Wakazi Dodoma wafurahia kutua kwa Air Bus

0

NA DOTTO KWILASA ,DODOMA

WAKAZI wa mkoa wa Dodoma wamefurahishwa na kushukuru kitendo cha Serikali kuona haja ya kurahisisha mawasiliano kwa njia ya Usafiri wa ndege na kuelezea kuwa hali hiyo itarahisisha Usafiri ikiwa ni Pamoja na  kuchochea biashara.

Hatua hiyo imekuja baada ndege  aina ya Airbus A220-300 yenye uwezo wa kubeba abiria 132, kwa mara ya kwanza kutua katika Uwanja wa ndege wa Dodoma baada kufanyiwa marekebisho makubwa ya kupanuliwa kwa njia ya kutua na kufikia urefu wa kilometa 2.8.

Ndege hiyo imetua jijini hapa na kupokelewa na viongozi mbalimbali,wananchi huku wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Bilinithi Mahenge.

Akiongea mara baada ya kuwasili kwa ndege hiyo, Dk.Mahenge alisema kutua kwa ndege hiyo kunatokana na Juhudi za Rais Dkt.John Magufuli kwa kuleta maendeleo kwa watanzania ili  kurahisisha huduma za usafiri wa anga.

Aliongeza Kuwa, Serikali imeamua kuboresha miundombinu ya huduma za usafiri wa ndege katika jiji la Dodoma ambao utawasaidia wakazi wa Dodoma kuachana na  gharama kubwa za usafiri walizokuwa wakitumia  kabla ya kuboreshwa kwa huduma za usafiri.

“Ndege hii ni kubwa itakuwa inabeba abiria 132 kwani hapa zamani tulikuwa na ndege ambayo ilikuwa inabeba abiria 12 na bei yake ilikuwa ni Sh.530,000 wakati hii bei unaenda Dar es Salaam na kurudi ,”alisema Dk. Mahenge.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini(TANROAD), Mhandisi Patrick Mfugale, alisema  awali uwanja wa Ndege wa Dodoma ulikuwa na urefu wa kilometa 2.5 lakini kwa sasa una kilometa 2.8  hivyo  ndege zenye ukubwa  wa ndege hiyo iliyotua zitakuwa zinatua jijini hapa.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa  hatua hiyo kumetokana pia na nguvu ya wanadodoma Kuwa wepesi wa kukubali maendeleo na kuruhusu maeneo yao kuchukuliwa kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo.

“Uwanja huu ulipanuliwa kwa awamu mbili ya kwanza ilikuwa kutua kwa ndege ya Bombadier yenye uwezo wa kubeba abiria 76 na hatua ya pili ni  hatua ya kupanua ili ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 132,tunashukuru tumefikia malengo lakini Mambo mengine mazuri zaidi yanakuja,”alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here