Trump atangaza kuiondoa Sudan kwenye orodha ya wafadhili magaidi

0

NEW YORK, Marekani

RAIS wa Marekani, Donald Trump amesema Sudan itaondolewa kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili makundi ya kigaidi, ikiwa itakubali kutoa dola milioni 335 kuwalipa wahanga wa Kimarekani wa mashambulizi ya kigaidi.

Hatua hiyo imetajwa itafungua milango kwa nchi hiyo ya Afrika kupata mikopo ya kimataifa na misaada inayohitajika kufufua uchumi wake uliporomoka pamoja na kuisaidia nchi hiyo kuwa ya kidemokrasia.

Akizungumza na kituo cha televisheni ya taifa, Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok ameliunga mkono tangazo hilo la Trump alilotoa juzi kwenye vyombo vya habari.

“Uamuzi huu utaisaidia Sudan kupata unafuu katika madeni yake. Leo hii tuna deni la zaidi ya dola bilioni 60. Uamuzi huu umetufungulia milango ya Sudan kuweza kupata afueni kutokana na deni hilo,” alisema Hamdok.

Trump ametoa tamko hilo hivi karibuni, wakati zimebakia takriban wiki mbili hadi siku ya uchaguzi mkuu wa Marekani, ambapo Ofisa mmoja wa Marekani amesema makubaliano hayo pia yanaweza kuichochea Sudan kuboresha uhusiano wake wa kidiplomasia na Israel.

Marekani ilichukua uamuzi wa kuiweka Sudan katika orodha ya magaidi mnamo mwaka 1993, ikiamini rais wa wakati huo, Omar al-Bashir alikuwa akifadhili makundi ya kigaidi.

Hata hivyo, wanasiasa nchini Sudan, wamesema uamuzi wa Trump ni uamuzi uliopitwa na wakati, kwa kuwa Bashir aliondolewa madarakani mwaka jana, na taifa hilo limekuwa likitoa ushirikiano katika vita vya kupambana na ugaidi.

Kutokana na hali hiyo, inakuwa vigumu kwa serikali ya mpito ya Sudan kuweza kupata msamaha wa madeni unaohitajika haraka pamoja na ufadhili wa kigeni kutokana na zuio lililopo.

Akizungumza zaidi hatua zinazochukuliwa, Waziri Mkuu, Hamdok alisema walianza mazungumzo na Marekani mwaka jana, ambayo yalizungumzia zaidi kwenye suala la fedha na huku Trump pia akiwataka Sudan iwalipe wahanga wa mashambulizi yaliyofanywa na mtandao wa Al-Qaeda katika balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania mnamo mwaka 1998.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here