Viongozi wa dini: Walioshindwa uchaguzi wawe wavumilivu

0

NA MWANDISHI WETU

BAADHI ya viongozi wa kiroho mkoani Dodoma wamewashauri wagombea wa nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020, na matokeo ya mshindi wa urais kutangazwa jana Oktoba 30, kuhakikisha wanaridhika na matokeo waliyoyapata na kushirikiana katika kujenga nchi.

Akizungumza na East Africa Television Askofu Mkuu wa Makanisa ya Philadelphia Gospel Assembly, lenye makao makuu yake jijini Dodoma Dkt. Yohana Masinga, amesema wagombea walioshindwa wasikate tamaa kwani wanatakiwa kujaribu kipindi kijacho.

Kwa upande wake Askofu wa kanisa la AGT Ipagala Dk. Evance Chande, amesema kuwa wagombea walioshindwa ni kutokana na kile walichopanda kwa wananchi na hivyo amewaomba washirikiane na washindi.

Kwwa upande wao Viongozi wa Kamati ya Amani Mkoani Rukwa Wameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa utaratibu mzuri waliouweka katika vituo vya kupigia kura hali iliyopelekea kuondoa msongamano na wapiga kura kutimiza haki yao ya kikatiba bila ya bugudha wala kupoteza muda kwa kusimama kwenye foleni muda mrefu katika vituo hivyo.

Aidha, viongozi hao wametanguliza Shukrani zao kwa Mwenyezi  Mungu kwa kujalia hali ya utulivu na amani wakati wote wa kupiga kura na kuwashukuru Watanzania kwa kuzingatia maelekezo ya Tume katika muda wote wa zoezi hilo.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika alisema.

“Tumeshuhudia katika vituo vyetu vya kupigia kura hali ikiwa shwari kabisa, na wapiga kura katika maeneo mengi nchini wameshuhudia kuwa kulikuwa na utengamano na utulivu mkubwa san ana tunawashukuru watanzania kwa kuzingatia maelekezo ya Tume mathalan, mara baada ya kupiga kura rudi nyumbani ili kupisha msongamano na karibu wote walifanya hivyo.”

Halikadhalika, Askofu Mwaipopo amewaomba watanzania kuendeleza utulivu wakati huu ambapo matokeo ya kura katika majimbo bado yanaendelea kutangazwa hadi pale wateule kwa nafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani watakapokula nyapo zao.

“Kikubwa ni kwamba baada ya haya matokeo kutangazwa, tuvunje makambi yetu ya kisiasa na kutoa ushirikiano kwa wale wote walioshinda na ikumbukwe kwamba, kwa nafasi ya Urais, iwe ama ulimchagua au la, ni Rais wako, vivyo hivyo kwa Wabunge na Madiwani, ni uungwana na Uzalendo kwa Taifa letu kushikamana na kuwa wamoja kwaajili ya maslahi mapana ya nchi yetu,” alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo aliwasihi wanachi wa mkoa wa Rukwa kuendeleza utulivu akiamini kuwa wanarukwa hawawezi kudanganywa na watu ambao wanadhamira ya kuanzisha vurugu baada ya kushindwa na kuwasihi kujikita kwenye masuala ya kilimo baada ya kumaliza zoezi la kuwachagua viongozi wawapendao.

“Kuna watu ambao kula yao ipo huko, akichochea ndio anaenda kula lakini wewe usipokwenda kulima hutakula, kwahiyo wanachi wawapuuze, hasa vijana, wawapuuze watu wote ambao wanataka kutuletea vurugu, lakini pili niwaonye wale wote wanaotaka kujaribu kutuvuruga ndani ya Rukwa wasijaribu, vyombo vya ulinzi na usalama viko macho sana, tuko vizuri mno tumejipanga, yeyote atakayeleta vurugu tutamshughulikia ipasavyo, tena kwa ukamilifu,” alisisitiza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here