Uswisi yaimwagia Tanzania mabilioni

0

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

SERIKALI imepokea msaada wa Faranga za Uswisi milioni 15.75 sawa na Sh. bilioni 39.59 kwa ajili ya kugharamia mradi wa uboreshaji wa afya na uimarishaji wa mfumo wa afya pamoja na kugharamia program ya kutokomeza Malaria nchini.

Akipokea msaada huo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, alisema lengo kuu la msaada huo ni uanzishwaji wa huduma ya msaada wa kitaalam kwa Serikali chini ya utaratibu wa kituo cha kuimarisha mifumo ya afya kilichopo Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Aidha, James alisema msaada huo utatumika kuwezesha mpango wa kudhibiti Malaria Tanzania ili kuondoa kabisa vifo vinavyotokana na malaria na kupanua wigo wa maeneo yasiyokuwa na malaria (Malaria Free Zones).

James alisema kuwa hii ni mara ya pili katika kipindi cha siku 30 zilizopita kwa Serikali ya Uswisi kuipatia Tanzania msaada wa kuboresha masuala ya afya ambapo Oktoba 6, 2020 nchi hiyo iliipatia Tanzania shilingi bilioni 44.10  na kufikisha kiwango cha msaada katika kipindi hicho kufikia sh. Bilioni 83.7.

“Nchi zetu mbili zina uhusiano mzuri unaoendelea kukua kama unavyothibitishwa na kuongezeka kwa idadi ya miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali za Uswisi,” alisema James

James alieleza kuwa Tanzania imekuwa ikinufaika na inatarajia kuendelea kunufaika na ufadhili wa Serikali ya Uswisi, hususan katika maeneo ya afya, ajira na kipato, utawala bora, utamaduni na elimu.

Aliongeza kuwa miradi au program zinazoendelea kutekelezwa nchini kupitia ufadhili wa Serikali ya Uswisi inagharimu zaidi ya Faranga za Uswisi milioni 65.3 sawa na shilingi bilioni 164.12 na miradi iliyokamilika inagharimu zaidi ya Faranga za Uswisi milioni 59.87 sawa na shilingi bilioni 150.87.

Kwa upande wake Balozi wa Uswisi nchini, Didier Chassot, alisema tangu mwaka 2001, Uswisi kwa kushirikiana na Tanzania imekuwa ikitekeleza mapambano dhidi ya malaria kupitia program mbalimbali zenye lengo la kuisaidia nchi kufikia malengo iliyojiwekea kupitia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Chassot aliongeza kuwa kati ya mikataba miwili iliyosainiwa mmoja unalenga kuimarisha mfuko wa bima ya afya ya jamii, ambao unasimamiwa na TAMISEMI ujulikanao kama ‘’CHF iliyoboreshwa’’.

Akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Mkurugenzi wa Kinga Wizara hiyo, Dkt. Leonard Subi, alisema msaada huo utasaidia kuendeleza mafanikio yaliyopatikana hasa upatikanaji wa dawa na kuimarisha mifumo ya takwimu katika sekta ya afya nchini.

Dk. Subi alisema katika mapambano ya malaria, Tanzania imepunguza idadi ya vifo vinavyotokana na malaria kutoka aslimia 14.8 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3 mwaka 2017.

Aliongeza kuwa Wizara ya afya kwa kushirikiana na Tamisemi itahakisha msaada huo unatumika vizuri kwa kutekeleza ipasavyo malengo ya msaada huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here