TPA ilivyotekeleza maagizo ya Waziri Mkuu

0

NA JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema tayari wameshaanza kuyafanyiaka kazi maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya kuhakikisha Bandari ya Kagunga iliyopo Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma inaanza kazi ifikapo Januari Mosi, 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam yalipo makao makuu ya Mamlaka hiyo, Mhandisi Kakoko alimshukuru Waziri Mkuu kwa kuendelea kutoa maelekezo mbalimbali pale anapoona kuna kasoro katika bandari zao na kueleza kwamba watahakikisha bandari hiyo inaanza kufanya kazi Desemba 31, 2020 siku moja kabla ya siku aliyoagiza.

Itakumbukwa kuwa WAZIRI Mkuu Majaliwa aliipa wiki mbili kuanzia Desemba 18, 2020 TPA ihakikishe kwamba ifikapo Januari Mosi mwakani Bandari ya kimkakati ya Kagunga iliyoko katika Kata ya Kagunga wilayani Kigoma iwe imeanza kutoa huduma.

“Leo nimekuja hapa kuona bandari, hii bandari ilikamilika mwaka 2017 imekaa tu, nyumba zimejaa popo tu na mle ndani kumejaa takataka na mmefagia jana baada ya kusikia mimi nakuja, hovyo kabisa nawauliza hapa wanajikanyaga tu tuna mtumishi hapa hakuna mtumishi amekuja jana badaa ya kusikia nakuja hovyo kabisa hawa.”

Alitoa agizo Desemba 18, 2020 baada ya kukagua mradi wa bandari ya Kagunga iliyopo kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika, wilayani Kigoma. Waziri Mkuu alichukizwa na kitendo cha bandari hiyo kushindwa kutoa huduma licha ya kuwa imekamilika.

Waziri Mkuu alisema mbali na bandari hiyo ya Kagunga kuanza kazi Januari Mosi, 2021, pia aliagiza soko la kisasa la Kagunga nalo lianze kazi siku hiyohiyo ili kuwawezesha wananchi wa Kagunga waanze kufanya biashara na kuinua kipato chao.

Pia, Waziri Mkuu alishangwaza na kuchukizwa na kitendo cha Meneja wa Bandari kutoka Makao Makuu ya TPA ambaye hajawahi kufika katika bandari hiyo na haijui chumba chake. “Kama kweli wewe ni Meneja wa Bandari Tanzania bandari zako huzijui na una miaka chungu nzima unafanya kazi gani, hovyo kabisa.”

Waziri Mkuu alisema mradi wa ujenzi wa bandari hiyo ulikamilika 2017 ukihusisha ujenzi wa jengo la abiria pamoja na la mizigo, nyumba ya kuishi mtumishi na jengo maalumu lakini hakuna mtumishi katika bandari hiyo ambayo ujenzi wake uligharimu shilingi bilioni 3.8.

“…Tarhe moja ya mwezi wa kwanza mwaka 2021 nataka bandari hii ianze kazi, nenda mkajipange. Hapa hakuna mtumishi hamisha watumishi kama wapo Dar es Salaam, kama wapo Kigoma leta watumishi hapa wawatumikie wananchi kwenye bandari hii.”

Aliwaagiza watendaji wa TPA waruhusu meli na boti za watu binafsi zifanyekazi ya kutoa huduma katika bandari hiyo ili kuwawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha mizigo kwa urahisi. Alisema Serikali inataka majengo hayo yatumike kama ilivyokusudiwa. “Hizi fedha za Watanzania shilingi bilioni 3.8 watu wanafanya nazo mchezo tu, nataka nione bandari hii inafanya kazi.”

HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Mhandisi Kakoko alisema kwanza wamewachukulia hatua za kinidhamu wasaidizi wake waliotakiwa kuhakikisha bandari hiyo inaanza kazi mwaka 2018 kama ambavyo yeye mwenyewe aliwahi kuagiza.

Alisema mbali na kupeleka Wakurugenzi wanne kusimamia utekelezaji wa maagizo ya waziri mkuu wameshapeleka maafisa wawili wa kusimamia bandari na afisa mmoja wa usalama ameshahamishiwa katika bandari hiyo. Alisema pia wameingia makubaliano na SUMA JKT kwaajili ya kushirikiana na afisa huyo.

Kuhuu kukamilisha jengo la Polisi alisema wamejipanga likamilike kabla ya tarehe iliyoelekezwa na Waziri Mkuu yaani Januari Mosi na sasa litakamilika Desemba 29 na kufikia Desemba 31 polisi wawe wameshaingia.

 Kwa kwa upande wa barabara inayounganisha bandari hiyo na mpaka wa Tanzania na Burundi itakamilika Desemba 30 na kwamba kikwazo cha kukamilika kwake ambaye ni mwananchi aliyekataa kuhama sasa wamefikia makubaliano na amekubali kuhama baada ya kulipwa fidia ya Sh milioni 20.3.

Kwa upande wa soko la Kagunga ambalo Waziri Mkuu aliagiza likamilike Kakoko alitolea ufafanuzi kuwa Bodi ya Mamlaka ilipendekeza soko hilo liimarishwe ili kuongeza boti zitakazokuwa zinatia nanga katika gati hiyo kupeleka na kuchumkua mizigo ya sokoni.

“Maelekezo ya Waziri Mkuu ya kukabidhi soko lile yalitekelezwa wiki ile ile Alhamisi tuliweza kuandika barua kwa Halmashauri kuwakabidhi na Jumatatu kitendo hicho kitakamilika kwa timu yangu kuwakabidhi soko hilo rasmi,” alisema Kakoko.

“Kulikuwa na suala la uangalizi wa majengo tayari tumepeleka timu itasafisaha, viti pamoja na fanicha tumeshapeleka na nimepeleka timu ambayo ni pamoja na kapteni wetu, ili aweze kujadili na wenye boti.

“Kusema kweli eneo lile lilikuwa na changamoto ya wateja kuleta boti zao lakini kwasababu tumeshazungumza nao kwamba ni eneo zuri na kama walivyomsikia Wziri Mkuu basi na wenyewe watoe ushirikiano mzuri waweze kupatumia mahali pale.” Alisisitiza.

Kwa upande wa kuhakikisha gharama za barabara zinaangaliwa alisema tayari Meneja aliyekuwaanasimamia bandari hiyo ameshaachishwa kazi na hata aliyekuja baada yake naye ameachishwa kazi kwa kuchelewesha mambo.

Alisema yeye mwenyewe alitembelea bandari ile na kukuta inafanya kazi na kufanya mazungumzo na meneja wa Bandari ya Kigoma pamoja na Mhandisi wake.

“Inasikitisha kuona kwamba sisi TPA baadhi yetu tunasubiri kusukumwa na viongozi wakubwa.

Alisema Meneja huyo ambaye hakumtaja alihusika na mambo mengine ya utovu wa nidhamu na alishafukuzwa kazi na anaendelea na mambo mengine ya kisheria.

Alisema Menja huyo alitakiwa kuhakikisha miundombinu ya bandari hiyo imekamilika na inaanza kufanya kazi.

Alisema pia Mkurugenzi anayehusika na TEHAMA naye ameandikiwa kwa kushindwa kuhakikisha mashine ya kukusanya mapato ya POS inaanza kutumika katika bandari hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here