Wananchi wajitokeza kwa wingi kupiga kura

0

>>Waipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa maandalizi mazuri

>> Wasema uchaguzi wa mwaka huu umeenda vizuri kuliko uliopita

NA WAANDISHI WETU, PEMBA

ZOEZI la upigaji kura nchini, limeripotiwa kwenda vyema, huku vituo navyo vikifugulia kwa wakati na vifaa vya kupigia kura kufika kwa wakati.

Waandishi wetu waliotembelea vituo mbali mbali, walisema wananchi wengi wao, walifika kwenye vituo hivyo baina ya saa 11:55 na saa 12:00 asubuhi ingawa wengine walikwenda chini ya hapo.

Wakizungumza na waandishi wetu, wapiga kura hao walisema vituo vilifunguliwa kwa wakati uliopangwa na  ilipofika majira ya saa 1:00 asubuhi, vilianza kazi kwa kasi.

Walisema, hata watendaji wa Tume za Uchaguzi ya Zanzibar ZEC na ile ya Taifa NEC, walifika kwa uharaka na kutoa huduma kwa wananchi wanaoingia vituoni, jambo ambalo linaweza kusababisha hadi ikifika saa 9:00 huwenda wakawa wameshamalizika.

Ali Khamis Makame ambae ni mpiga kura kwa mara ya kwanza, akiwa kituo cha Fidel- Castro jimbo la Wawi alisema, hali iko shwari.

“Mimi nilitoka nyumbani nikiwa na woga, lakini hadi nafika kituoni sijazuiwa na wala sikutumia muda mrefu kituoni, nawaomba wengine waje,’’alisema.

Aisha Khamis Haji miaka 60, alisema kati ya chaguzi zote alizowahi kushiriki, wa mwaka huu 2020, umekuwa bora zaidi kwa kule kuimarisha ulinzi.

“Jengine ambalo naliona ni zuri liliowekwa na tume zetu kwa sisi wazee, walemavu, wenye watoto wachanga na wajawazito tumewekewa foleni yetu, hili linapunguza machungu,’’alieleza.

Akizungumza kwenye eneo hilo, Waziri wa Nchi afisi ya Makamu wa Pili wa rais Mohamed Aboud Mohamed, alipongeza kasi ya watendaji wa Tume.

Alisema zoezi hilo huwenda likawa “laini mno,” jambo ambalo litawapa nafasi na fursa ya wananchi wengi kupiga kura.

“Zoezi liko rahisi na laini mno, na inaonekana kwa uchaguzi huu wa mwaka 2020, wananchi wamepata muamko mkubwa, maana leo kila kituo unachopita unakuta watu wengi,’’alieleza.

Wananchi wa Jimbo la Chake Chake wa vituo vya skuli ya Michakaini na Mdungu, walisema utaratibu wa kuweka foleni za wanawake na wanaume mbali mbali ni jambo jema.

Khamis Nahoda Juma (55) na Fatma Haji Khamis (20) waliokuwa vituo vya skuli ya msingi Michakaini walisema, kama chaguzi zote zingekuwa kama wa mwaka huu, kusingekuwa na lawama.

Hamad Juma Hamad (19) na Asha Himid Mmanga wa vituo vya Micheweni Jimbo la Micheweni, waliwataka wenzao ambao wana hofu kufika vituoni.

Omar Hamad Jabu (30) na Fatma Khamis Muhidini (50) wa kituo cha skuli ya Jadida Jimbo la Wete, wakizungumza na vyombo vya habari, walisema zoezi hilo liko vyema na wala halijatawaliwa na vurugu.

Mgombea uwakilishi wa Jimbo la Mtambile kwa tiketi ya CUF Asha Said Suleiman alisema, zoezi ni zuri na vituo vilifunguliwa kwa wakati uliopangwa.

“Mimi mwenyewe hadi saa 3:50 asubuhi sijapiga kura, lakini nimesharidhika nalo maana, nilipofika skuli ya Mizingani hapa nimelifurahia mno na jinsi ulinzi ulivyoimarishwa ,’’alieleza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here