangia watu cha kufanya.
Alisema hiyo si kazi ya viongozi wa dini kwani wao wapo kwaajili ya kuomba amani na kuhimiza jamii kuzingatia sheria za dini na sheria za nchi.

Naye Mchungaji Joseph Abeli kutoka Busega Kata ya Lamadi alisema ni vema kila mtanzania kutambua kuwa amani iliyopo ndiyo inayowapa nafasi ya kufanya hata uchaguzi na shughuli zingine za maendeleo na kuonya kuwa uvunjifu wowote wa amnai ni hatari kwa maendeleo ya taifa na haina mbadala.

Wakati huo huo Shura ya Maimamu kwa kushirikiana na Baraza Kuu, Taasisi na Jumuiya za Kiislam zimevitaka vyombo vya dola kuwashughulikia pasipo upendeleo viongozi wa dini hususani ya Kiislam watakaosimama kwenye majukwaa ya kisiasa kunadi wagombea ili kunusuru Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana  kwa niaba ya Mkuu wa Shura ya Maimamu Mjumbe wa Shuraa hiyo, Sheikh Juma Ramadhan Juma alisema, sasa imejitokeza tabia ya viongozi wa dini si mara moja kusimama kwenye majukwaa ya kisiasa na kuwataka watu wamchague kiongozi fulani jambo ambalo linaweza kuleta athari.

Alisema kuwa, viongozi wa dini hawapaswi kusimama katika majukwaa ya siasa na kuwanadi wagombea na badala yake wawaachie wanasiasa wenyewe na kwamba wananchi ndio wataamua kwenye masanduku ya kura.

Alisema, hakuna kikao chochote kilichokubaliana kwamba Waislam wampigie kura mgombea fulani na kutaka masuala hayo waachiwe watanzania wenyewe ndio wataamua nani anafaa kuwa kiongozi wao si vingine.

“Kwa niaba ya Shura ya Maimamu, naomba Jeshi la Polisi kuwashughulikia viongozi wa dini hasa ya Kiislam wanaosimama kwenye majukwaa ya kisiasa iwe ya CCM au ya upinzani ili kuepusha kuhatarisha amani,”alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here