Tuwe na utaratibu wa kuyakarabati majengo ya kale

0

JUZI Jumba la kihistoria la Beit al Ajaib, lililopo visiwani Zanzibar liliporomoka wakati likiwa katika ukarabati mkubwa unaosimamiwa na Serikali ya Kisultan ya Oman.

Jengo hilo lililojengwa mwaka 1883, limesimama kwa zaidi ya miaka 100 ambapo  ilichelewa kufanyiwa ukarabati wa aina hiyo hasa ikizingatiwa ujenzi wake ulitegemea mawe na udongo, kama hiyo haitoshi shughuli za kitalii zilizokuwa zikifanyika hapo zilihusisha pia matumizi ya maji bila utaratibu.

Kuna urithi mkubwa katika majengo yanayopatikana kwenye mikoa mbalimbali nchini, wachilia mbali maeneo ya kihistoria kama Bagamoyo, Kilwa, Zanzibar na kwengineko kama Tanga maeneo ya Pangani na Tongoni.

Lakini hata mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kaskazini yapo majengo ya kizamani ya Waarabu, Waajemi, Wajerumani, Waingereza na hata machifu wa Kiafrika katika makabila yaliyokuwa makubwa nchini. Yapo na yamesimama kwa zaidi ya miaka 100. Hakuna wa kuyatazama wala kuyashughulikia.

Hili linatakiwa kuwa funzo, watu wanaohusika na Mali Kale waliangalie hili la kuporomoka jengo la Maajabu (Bait al Ajaib) kama somo la kujua kuwa majengo haya itafika wakati yatachoka, yakiporomoka tutakuwa na hasara mbili, kwanza tutakosa fedha za watalii lakini pili tutapoteza maisha ya ndugu zetu ambao watafukiwa na vifusi.

Tunafahamu kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inalo jukumu la kuyasimamia haya, kuwepo na mfumo wa kueleweka wa kuwaita wataalamu wa majumba ya kale ambao wanaweza kuyakarabati upya yakawa kama zamani.

Mifano ipo mingi, Bagamoyo katika jengo la Boma. Kumefanyika ukarabati mkubwa ambao umelifanya jengo kama limejengwa jana. Ipo haja ya kuiga utaratibu huo. Inawezekana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here