Vandenbroeck avidanganya vyombo vya habari

0

NA MWANDISHI WETU

KATIKA vita kuna mbinu mbalimbali zinazotumika kwa ajili ya wahusika kupata ushindi, lakini sio mbinu alizotumia Kocha Mkuu wa Simba SC, Sven Vandenbroeck.

Kuelekea mchezo wa Watani wa jadi, yani Yanga na Simba SC kocha huyo alikutana na vyombo vya bari kuzungumzia mchezo huo ambao ulipigwa mwishoni mwa wiki kwa timu hizo kugawana pointi baada ya kutoka sare ya 1-1.

Kikubwa ambacho kimejitokeza kwenye mkutano huo, ni pale kocha huyo, wa Simba SC klabu alipotoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa kuwaaminisha kuwa baadhi ya wachezaji wake hawatakuwa sehemu ya mchezo huo kutokana na sababu za kuwa majeruhi.

Kwa mujibu wa Sven Vandenbroeck, Kocha Mkuu wa Simba, maandalizi ya mchezo huo yalikuwa sawa ila angekosa huduma ya Chama kwa kuwa ni majeruhi.

Kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Kagera Sugar, Chama hakumaliza dakika 90 alitoka na kumpisha Miraj Athuman dakika ya 69.

Baadhi ya mashabiki wa Simba waliichukulia hali hiyo kwa tahadhari kubwa huku wakijua fika kuwa mambo yangekuwa mazito kwa mabingwa watetezi Simba ambao kwa kukutana na Yanga kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Mkapa kwa kumkosa Chama..

Simba ikiwa imefunga mabao 21 Chama alihusika kwenye mabao saba ambapo ametoa pasi tano za mabao na kutupia mabao mawili.

Kwenye mechi mbili ambazo hakuwepo kikosi cha kwanza wala benchi, Simba iliambulia maumivu kwa kupoteza pointi sita na kufungwa jumla ya mabao mawili ndani ya dakika 180.

Ilifungwa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Nelson Mandela na ikachapwa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru.

Tukirudi kwenye taarifa ya kocha wa Simba mbele ya vyombo vya habari, taarifa hiyo ilitangazwa na vyombo mbalimbali vya habari na kuwaaminisha kuwa Chama hata kuwa sehemu ya mchezo.

Bada ya tarifa ya kocha, siku iliyofuata baadhi ya magazeti yalitoka na kichwa cha habari mfano Chama kuikosa Yanga uwanja wa Mkapa kesho.

Lakini cha kushangaza mchezaji huyo alionekana kwenye mchezo huo tena akicheza dakika 90 kinyume na magazeti yalivyofikisha taarifa katika jamii.

Baada ya mchezaji huyo, kuonekana uwanjani baadhi ya wadau wa soka ambao walipitia vichwa vya habri tu kwenye magzeti waliyashutumu magazeti yalioandika taarifa hiyo ya kukosekana Chama kwenye mchezo huo.

Baadhi ya Wadau hao walisikika wakisema”Waandishi waongo sana inakuwaaje wanaandika Chama ni majeruhi na atakosekana kwenye mchezo wa watani wajadi wakati mchezaji sio majeruhi,”.

Hata hivyo, inawezekana kabisa kuwa Chama alikuwa majeruhi kwani katika mchezo huo alionesha kiwango cha chini kinyume na kawaida yake.

Chama analalamikiwa kuwa alikosa goli ambalo kama angekuwa kwenye ubora wake asingelikosa.

Kutokana na mazingira hayo, baadhi ya wadau wanamuona Kocha Vandenbroeck hakuvitendea haki vyombo vya habari kwani alivipa taarifa ya uongo ambao umevifanya vionekane viliandika taarifa za uongo katika jamii.

Inafahamika kuwa kwenye mchezo huo zipo mbinu kama hizo lakini si kwa alizotumia Vandenbroeck kwani alivihakikishia vyombo vya habari kuwa mchezaji huyo hangekuwa sehemu ya mchezo na ndio maana vikaandika.

Kwa baadhi ya mashabiki wanaweza kulichukulia suala hili kwa wepesi lakini lazima watambue kuwa madhara yake kwa vyombo vya habari kama vile magazeti ambayo baadhi ya wasomaji wake husoma vichwa vya habari bila kilichoandikwa ndani.

Wasomaji kama hao, baada ya kusoma taarifa ile na kilichotokea, uwanjani juzi kimewashangaza na kubaki kuyalaumu magazeti.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wa habari wanapaswa kuamini taarifa zilizochapishwa siku moja kabla ya mchezo zilikuwa sahihi, wala hazikuwa za uongo kama zinavyofikiriwa na baadala yake wa kulaumiwa ni kocha wa Simba.

Ifiki pahala makocha waepuke kutoa taarifa ambazo za uhakika baadala ya kutumia mbinu za kizembe ambazo vyombo vya habari huzitumia kuwafikishia jamii.

Kwa hiki kilichotokea kwa kocha wa Simba SC, kiwe cha kwanza na cha mwisho kwani ulikuwa ni ubabaisha uliopitiliza.

Katika mpambano huo, mabingwa watetezi, Simba SC wamenusurika kupoteza mechi mbele ya watani wao wa jadi, Yanga SC baada ya kulazimisha sare ya 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Kwa sare hiyo, Yanga SC inayofundishwa na Mrundi Cedric Kaze inafikisha pointi 24 na kuendelea kushika nafasi ya pili, ikizidiwa pointi moja na Azam FC, wakati Simba SC inabaki nafasi ya tatu ikifikisha pointi 20 baadaya wote kucheza mechi 10.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Mwinyimkuu aliyesaidiwa na Frank Komba na Mohamed Mkono pembezoni mwa Uwanja na Ramadhani Kayoko na Abubakar Mturo nyuma ya makipa, hadi mapuziko Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.

Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Mghana, Michael Sarpong kwa mkwaju wa penalti dakika ya 31 baada ya beki Mkenya, Joash Onyango kumuangusha kiungo Tuisila Kisinda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).


Na ni Yanga SC ndio waliotawala mchezo kipindi cha kwanza na pamoja na kuondoka wanaongoza kwa 1-0, lakini ilipoteza nafasi nyingine za wazi mno kupitia kwa Farid Mussa na Sarpong.

Kipindi cha pili kibao kikageuka na Simba SC wakauteka mchezo, huku Yanga SC wakicheza kwa kujihami na kushambulia kwa kushitukiza.

Hata hivyo, safu ya ulinzi ya Yanga SC ikapata pigo baada ya kumpoteza beki wake tegemeo, Mghana Lamine Moro aliyeumia goti na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Said Juma ‘Makapu’ mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Safu ya ulinzi ya Yanga ikapwaya na kuruhusu mashambulizi zaidi ya watani na haikuwa ajabu Mkenya Onyango alipoisawazishia Simba SC kwa kichwa dakika ya 86 akimalizia kona iliyochongwa na kiungo wa kimataifa wa Msumbiji, Luis Jose Miquissone.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Yassin Mustafa, Lamine Moro/Said Juma ‘Makapu’ dk50, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Michael Sarpong/Yacouba Sogne dk68, Ditram Nchimbi na Farid Mussa/Zawadi Mauya dk82.

Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa, Joash Onyango, Jonas Mkude, Rally Bwalya/Hassan Dilunga dk46, Muzamil Yassin/Ibrahim Ajibu dk85, John Bocco, Clatous Chama na Luis Miquissone.

Akizungumzia mchezo huo mara baada ya kukamilika, Vandenbroeck, Kocha Mkuu wa Simba anasema kuwa kupata sare ya kufungana baoa 1-1 dhidi ya Yanga jana Novemba 7 haikuwa kwenye mpango wake wa kazi.

Sven mwenye kibarua cha kutetea taji la Ligi Kuu Bara anasema kuwa ilikuwa ngumu kuamini kwamba ameambulia sare kutokana na maandalizi waliyofanya.

“Tulikuwa na maandalizi mazuri licha ya kwamba tuliwakosa wachezaji wetu wengine ikiwa ni pamoja na Meddie Kagere na Chris Mugalu.

“Yote ambayo yametokea tunayachukua na tutayafanyia kazi kwa ajili ya mechi zijazo, haikuwa mpango wetu kuambulia sare tulikuwa tunahitaji ushindi,”anasema.Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 20 inaachwa na Yanga kwa pointi nne kwa kuwa imefikisha pointi 24 ikiwa nafasi ya pili zote zimecheza mechi 10 na kinara ni Azam FC mwenye pointi 25.

Ikumbukwe Simba na Yanga wana kutana kwa mara ya nne mwaka huu, ambapo katika michezo miwili ya Ligi Kuu Msimu wa 2019/20; Yanga walishinda mmoja baada ya kuichapa bao 1-0 Simba.

Na mchezo mwingine wa wababe hao walitoka sare ya mabao 2-2 na mara ya mwisho Simba ili iliigaragaza Yanga 4-1 kwenye mchezo wa nusu fainali wa kombe la ligi (Azam Federation Cup).

Kwa sasa timu hizo zimekuwa zikitambiana, kwa kila upande ukijivunia kufanya usajili ubora wa kikosi chake msimu wa 2020/21.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here