TUNDU LISSU ASIMAMISHWA KAMPENI KWA WIKI MOJA

0

 

Mgombea urais kutoka chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu amesimamishwa kufanya kampeni kwa muda wa wiki moja.

Hatua hiyo imechukuliwa mapema hii leo na Kamati ya Maadili ya Taifa ya Tume ya Uchaguzi.

Katika taarifa yake, kamati hiyo imesema imechukua hatua hiyo baada ya malalamiko yaliyowasilishwa na Chama cha NRA na CCM wakilalamika kitendo cha Tundu Lissu alipokuwa mkoani Mara alipodai kuwa rais John Magufuli ameitisha kikao cha wasimamizi wa Uchaguzi nchi nzima ili kuhujumu Uchaguzi.

Taarifa hiyo pia imesema Lissu alilalamikiwa kutoa kauli za kichochezi pindi alipokuwa akifanya kampeni mkoani Geita.

“Baada ya makubaliano ya kina kamati imekubali kuwa Bw. Tundu Lissu amekiuka maadili ya uchaguzi kwa kutoa lugha chochezi na tuhuma zisizothibitika kinyume cha kanuni,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Hatahivyo akizungumza na vyombo vya habari Tundu Lissu amesema kwamba uamuzi huo sio wa haki akiongezea kwamba katika kutoa haki mtu anafaa kupewa tuhuma zake kabla ya kupatiwa adhabu.

Lissu ameongezea kwamba haukubaliki na kwamba kamati kuu ya Chadema itakutana siku ya Jumamosi ili kulijadili swala hilo na kulitolea uamuzi.

”Taratibu zote zilizowekwa katika maadili ya uchaguzi zimevurugwa’, alisema mwanasiasa huyo.

Hatahivyo anaruhusiwa kukata rufaa.

Lissu anatarajiwa kuendelea na kampeni zake kuanzia tarehe 10 mwezi Oktoba 2020.

Barua ya kumtaka Tundu Lissu kujibu tuhuma hizo iliandikwa kupitia katibu mkuu wa Chadema kulingana na taarifa hiyo .

Hatahivyo kwa mujibu wa taarifa hiyo ya NEC , katibu mkuu huyo alijibu kwamba malalamiko hayakihusu chama , hivyobasi mgombea na chama ni vitu tofauti.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here