Wakulima wa korosho wapewa somo kuhusu magonjwa

0

NA  MWANDISHI WETU,TANGA

UBWIRI unga ni ugonjwa unaolikumba zao la korosho nchini Tanzania na pale usipodhibitiwa husababisha hasara kati ya asilimia 70 hadi 100. Ugonjwa huo ni wa aina ya uyoga ambao husababishwa na vimelea aina ya Oidium anacardii.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini Tanzania (TARI), tawi la Naliendele kuna magonjwa ya mikorosho zaidi ya 12 yanayo fahamika kushambulia mikorosho, kati ya hayo magonjwa matatu yasipodhibitiwa yanaweza kuleta hasara kubwa.

Mtafiti upande wa wadudu waharibifu na magonjwa ya korosho kutoka TARI-Naliendele, Dadili Majune anayataja magonjwa hayo mbali na ubwiri unga (powdery mildew) kuwa ni blaiti ya mikorosho (cashew leaf and nut blight), pamoja na debeki (cashew dieback).

 Anasema ubwiri unga hushambulia maeneo machanga na laini kwenye mkorosho kama vile majani, maua na matunda (tegu na bibo). Dalili za ugonjwa huo katika maeneo yaliyoshambuliwa ni unga unga mweupe au wa kijivu.

 Kwenye majani ugonjwa huo hushambulia pande zote za majani na huchukua muda mfupi kufunika jani zima isipokuwa majani yaliyokomaa ambayo huwa hayashambuliwi. Kwa upande wa maua, yakishashambuliwa hukauka na kushindwa kufunguka na hivyo kukwamisha uchavulishaji hatua ambayo ni kiini cha hasara kwenye mikorosho.

 Kwenye matunda, yaani mabibo, yakishashambuliwa husinyaa na kudumaa kabisa na ngozi huharibika na kuchafuka. Mabibo pia hupasuka pasuka kadri yanavyojaribu kupanuka hivyo hubakia madogo kwa umbo na korosho hubakia chafu na ikivunwa hutengwa kwenye daraja la pili.

Mtafiti anasema ugonjwa huo hushamiri sana wakati wa kiangazi, hasa kuanzia mwezi Juni hadi Agosti. Ugonjwa huo hupendelea mazingira ambayo usiku ni baridi na mchana ni joto.

 Njia za kudhibiti ugonjwa ni pamoja na ile ya asilia ya kuondoa vyanzo vya ubwiri unga. Njia hii kuchelewesha kuanza mashambulizi, kupunguza kasi ya ugonjwa na mkulima kubana matumizi ya viuatilifu.

Mbinu hiyo ya asili ni pamoja na kupunguzia mikorosho kwa kukata na kuondoa mikorosho iliyosongamana ili kutoa nafasi kwa miti iliyobaki.

Hii ni pamoja na kupunguza matawi kwa kukata na kuondoa baadhi ya matawi/ machipukizi katika mikorosho ili kupitisha vizuri mwanga na hewa ndani ya mikorosho. Mbinu hizo kutoa mazingira magumu kwa vimelea vya ugonjwa kustawi na kushamiri vizuri.

Njia nyingine ya kudhibiti ugonjwa huo ni kutumia viuatilifu vya unga au vya maji kwa kupulizia kwenye mikorosho kwa kutumia mashine.

Upuliziaji huo unaanza mara baada ya mkorosho kutoa maua walau asilimia tano, pale yanapoonesha dalili za ugonjwa lakini pia ni muhimu ukaguzi wa maua ufanyike ili kujua siku ya kuanza kupulizia. Inapobidi ni vema kuanza kupulizia dawa mikorosho kwa kuchagua maua ambayo tayari yameanza kuonyesha dalili.

Hivi karibuni kulitolewa mafunzo kwa wakulima kutoka maeneo mbalimbali yanayolima korosho nchini, lengo likiwa ni kuwapatia teknolojia mpya za kilimo bora cha zao la korosho ikiwa ni pamoja na mbegu bora na namna ya kudhibiti wadudu waharibifu na magonjwa.

Mafunzo hayo yaliyotolewa na TARI kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) yalihusisha mikoa ya Pwani, Tanga pamoja na Kilimanjaro.

Immaculata Nyaki, mkulima kutoka Kijiji cha Magamba katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga anasema kuwa, mafunzo hayo yamemwongezea uelewa zaidi katika kilimo cha korosho na hasa eneo la kukabiliana na magojwa.

 “Mafunzo yamenisaidia kutambua magonjwa ambayo yanaleta athari kwenye mikorosho na namna ya kutunza mikorosho,” anasema.

 Anatolea mfano ugonjwa huo wa ubwiri unga kwamba awali alikuwa akiona mikorosho yake inabadilika bila kujua tatizo na sasa baada ya mafunzo atakuwa makini kufuatilia changomoto yoyote ambayo itajitokeza kwenye mikorosho hasa pale atakapoona dalili za magonjwa zikijitokeza

 Bilyery Kihombo, mkulima kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani anasema kuwa, ubwiri unga umekuwa ni tatizo katika kilimo hicho kwa sababu kwenye shamba lake majani yamebadilika rangi kutoka kijani na kuwa mfano wa unga unga.

Anakiri kwamba kabla ya mafunzo hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo na namna ya kupambana nao. “Mafunzo tuliyopata ni ya msingi sana kwani yatatusaidia sana katika kuboresha zao la korosho na kuweza kuzalisha kwa tija,” anasema Kihombo.

 Bakari Kaniki, mkulima wa korosho kutoka Kata ya Okaoni katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro anasema: “Kupitia mafunzo haya nimepata uelewa mzuri sana kutunza mikorosho dhidi ya magonjwa ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya dawa za kuuwa wadudu wanaoathiri mikorosho na namna ya upuliziaji wake.”

“Lakini pia nimejifunza aina mbalimbali za magonjwa ya mikorosho, elimu ambayo tukizingatia kwa umuhimu wake kama vile kupanda mbegu bora za kisasa tutazalisha kwa wingi kuliko sasa.”

Akizungumzia mada kuhusu ubora katika zao hilo, ofisa kilimo kutoka Bodi ya Korosho, tawi la Tanga, Frank Futakamba anasema, kwa kawaida korosho zikishakomaa huanguka zenyewe chini zikiambatana na mabibo na uvunaji ni kuziokota na kuzitenganisha na mabibo kabla ya kuanguka.

 Anasema, ni muhimu kupalilia na kusafisha eneo linalozunguka mikorosho ili kurahisisha uvunaji pia ni vema kutenganisha korosho na mabibo kwani ubora wa korosho unaathirika endapo mabibo hayajakonyolewa kwa usafi na kusalia kwenye korosho.

Hali hiyo anasema husababisha kuwepo kwa ugumu katika ukaushaji kwamba hiyo inavutia wadudu kuja kutoboa na kuongeza uchafu kwenye korosho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here