UGANDA: RAFU ZA KAMPENI, MUSEVENI ATISHIWA KUADHIBIWA NA TUME YA UCHAGUZI

0
Yoweri Museveni, Rais wa Uganda anaye gombea kutetea kiti chake kupitia chama cha NRM

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Uganda jaji Simon Mugenyi Byabakama, amesema kwamba tume hiyo haitasita kumchukulia hatua rais Yoweri Museveni ambaye ni mgombea urais kupitia chama cha National Resistance Movement – NRM, endapo hatafuta sheria za kampeni zilizowekwa na tume.

Kulingana na tume ya uchaguzi, wagombea wanastahili kuandaa mikutano ya kampeni isiyozidi watu 200, na lazima wafuate maagizo ya maafisa wa afya ya kukabiliana na janga la virusi vya Corona.

Maagizo hayo ni pamoja na kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kutokaribiana.

Museveni amekuwa akifuata maagizo hayo na kuhutubia wafuasi wake kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, lakini katika siku mbili zilizopita, amehutubia umati wa watu ambao hawakufuata maagizo ya afya, katika wilaya za Busia na Bukedi.

“Tutamwandikia barua kumkumbusha kwamba anastahili kufuata maagizo yetu ili sote tupambane na janga la Covid-19. Maagizo yetu hayana ubaguzi na usimamizi wetu wa kampeni hauna ubaguzi. Unapoidhinishwa na tume ya uchaguzi kugombea nafasi yoyote, unakuwa mgombea wetu na lazima ufuate masharti yetu,” amesema Byabakama akiongezea kwamba “mwelekeo tuliotoa unatumika kwa kila mgombea. Museveni ni mmoja wao na anastahili kufuata masharti yetu. Kila mgombea anastahili kuhakikisha kwamba wafuasi wake ama mawakala wake wa kampeni wanafuata masharti hayo.”

Byabakama alikuwa akihutubia waandishi wa habari baada ya kufanya mkutano na mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine katika makao makuu ya tume ya uchaguzi jijini Kampala.

Kyagulanyi alikutana na maafisa wa tume ya uchaguzi baada ya mikutano yake ya kampeni kuzuiwa na maafisa wa polisi wilayani Jinja na Kayunga.
Mikutano yake imekuwa ikishuhudia visa vya polisi kutumia gesi ya kutoa machozi na risasi za moto kutawanya wafuasi wake.

“Kama Byabakama ameshindwa kuandaa uchaguzi, anastahili kujiuzulu amoja na timu yake kwa sababu tunanyanyashwa na amesalia kimya.”amesema Kyagulanyi.

Hata hivyo, Byabakama amesema kwamba hawezi kujiuzulu na hajawahi kufikiria kwamba anaweza kujiuzulu.

“Mchakato wa uchaguzi ulianza mwaka 2018 na sasa tunakaribia kumaliza. Siwezi kujiuzulu kwa sababu ya mambo madogo yanayojitokeza. Tumewajibika katika kazi yetu kama tume ya uchaguzi la kuweka mwelekeo namna wagombea wanastahili kufanya kampeni lakini wagombea na wafuasi wao ndio wamekataa kufuata mwelekeo huo.”

Byabakama amewaambia waandishi wa habari kwamba tume ya uchaguzi imepanga kukutana na maafisa wa usalama Pamoja na wagombea ili kukubaliana namna ya kushirikiana kufanikisha uchaguzi mkuu wa Januari 14 2021 na uwe huru na haki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here