Utekelezaji ilani ya CCM: Mawaziri waanza kazi kwa kasi

0

NA MWANDISHI WETU

SIKU moja baada ya Mawaziri na Manaibu Waziri kuapishwa, wameanza kazi rasmi kwa kufika katika maeneo yao ya kazi na kutoa mwelekeo wa utendaji kazi ili kufikia malengo mbalimbali ya Serikali katika kuwahudumia wananchi.

Jana mara baada ya kuapishwa Rais Dk. John Magufuli aliwataka Mawaziri  kwenda kushirikiana na Manaibu wao kufanya kazi kwa bidii na kufanya maamuzi katika utekelezaji wa mipango iliyopo.

Rais Magufuli pia alisema hatosita kumwondoa yeyote ambaye hatoleta matokeo chanya katika utendaji kazi wake na kuanisha yale anayotarajia katika kila wizara.

Mbali na Rais Magufuli pia Waziri Mkuu alikutana nao mara baada ya kuapishwa kwa lengo la kupeana maelekezo ya kile kinachotakiwa kufanyika katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Huenda maelekezo hayo ndiyo imekuwa chachu ya mawaziri hao kuanza mara moja kutembelea maeneo yao wakiwa na Manaibu wao kwaajili ya utambulisho na kupeana maelekezo ya namna bora ya utendaji kazi.

Aweso amsimamisha kazi Mkurugenzi DUWASA

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso yeye alianza kwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Dodoma (Duwasa), David Palangyo na kumtaka asubiri kupangiwa kazi nyingine.

Akizungumza  jana Aweso alisema amechukua uamuzi huo kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wa Palangyo kwa maelezo kuwa Jiji la Dodoma linahitaji mtendaji mwenye kasi zaidi.

Alisema kuondolewa kwa kiongozi huyo ni ishara kuwa hatakuwa tayari kufanya kazi na watu wazembe na ambao hawaendi na kasi ya Rais Magufuli.

“Najua kaka yangu umefanya kazi kubwa, hata hivyo lazima tuwe wa kweli kwamba Dodoma tunahitaji kasi zaidi kwa kuwa macho ya viongozi yanatazama hapa, sitakuwa mpole naomba utupishe utapangiwa majukumu mengine baadaye,” alisema Aweso.

Kiongozi huyo alisema hawezi kudanganywa kwa namna yoyote kwa kuwa anaifahamu Duwasa kuliko wanavyodhani na jicho lake liko hapo.

Alisema ni wakati wa watumishi wazembe kukaa mguu sawa na ikibidi waanze kupisha wenyewe na kusisitiza a kuwa atawapa ushirikiano mkubwa watumishi wote kuanzia ngazi ya chini ambao watakuwa wakiwajibika.

Waziri Aweso aliwaonya watumishi wa Duwasa watakaoanza kukwamisha kazi ya mkurugenzi atakayeteuliwa, “hao ndio watakuwa wa kwanza kuondoka kabla ya huyo aliyepewa jukumu hilo.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi David Palangyo (aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao kilichoongozwa na Waziri wa Maji  Mhe. Jumaa Aweso. Katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga.

Dk. Ndungulile na uchumi wa kidigitali

Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk. Faustine Ndugulile alikutana na Menejimenti ya Wizara hiyo akiwa na Naibu wake Mhandisi Kundo Andrea Mathew kwa lengo la kufahamiana na kutoa maagizo juu ya utendaji kazi ili Wizara hiyo mpya isimame na kuchukua nafasi yake katika utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi.

Akizungumza na Menejimenti kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara uliopo Mji wa Serikali Mtumba, Dk. Ndugulile aliwataka watendaji wasisubiri kuagizwa, wafanye kazi kwa bidii ili kabla ya kuulizwa wawe wamejiongeza na kutekeleza.

Aliongeza kuwa, Wizara hiyo ni mtambuka, ya kimkakati na kiuchumi na inagusa Wizara zote na maisha ya kila mtanzania, ina nafasi kubwa na muhimu katika kuchangia pato la Taifa na kukuza uchumi wa nchi.

“Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha Wizara inasimama na kuchukua nafasi yake, sisi ndio wenye sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016, sheria, kanuni na miongozo mbali mbali hivyo tunaenda kugusa Wizara takribani zote zinazotumia miumboninu na mifumo ya TEHAMA na huduma za mawasiliano katika utoaji huduma na ukusanyaji wa kodi za Serikali,” alisisitiza Dk. Ndugulile na kuongeza;

“Tunapoongelea  uchumi wa kidijitali ni pamoja na ukuaji wa matumizi ya TEHAMA ambayo dunia inaitambua na kuwekeza katika teknolojia hii muhimu ambayo ina akisi akili za binadamu katika uzalishaji na utoaji wa huduma kwa jamii.”

Hivyo, aliwataka watendaji wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii huku wakitekeleza masuala yanayohusu Wizara hii mpya kama yalivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 pamoja na yaliyopo kwenye hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba mwaka huu.

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi Mathew, alisema kuwa Wizara hii mpya imebeba mambo mengi ya kijamii, kiuchumi na usalama wa nchi ambapo mawasiliano yanagusa moja kwa moja usalama wa nchi hivyo ni budi kufanya kazi kwa ubunifu, umakini na weledi mkubwa.

Aliongeza kuwa, changamoto za mawasiliano zipo hivyo tujipange kuzifanyiwa kazi katika mtazamo wa utendaji unaoleta matokeo yanayoonekana badala na wataalamu ambao ni wazungumzaji mahiri na sio watendaji

“Umefika wakati wa kutumia wataalamu wetu wa ndani kutengeneza mifumo yetu wenyewe, ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii ambayo itatengenezwa na sisi wenyewe kuendana na mahitaji ya wananchi wetu badala ya kukumbatia teknolojia kutoka nje ya nchi, tukijipanga vizuri hakuna kinachoshindikana ili Serikali iweze kuwasiliana yenyewe kwa yenyewe, na wananchi wake na wafanyabiashara kutumia TEHAMA”, alisisitiza Mhandisi Mathew.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Zainab Chaula alisema kuwa mifumo ya TEHAMA inahitaji watu makini, waadilifu na weledi ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuelekea Tanzania ya kidijitali ili kutafsiri maono ya Rais Dk. Magufuli ya kuunda Wizara mpya.

“Sisi ndio tumepewa dhamana ya kuisimamisha hii Wizara mpya isimame, misingi ipo lakini ili kuleta matokeo chanya inatupasa kuwa wazalendo kwa kuitendea haki nchi yetu kwa niaba ya wengi”, alisema Dk. Chaula

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile akiwa na Naibu wake, Mhandisi Kundo Andrea Mathew wakipokelewa katika ofisi za Wizara hiyo, Mji wa Serikali Mtumba na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula na Menejimenti mara baada ya kuapishwa.

Biteko awakumbusha watumishi vipaumbele madini

Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake wamekumbushwa kuzingatia maeneo muhimu ya kipaumbele yanayopaswa kutekelezwa kwenye Sekta ya Madini kama yalivyoanishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025, Hotuba ya Rais Dk. Magufuli aliyoisoma wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano Novemba, 2020 na Hotuba aliyoitoa Bungeni Mwaka 2015.

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Madini Doto Biteko katika kikao chake na Menejimenti ya Wizara na taasisi zake, baada ya kuteuliwa na kuapishwa tena kuiongoza Wizara ya Madini.

Biteko aliwataka viongozi hao kurejea tena maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 -2020 ili kuona ni namna gani masuala hayo yametekelezwa huku kila taasisi ikitakiwa kuhakikisha inayafanyia kazi maelekezo yote kwa lengo la kuhakikisha Sekta ya Madini inazidi kukua na kuongeza tija kwa taifa ikizingatiwa kuwa, hivi sasa sekta hiyo imeonekana kuwa kichocheo cha ukuaji kwa sekta nyingine kiuchumi.

Aidha, Waziri Biteko alisisitiza suala la ubunifu ili kuwezesha kuibuliwa kwa miradi mikubwa ambayo itapelekea kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka nje ya Tanzania na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye maendeleo na uchumi wa nchi.

Kadhalika, Waziri Biteko alizuia urasimu katika kushughulikia masuala yanayohusu sekta ya madini akilenga kuweka mazingira bora yatakayowezesha biashara ya madini kufanyika kwa ufanisi ili kuwezesha matokeo chanya katika ukusanyaji wa mapato ya serikali ikiwemo kuwezesha uwekezaji katika sekta ya madini kufanyika bila kuwepo vikwazo visivyokuwa na sababu.

“Kama kuna watu wanataka kuchimba wapewe lesni na wapewe fursa na kama kuna maoni yanayohusisha taasisi nyingine basi yafanyiwe kazi haraka. Tuwalee wawekezaji tulio nao ili waendelee kufanyakazi,” alisisitiza Biteko.

Alitaka kuwepo kwa mazingira wezeshi yatakayopelekea wafanyabishara na wachimbaji kufanya shughuli zaokwa amani ili kuwezesha kuzalishwa kwa ajira, teknolojia mpya za uchimbaji na uchenjuaji wa madini  vilevile, kuiwezesha sekta kuzalisha mabilionea wengi.

Vilevile, Waziri Biteko alitaka  kufanyiwa kazi suala la utoroshaji wa madini ili kuzuia mianya inayopelekea kutoroshwa kwa madini ambalo ameeleza awali lilianza kufanyiwa kazi vizuri lakini  kwa sasa tabia hiyo imeanza kurejea.

“Mwanzo tulikwenda vizuri lakini sasa tabia hii imeanza kujirudia. Kwenye upande madini feki tumepambana nao na tumekamata mitandao ya watu wa madini feki,” alisema Biteko.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko alitaka kuhuishwa kwa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ili iendane na matakwa ya sasa akirejea Marekebisho yaliyofanyika katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

“Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ni ya muda mrefu. Sera hii ianze kuhuishwa haraka ili iandane na matakwa ya sasa kama tulivyofanya kwenye Sheria ya madini ambayo ilitoa nafasi ya kurudisha umiliki wa madini kwa wananchi,” alisema Waziri Biteko.

Pia, alitaka suala la kuanzishwa kwa Chama Cha Wajiolojia kupewa msukumo ili likamilishwe haraka ili kuongeza uwajibikaji wa Wataalam hao katika sekta ya madini.

Aidha, katika kikao hicho, Waziri Biteko alitumia fursa hiyo kuwashukuru watumishi wote wa wizara ya madini na taasisi zake kwa kufanya kazi kwa pamoja kama familia moja na hivyo kuwezesha kupatikana kwa mafanikio makubwa  katika sekta ya madini.

“Kuna wakati niliwaeleza kiu yangu ni kujengwa kwa taasisi imara. Nashukuru hata wakati sipo kila taasisi iliendelea kufanya kazi zake vizuri. Kiu yangu ni kuona wizara na taasisi zinafanya kazi kwa pamoja ili tuwatumikie watanzania na tumalize matatizo ya wadau wetu,” alisema Biteko.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila almpongeza Waziri Biteko kwa kuaminiwa na kuchaguliwa tena kuiongoza wizara ya madini na hivyo kutumia fursa hiyo kumkaribisha tena wizara ya madini na kueleza “mafanikio yote yaliyopatikana ni yetu sote kwani sisi sote tulioongea lugha moja.”

Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa amebeba ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025 kama sehemu ya kutekeleza wajibu wa wizara ya kusimamia utekelezaji huo, Disemba 10, 2020, alipokutana na watendaji wa Wizara ya Madini Ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma.

Ummy Mwalimu: Uhifadhi wa Mazingira kugusa maisha ya watu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Ummy Mwalimu alisema atahakikisha utekelezaji wa majukumu ya kusimamia masuala ya Muungano na Mazingira yanagusa Maisha ya wananchi moja kwa moja kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili.

Akizungumza na Menejimenti ya Ofisi yake mara baada kupokelewa rasmi katika Ofisi za Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma jana, Waziri Mwalimu aliwataka wafanyakazi wote kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo chanya kwa taifa.

“Tuna jukumu kubwa la kulinda na kuhifadhi mazingira pamoja na kudumisha muungano wetu ambao ni tunu ya Taifa letu” Alisisitiza Waziri Ummy Mwalimu.

Alisema ni muhimu kuendelea kuelimisha umma juu ya umuhimu wa Muungano kwa kushirikisha vijana ambao ni taifa na leo, hususan waliozaliwa baada ya muungano kwakuwa kuna mengi ya kujifunza.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mwita Waitara alisema kuwa atahakikisha kuna kuwa na ushirikiano baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika kusimamia kwa pamoja masuala ya hifadhi na usimamizi wa Mazingira nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here