NA DOTTO KWILASA,DODOMA
MKURUGENZI Mtendaji wa Haki Elimu Dk John Kalage amesema Licha ya Serikali kuchukua hatua stahiki kuhakikisha miundombinu ya elimu inakuwa rafiki,bado mitaala Kwa baadhi ya shule zinazojumuisha watoto wenye mahitaji maalumu haikidhi mahitaji kwa wenye ulemavu.
Hatua hii inatokana na uhaba wa walimu wenye sifa na taaluma za watoto wenye ulemavu kwenye shule za elimu jumuishi.
Dk Kalage amesema hayo kwenye kongamano lililowakutanisha wadau mbalimbali wa elimu jumuishi lililoandaliwa na mradi wa elimu wa Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) jijini Dodoma,ambapo alisema kuwa miundombinu hiyo bado inahitajika ili watoto wenye ulemavu waweze kufikia malengo katika kufanya vizuri kimasomo .
Alisema jamii familia zenye watoto ambao wana ulemavu bado hawana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa kuwapeleka kuwaandikisha watoto shule kwa kidhani kuwa hawawezi kupata faida yoyote hata kama watasoma.
Alisema ili kuondoa tabia hizo,wadau was masuala ya elimu na serikali kwa ujumla ni muhimu wakaelekeza nguvu zao kwa ajili ya kuhakikisha kero zilizopo kwenye shule hizo zinatatuliwa na hatimaye wanapata haki zao za kimsingi za elimu jumuishi.
Naye Mratibu wa mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) Ansila Mavandu ameiomba serikali na wadau wa elimu kuwekeza kwa nguvu zote kwenye mpango mkakati wa elimu jumuishi,ili watoto hao wenye ulemavu waweze kupata elimu itakayowawezesha kufikia malengo yao ya kitaaluma.
Mavandu ambaye alimwakilisha mkurugenzi wake alisema ili shule za elimu jumuishi ziweze kuondokana na kero,serikali na wadau wa elimu ni muhimu zikawekeza kwa kutenga bajeti ya kutosha ambayo itakayowezesha kuondoa kero hizo zilizopo kwenye shule hizo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) Askofu George Mwita,alisema wao Kama wadau wa elimu wataendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya kuendeleza Sekta ya Elimu hapa nchini ili kuimarisha utoaji wa Elimu Jumuishi katika Jiji la Dodoma.
Alisema wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu ,kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu kielimu ili nao waweze kupata haki yao ya kimsingi ya elimu Kama watoto wengine.
Kwa upande wao wadau wa elimu jumuishi walioshiriki katika kongamano hilo wakiwemo Ofisi ya Tamisemi,Tenmen ,Tcf,Tie, Add,Shivyawata,Moest, Haki Elimu na makundi ya kijamii walisema kuwa elimu hiyo itawasaidia kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum na kuwatatulia kero zinazowakuta.
Akizungumza kwa niaba yao Rogathe Makupa Mkuu msaidizi wa Shule ya Msingi Nkuhungu alisema wamepata mafunzo juu ya Elimu Jumuishi ambayo itawawezesha kuwabaini watoto wenye mahitaji maalumu tofauti na huko nyuma ambapo hivi sasa watahakikisha watoto hao wanafanya vizuri kwenye masomo na hatimaye wanafaulu kimasomo.