Vinara utoroshaji dhahabu Geita hawa hapa

0

NA MWANDISHI WETU, GEITA

WAZIRI wa Madini, Doto Biteko ametaja majina matatu ya wafanyabiashara wa kununua na kuuza madini ya dhahabu (dealers) ambao wanashiriki katika vitendo vya utoroshaji dhahabu Mkoa wa Geita.

Alisema ana majina ya wafanyabiashara sita katika mkoa wa Geita, lakini ameamua kutaja majina matatu kwanza na mengine matatu ameyahifadhi.

Alisema wafanyabiashara hao wananunua dhahabu nje ya masoko na kuuza kusikojulikana kinyume na sheria zinazosimamia sekta ya madini nchini.

Waziri Biteko ametaja majina hayo kuwa ni mfanyabiashara wa Dhahabu Maduka Mbaraka, Makandaga Sita na Makaranga Kiserya.

Alitaja majina hayo katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Kituo cha Uwekezaji cha mjini Geita (EPZA) alipokuwa na kikao cha pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo wa dhahabu (brokers) na wafanyabiashara wakubwa wa dhahabu (dealers) ili kujadili namna ya kudhibiti utoroshaji wa madini.

Alisema, wafanyabiashara hao anawapa onyo la mwisho ili waweze kujirekebisha na wasipobadilika na kuacha tabia hiyo ya kutorosha madini hatua kali zinatachukuliwa dhidi yao ikiwemo kuwafilisi mali zao pamoja na kuwafikisha mahakamani.

Waziri Biteko aliwataka wafanyabiashara kuzingatia sheria na kanuni wakati wanafanya biashara hiyo ili kuepuka kufilisiwa au kufungwa kwa makosa ya kukiuka sheria za madini.

Alisema kuwa, Rais John Magufuli aliwafutia kodi na tozo nyingi za madini ambazo zilikuwa zinafikia takribani asilimia 21 ili waweze kufanya biashara hiyo bila kutorosha madini.

Alitaja kiwango cha kodi wanacholipa kwa mujibu wa sheria kuwa ni asilimia saba tu ambacho ni rafiki kwa kila mfanyabiashara hiyo .

Waziri Biteko alisema kuwa awali alipata majina ya wanunuzi 16 wa Dhahabu wanaojihusisha na utoroshaji, lakini baada ya uchunguzi wa kina walithibitisha bila shaka wanaohusika ni watu sita katika mkoa wa Geita.

Aliwataka wafanyabiashara hao wasioneane wivu wa kibiashara kwa kuwasingizia wengine kuwa wanahusika na utoroshaji baada ya kuona wenzao wanafanyabiashara vizuri badala yake watoe taarifa sahihi na zenye ukweli.

Katika hatua nyingine Waziri wa Madini Biteko,aliagiza wafanyabiashara wadogo wa Dhahabu (brokers) kununua dhahabu bila kuzuiliwa kwa kuwekewa matabaka ya Dhahabu inayotoka kwenye viwanda vya kuchenjua Dhahabu ( Elution plant) na inayotoka kwenye mialo .

Agizo hilo limekuja baada ya mfanyabiashara Charles Kazungu kulalamikia utaratibu wa kuzuia wafanyabiashara hao kununua dhahabu inayotoka kwenye vinu vya kuchenjulia badala yake wameelekezwa wanunue inayotoka kwa mchimbaji mdogo anayepata Dhahabu kwa kukamatisha kwa Zebaki.

Biteko alisema, sheria inamruhusu mfanyabiashara huyo mdogo kununua dhahabu yoyote na kiwango chochote ilimradi hawezi kuuza nje ya nchi.

Aidha, Waziri Biteko alitoa siku 30 kwa mgodi wa uchimbaji wa madini ya Dhahabu wa Geita (GGML) kulipa fidia wananchi 1,200 ambao nyumba zao zimepasuka kutokana na shughuli za uchimbaji zinazofanywa na mgodi huo.

Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Constantine Kanyasu alipongeza uamuzi wa Waziri Biteko kuchukua hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wanaotorosha madini kwani wanahujumu mapato ya serikali.

Pia alisema kitendo cha kutoa siku 30 kwa GGML kulipa fidia wananchi 1200 wa mitaa inayozunguka mgodi huo ambayo nyumba zao zilipasuka ni jambo muhimu na kutaka mgodi huo kuheshimu maagizo hayo.

Alisema siku za nyuma mgodi huo ulisingizia mlipuko wa ugonjwa wa Covid -19 lakini sasa hivi ni muda muafaka kuwalipa wananchi hao.

Waziri wa Madini Doto Biteko yuko mkoani Geita katika ziara za kukutana na wadau wa madini ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara na wachimbaji wa madini.

Wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa dhahabu Mkoa wa Geita wakiwa katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Kituo cha Uwekezaji cha Mjini Geita (EPZA) wakiwa kwenye kikao na Waziri wa Madini, Doto Biteko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here