Ubungo yatoa mikopo ya Bil 1/= kwa vikundi 111

0

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam imekabidhi mkopo wa zaidi ya Sh bilioni 1 kwa vikundi 111 vya ujasiriamali.

Mkopo huo  ulikabidhiwa jana  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ya kila halmashauri kwa ajili ya kuvipa vikundi.

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa mkopo huo, mkuu wa wilaya ya Ubungo, Kisare Makori, alivipongeza vikundi hivyo vyenye wanachama 1,566 huku  akivikumbushia  vikundi hivyo umuhimu wa marejesho akisema  bado kuna changamoto kuhusu suala hilo.

Hata hivyo Makori alisema manispaa hiyo inadai Sh bilioni 1.7 zilizotolewa kwa vikundi hivyo mwaka jana.

Makori alisema mwaka wa fedha uliopita Ubungo ilitoa Sh bilioni 3.9 kwa vikundi 914 vyenye watu zaidi ya 9,281 lakini fedha zilizorejeshwa Sh bilioni 1.3 tu.

“Kiasi cha Sh bilioni 1.7 bado zipo mikononi mwa watu ambao hawajazirejesha. Rai yangu kwenu tusififishe ndoto na nia njema ya Serikali katika utaratibu huu wa kuwawezesha wananchi kiuchumi.

“Fedha hizi zikirejeshwa kwa wakati inasaidia kupanua wigo wa watu wengi kupata mikopo. Naomba tuwe na nidhamu ya kuzirejesha fedha hizi,” alisema Makori.

Mratibu wa mikopo wa manispaa ya Ubungo, Elizabeth Kebwe alisema vikundi hivyo vimetoka kwenye kata saba za manispaa hiyo zikiwemo za Goba, Kimara, Saranga, Msigani na Kwembe.

“Lengo la mafunzo haya kabla ya kuwapa mikopo  ni kuwajengea uwezo ili kufanya shughuli zao kwa ufanisi. Tunawafundisha kuhusu utunzaji wa kumbukumbu na akaunti zao na masuala ya ujasiriamali,” alisema Elizabeth.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here