Tumejenga daraja Kigongo- Busisi kuokoa maisha ya watu- Magufuli

0

Na Mwandishi Wetu

Rais Dk.John Magufuli  amesema toka akiwa Waziri wa Ujenzi amekuwa akitaka kuokoa maisha ya watu waliokuwa wakifa kwa kuzama katika Ziwa Victoria katika kivuko cha Kigongo- Busisi mkoani Mwanza.

Ameyasema hayo jana baada ya kukagua  maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Kigongo–Busisi ambalo litakuwa na urefu wa kilomita 3.2 na litakua ndio daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati.

Alisema kuna kisa cha kuhuzunisha ambacho alisema ndicho kilimfanya aweke dhamira ya kuhakikisha hilo daraja linajengwa

Akisimulia kisa hicho alieleza namna alivyonusurika kifo katika ajali iliyoua watu 11 baada ya kusita kupanda mashua iliyokuwa inavusha watu kutokana na kivuko kilichokuwepo kuharibika.

“Daraja hili nina historia nalo nakumbuka mwaka 2009 tulienda kuposa kule Busisi baada ya kuposa tukawa tunarudi usiku tukaambiwa kivuko kilichokuwepo nafikiri ni MV Sengerema kimeharibika na ilikuwa kawaida kuharibika, nilikuwa na pikipiki yangu nyekundu XL 125 na pale ilikuwa kivuko kikiharibika watu wenye mitumbwi wanakuja kupakia abiria wakaniambia panda ingia na pikipiki yako lakini roho yangu ikasita wengine wakapanda mimi nikazunguka nikafika Mwanza ndipo ikatoka taarifa wale mtumbwi ulizama na watu 11 wakapoteza maisha. Tumeamua kujenga daraja hili ili kuokoa maisha ya watu,” alisema Rais Magufuli.

Daraja hilo ambalo linajengwa na Mkandarasi wa China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa gharama ya karibu sh. Bilioni 700, linatarajiwa kukamilika Februari 2024 na tayari ujenzi umefikia asilimia 11.18.

Rais Magufuli amefurahishwa na hatua iliyofikiwa, lakini amemtaka Mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili likamilike haraka na kuanza kutumika.

Aidha Rais Magufuli alisema, daraja hilo lina umuhimu mkubwa kwa Watanzania na Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

“Niwapongeze wananchi wa Kanda ya Ziwa kwa kujengwa daraja hili ambalo litaepusha ajali za mara kwa mara za kuzama kwa mitumbwi inayovusha watu na bidhaa mbalimbali kati ya Kigongo-Busisi. Vijana mlioajiriwa Katika mradi huu mfanye kazi kwa bidii, msiibe vifaa vya ujenzi.

“Tumieni mvua zinazonyesha kulima mazao mbalimbali kwa wingi hasa ya chakula kwa kuwa yatahitajika Katika nchi ambazo wananchi wake wapo katika ‘lock down’ kutokana na ugonjwa wa Corona hivyo kushindwa kuzalisha Mali ikiwamo chakula kwa ajili ya mahitaji yao” alisema.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here