Ummy Mwalimu afunguka kuhusu fursa za muungano

0

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu amesema kwamba, licha ya kuwepo kwa changamoto chache  za Muungano  wa Tanganyika na Zanzibar kuna fursa nyingi za kiuchumi ambazo wananchi wanafanufaika nazo kutokana na Muungano huo.

Aliyasema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muungano wa damu ambao  jamii imeoana tangu asili na kuleta  faida nyingi za kiuchumi na kimaendeleo kwa pande zote mbili za Jamuhuri

Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa ziara yake maalumu ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na mpango wa kunusuru Kaya Masikini Nchini, TASAF na kusema kuwa Muungano huo  umefungua   fursa nyingi za kiuchumi na kimaendeleo kwa wananchi hivyo wanapaswa kulinda,kuenzi na kudumisha Muungano huo.

“Muungano wetu unafaida nyingi sana kwa pande zote, hivyo nitoe rai kwa wananchi kuweza kulinda, kudumisha na kuenzi ili tuendelee kuneemeka nao,” alisema Waziri Ummy Mwalimu.

Aliongeza, kusema kuwa wanatambua kuna baadhi ya changamoto ndogo ndani ya Muungano huo ambazo zinatatulika na kuwaomba wananchi wasitumike kuleta chuki  Kwa lengo la kuharibu Muungano huo.

“Tunatambua kuna baadhi ya changamoto lakini zisitumike kwa kupandikizwa watu chuki kwa lengo la kuharibu Muungano wetu ambao kwa sasa unafaida nyingi kwa wananchi we,” alieleza Mwalim.

Ummy Mwalim akizungumzia Miradi inayotekelezwa na Mpango wa kunusuru kaya masikini nchini alisema ameridhishwa  na utekelezaji mzuri wa miradi hiyo ambayo lengo lake ni kuwasaidia wananchi na kuwaondoa katika umasikini.

“Katika ziara yangu nmeona  hatua kubwa iliyopigwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya TASAF ambapo nimeona kituo cha afya Kianga ambacho kinawasaidia wananchi ambao awali walikuwa wanatoka mbali kupata huduma za afya, pia nmetembelea majengo ya shule ya sekondari Fujoni na Mahonda na kuona namna wananchi watakavyo kwenda kunufaika,” alifahamisha Waziri Ummy Mwalimu.

Aktoa taarifa ya mpango wa kunusuru kaya Masikini Tasaf Zanzibar, Mratibu wa TASAF kanda ya Unguja, Makame Ali Haji alisema kwamba Mpango huo wa kunusuru kaya Masikini u nafaida kubwa kwa wananchi ambapo miradi inayoibuliwa na wananchi inalengo la kuwaongezea kipato, ujuzi na kutengeneza mali ya Jamii.

“Miradi hii ilitekelezwa kwa vipindi vitatu kwa mwaka 2014/2015, 2016/2017 na kipindi cha mwaka 2018/2019 jumla ya miradi 539 unguja na Pemba kupitia sekta ya za mazingira, Misitu, barabara, maji Uvuvi Kilimo na umwagiliaji,” alieleza Makame.

Aliongeza kuleza kwamba Jumla ya Shilingi 8,179,277,800.00 zilizipwa kwa walengwa ikiwa ni ujira wao wa kushirikia katika kazi.

Alifahamisha kwamba mpango wa kunusuru kaya Masikini TASAF una lengo la kuchangia na kujenga misingi kwa kaya Masikini kuondokana na Umasikini kupitia njia za kujiwekea akiba na kuwekeza katika vikundi na kuanzisha miradi ambayo ni endelevu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here