Viongozi wa dini wazidi kukemea lugha za uchochezi

0

>> Wasema viongozi wa kisiasa wanaotaka kumwaga damu kwa kisingizio cha kuingia Ikulu wasichaguliwe

>> Wasisitiza hakuna Kanisa wala Msikiti lenye mgombea na anayepaswa kuungwa mkono na waumini

Na Mwandishi Wetu

VIONGOZI wa dini maaskofu na masheikh wazidi kukemea kwa vikali kauli na vitendo vya kichochezi vilivyotolewa na Sheikh Issa Ponda, ambaye ni kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu kuwa waislamu watampa kura za ndiyo Tundu Lissu.

Wa kwanza waliotoa kauli za kupinga kauli za Ponda ni pamoja na Mufti Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania(BAKWATA), Sheikh Abubakar Zubeir na Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi, kuwa kauli kichochezi za kidini zinazotolewa na viongozi wa kidini, zikiashiria ubaguzi wa dini katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu zisipewe nafasi.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, uliofanyika juzi, wilayani Korogwe, mjini Tanga, Mufti Zubeiry, alisema udini kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu haupo na kwamba, vitabu vitukufu vinakataza utengano wa kidini.

“Anayefanya masuala ya udini, akajidai yeye ana Uislamu na imani kamili, huyo amekwenda kando na maagizo na mafunzo ya Uislamu. Nikuthibitishie mheshimiwa, suala la udini halipo kwa sababu limekatazwa na Mungu katika aya ya 285, kipande cha katikati kinachosema ‘hatumtengi yeyote katika mitume yake Mwenyezi Mungu,” alisema.

Naye, Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, imewataka viongozi wa dini ya Kiislamu, wasichanganye  dini na siasa kwa sababu wanaweza kusababisha kutokea kwa uvunjifu wa amani na utulivu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ambapo alisema Sheikh Ponda alipanda katika jukwaa la kisiasa na kusema mambo yasikuwa na uhakika nayo.

Katika maelezo yake, Sheikh Mfaume, alisema Sheikh Ponda, aliwataka  waumini kutokaa kimya, endapo matokeo ya uchaguzi yatakuja kinyume na matarajio yao ya kisiasa, jambo hilo ni kinyume na taratibu za nchi zilizowekwa na kumtaka kufanya siasa na dini kwa wakati mmoja wakati huu ambao taifa limeamua kuwa mstari wa mbele na kudumisha amani iliopo.

Alisema Ofisi ya Mufti Zanzibar, imesema haitambui kabisa makubaliano hayo na wala haikubali kauli hiyo, hivyo imewataka viongozi wa dini, kutochanganya dini na matakwa ya kisiasa, kwani ni kinyume na muongozo wa vitabu vya dini na kwamba, pia ni uchochezi na uvunjifu wa amani.

“Tanzania haikuanzisha mfumo wa vyama vya kisiasa kwa misingi ya kidini na mtazamo wa kwamba, dua hazitokubaliwa na Mungu hatotuelewa. Huo ni upotoshaji wa kidini na mtazamo huo haukubaliki katika dini,” alisema.

Alisema kila raia ana uhuru wa kuchagua kiongozi anayemtaka, ambaye anahisi atatekeleza mahitaji yake na kwa upande wa dini, inawataka viongozi kuhubiri amani, usawa na upendo na kuacha kuhubiri mambo ambayo yatalea utofauti baina ya watu.

Katibu huyo, alisema Sheikh Ponda, siyo msemaji wa Waislam Tanzania, mwenye dhamana ya kusimamia Waislamu wote kwa Tanzania Bara ni Mufti wa Tanzana na kwa Zanzibar ni Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini limesema haliko tayari kuchokozeka kipindi hiki cha uchaguzi mkuu na atakayelichokoza na kuiingiza nchi kwenye shida, watamshughulikia kwa mujibu wa sheria.

Pia, viongozi wa dini wamewataka viongozi wa siasa, kutohatarisha amani kwa kumwaga damu za watu kwa kigezo cha kutaka kuingia Ikulu jambo ambalo halikubali na MwenyeziMungu hawezi kulipa kipaumbele.

Katika Kongamano la Amani la Viongozi wa Dini, lililofanyika jijini Dar es Salaam, jana, chini ya Askofu Mkuu na Mwanzilishi wa Wapo Mission International, Sylvester Gamanywa.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salam, Lazaro Mambosasa, alisema jeshi hilo limejipanga kikamilifu kuhakikisha hakuna vurugu zozote zitakazojitokeza kipindi cha uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Jumatano ya wiki ijayo.

“Ninasema mwaka huu tumejipanga kikamilifu, hivyo hatuko tayari kuchokozeka na siyo rahisi kutuchokoza, atakayetuchokoza tutashughulika naye kwa mujibu wa sheria,”alisema.

Alisema amani iliyopo ni matunda ya kazi kubwa iliyofanywa na waasisi wa taifa, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anaendeleza kuidumisha.

Pia, aliwataka wananchi kupuuza maneno ya vitisho kutoka kwa wanasiasa mbalimbali, badala yake wajitokeze kutekeleza haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Amani nchini, Alhad Mussa Salum, aliwataka wagombea kuacha kutumia damu na miili ya Watanzania kama daraja kuwaingiza madarakani.

Alisema wagombea wanatakiwa kuwa na hofu ya Mungu, kutumia lugha za heshima na kukubaliana na matokeo kwani ushindi unapangwa na Mwenyezi Mungu.

“Natoa wosia kwa wagombea wote, waache kutumia damu na miili ya wananchi kama madaraja ya kuwaingiza madarakani, vivyo hivyo wananchi mnapaswa kuzingatia taratibu na sheria za nchi katika utekelezaji wa haki yao ya kupiga kura,” alisema.

Aliwataka wadau wote wa uchaguzi, kutanguliza uzalendo kwani ndio chachu ya kuimarika kwa amani wakati na baada ya uchaguzi na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama, visimamie haki na uadilifu ili kuvuka katika kipindi hiki chenye joto kali la kisiasa kwa amani

Naye, Askofu Mkuu na Mwanzilishi wa Wapo Mission International, Gamanywa, alisema amani ni jambo lililotajwa katika vitabu vya dini zote nchini, hivyo ni budi kulipa kipaumbele.

Alisema amani haitokei bila kutafutwa, hivyo kila mtu atimize wajibu wake kuhakikisha amani inatawala katika kipindi cha uchaguzi na baadae.

“Wapo wanaodai kuwa viongozi wa dini hatutetei haki, sisi tunaweka kipaumbele amani kwa sababu ni jambo lililotajwa kwenye vitabu vya dini na halibadiliki,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Al-Hikma, Nurdin Kishk, aliwataka wananchi kuwakataa wanasiasa wanaoonyesha viashiria vya uvunjifu wa amani.

“Amani siyo jambo lililokuja kimasihara, hivyo tunatakiwa kuendelea kuitunza na kuhakikisha taifa linabaki na misingi yake ya haki, usawa na uadilifu,” alisema.

Naye, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa, alisema mataifa kadhaa ulimwenguni, yameshindwa kudumisha amani, lakini Tanzania imefanikiwa, hivyo wananchi wasikubali michakato ya kisiasa itumike kuiharibu tunu iliyopo kwa muda mrefu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here