Walibya wakubaliana kuhusu mpango wa kuandaa uchaguzi

0

TRIPOLI, Libya

UMOJA wa Mataifa umesema Walibya wanaoshiriki katika mazungumzo yanayosimamiwa na umoja huo wamekubaliana kuhusu mpango wa awali wa kuandaa uchaguzi katika kipindi cha miezi 18 ijayo.

Mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa yanafanyika Gammarth, Tunisia, wakati juhudi za kidiplomasia zikiongezeka ili kuvimaliza vita vilivyodumu kwa karibu muongo mmoja kwenye nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Kaimu Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya, Stephanie Williams, amesema kuwa wajumbe wa pande zinazohusika na mzozo wa Libya wamefikia makubaliano hayo na kuweka wazi hatua za kufanyika kwa uchaguzi mkuu, ikiwemo makubaliano ya kimsingi ya katiba.

“Leo washiriki wa mazungumzo ya kisiasa ya Libya, wamefikia makubaliano ya awali ya kumaliza kipindi cha mpito na kuandaa uchaguzi wa rais na bunge utakaokuwa huru, wa haki, utakaozijumuisha pande zote na utakaokuwa wa kuaminika,” alisema Williams.

Mazungumzo hayo yanalenga kuanzisha mfumo na serikali ya muda itakayoandaa uchaguzi pamoja na kutoa huduma katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita vya miaka mingi pamoja na kuathiriwa na janga la virusi vya corona.

Williams amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuingia haraka kwenye “uchaguzi wa kitaifa ambao utakuwa huru na utakaozingatia uhuru wa kujieleza na haki ya kukusanyika.”

Mazungumzo hayo ya Tunisia yanafanyika sambamba na mazungumzo ya kijeshi ndani ya Libya kwa lengo la kujaza taarifa za makubaliano ya kihistoria ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Oktoba.

Wajumbe 75 walichaguliwa

Umoja wa Mataifa uliwachagua wajumbe 75 kushiriki katika mazungumzo hayo ya kisiasa ili kuziwakilisha taasisi zilizopo na jamii za watu tofauti wa Libya, hatua iliyozusha ukosoaji mkubwa kuhusu mchakato huo na uaminifu wake.

Hata hivyo, makubaliano hayo yaliyofikiwa siku ya Jumatano, yaligubikwa na kuuawa kwa kupigwa risasi wakili maarufu na mtetezi wa haki za wanawake katika mji wa Benghazi ulioko mashariki mwa Libya, siku moja kabla.

Hanan al-Barassi, mkosoaji mkubwa wa ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na unyanyasaji dhidi ya wanawake, aliuawa mchana kweupe na mwanaume mwenye silaha.

Akizungumzia mauaji hayo, kaimu mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Stephanie Williams, amesema yanaashiria kitisho wanachokabiliana nacho wanawake wa Libya wakati ambapo wanasimama kidete kutetea haki.

Williams ametaka haki itendeke na wauaji wa al-Barassi wafikishwe katika vyombo vya sheria, ingawa amekataa kutoa maoni yake iwapo mauaji hayo yanahusika na mazungumzo yanayoendelea.

Amesema kutakuwa na vikwazo, kutakuwa na watu wasiotaka mabadiliko, lakini Walibya wengi wana hamu kubwa ya kurudisha enzi ya utawala halali wa taasisi zao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here