Trump na Biden walumbana juu ya COVID -19

0

WASHINGTON, MAREKANI

Rais Donald Trump na mshindani wake Joe Biden wamepambana katika mdahalo wa pili na wa mwisho wa kampeni za kugombea urais uliofanyika kwenye mji wa Nashville katika jimbo la kusini la Tennessse juu ya suala la virusi vya Corona nchini humo.

Biden aliyekuwa makamu wa rais wa Marekani hapo awali, alisema Trump hafai tena kuwa rais wa nchi hiyo kutokana na vifo vya wamarekani zaidi ya laki mbili vilivyosabaishwa na maambukizi ya virusi vya corona.

 Alisema rais Trump hana mkakati wowote juu ya kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo. Trump alijibu kwa kusema kwamba Wamarekani wanapaswa kutoka nje na kufanya kazi.

Katika mdahalo wa juzi uliofanyika kwa staha, tofauti na ule wa kwanza, rais Trump alidai kwamba chanjo dhidi ya virusi vya corona inakaribia kupatikana nchini Marekani.

Kwenye mdahalo huo rais Trump pia alimshutumu Biden kutokana na mahusiano ya mtoto wake nchini Ukraine. Trump alidai kwamba akina Biden wamejipatia mamilioni kutoka Ukraine. Trump alirudia tena kumtuhumu Biden na mtoto wake Hunter kwamba walifanya vitendo visivyo vya maadili nchini China na Ukraine ingawa hakuna ushahidi uliothibitishwa kuhusiana na madai hayo. Vile vileTrump alimtuhumu Biden kwamba amepokea fedha kutoka Urusi.

Joe Biden alikanusha madai hayo na alitetea familia yake. Alisisitiza kwamba hakuwahi kupokea hata senti moja kutoka nchi ya kigeni, na kusema Trump anajaribu kuwavuruga Wamarekani. Biden alibainisha kuwa aliweka wazi mrejesho wa ushuru aliolipa kwa kipindi cha miaka 22, ambapo hakuna ushahidi iwapo aliwahi kupokea pesa kutoka kwa chanzo chochote cha kigeni katika maisha yake.

Biden alimtaka Trump aonyeshe marejesho yake ya kodi badala ya kuwapakazia wenzake maneno yasiyo na ushahidi na Trump akajibu kuwa ataweka bayana haraka iwezekanavyo na kwamba alilipa kodi mapema kabla ya wakati katika miaka kadhaa iliyopita.

Wakati zimebakia siku 11 kabla ya uchaguzi, rais Trump anayewania muhula wa pili alijitetea juu ya madai ya kuwa na akiba ya benki nchini China na kusema kuwa akiba hiyo ya benki ni ya toka mwaka 2010 wakati alipokuwa mfanyabiashara.

Katika siku za hivi karibuni, maafisa wa Marekani waliripoti kuwa wadukuzi wa Urusi walilenga mitandao ya serikali za majimbo kadhaa na ile ya serikali za mitaa nchini Marekani na kuiba data kutoka kwenye seva mbili. Maafisa hao pia walituhumu Iran kwa kuhusika na kutumiwa barua pepe wapiga kura wengi wa chama cha Democratic katika majimbo kadhaa zikiwashinikiza au kuwatisha wampigie kura rais Donald Trump.

Juu ya madai ya kuingiliwa kati uchaguzi wa Marekani makamu wa rais wa zamani Joe Biden alisema ameweka wazi kuwa nchi yoyote, bila kujali ni ya nani, itakapobainika kuingilia kati uchaguzi wa Marekani, basi italipa gharama kubwa.

Mdahalo huo ulioonekana moja kwa moja kwenye televisheni kutoka Nashville, Tennessee, ulikuwa ni fursa ya mwisho kwa Trump wa chama cha Republican kuwasihi wapiga kura na kuweka mkazo kwenye kampeni iliyotawaliwa na janga la COVID -19 ambalo limesababisha vifo vya zaidi ya watu 220,000 nchini Marekani.

Kura za maoni zinaonyesha Trump yuko nyuma ya Biden, ingawa mashindano ni makali katika baadhi ya majimbo yanayogombewa ambayo yana nafasi kubwa ya kubadili mambo kwenye kinyang’anyiro hicho cha urais nchini Marekani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here