TIMU YA USHINDI

0

NA SHARIFA MARIRA, Dodoma

HATIMAYE kikosi cha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muhula wa pili katika awamu tano kimekamilika, hii ni baada ya jana jina la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupitishwa na Bunge kwa asilimia 100.

Majaliwa, jina lake lilipendekezwa jana na Rais Dk. John Magufuli likapigiwa kura na wabunge kwa asilimia 100 jambo ambalo limeandika historia mpya katika bunge hilo.

Majaliwa ambaye alikuwa katika nafasi hiyo kwa miaka mitano iliyopita aliinua shangwe bungeni baada ya jina lake kusomwa na Spika wa bunge Job Ndugai, ambapo kwa sasa timu ya ushindi imekamilika baada ya kupatikana Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.

Rais Dk. Magufuli amemteua Majaliwa kushika wadhifa huo kwa kuzingatia Ibara ya 51 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoeleza kuwa Rais atamteua Waziri Mkuu ambaye ni mbunge kutoka katika jimbo la uchaguzi ambaye anatoka katika chama chenye wabunge wengi bungeni.

Rais Dk. Magufuli aliwasilisha jina la Majaliwa bungeni, kupitia mpambe wake (Aide de Camp) Kanali Mlunga, ambaye aliingia akiwa na bahasha yenye karatasi iliyoandikwa jina la Waziri Mkuu.

Kanali Mulunga alimkabidhi Spika Ndugai bahasha hiyo kisha Ndugai akamtaka Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai kuifunga bahasha hiyo.

Wakati bahasha hiyo ikifunguliwa, Spika Ndugai alieleza namna ilivyohifadhiwa kwa kufungwa kisha kupigwa mihuri sita yenye chapa ya siri.

Baada ya bahasha hiyo kufunguliwa spika aliisoma kile kilichoandikwa ambapo alilitaja jina la Kassim Majaliwa kuwa ndiye aliyependekezwa na Rais Dk. Magufuli kuwa waziri mkuu.

HISTORIA YAKE

Kassim Majaliwa alizaliwa Desemba 22 mwaka 1960 mkoani Lindi ambapo alisoma Shule ya Msingi ya Mnacho, kati ya mwaka 1970 na 1976.

Aidha, alijiunga na Shule ya Sekondari Kigonsera, mkoani Ruvuma kati ya mwaka 1977 na 1980.

Baada ya hapo, alijiunga katika Chuo cha Ualimu Mtwara kati ya mwaka 1991 na 1993 kisha mwaka 1994 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambako alisomea ualimu kisha kuhitimu mwaka 1998.

Mwaka 1999 alijiunga na Chuo Kikuu cha Stockholm nchini Sweden kwa masomo ya stashahada ya uzamili.

Kuanzia mwaka 1984, Majaliwa ametumikia nafasi mbalimbali za utumishi serikalini ikiwemo kufundisha shule mbalimbali mkoani Lindi.

Vilevile aliwahi kuwa Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya na baadae mkoa kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani na Urambo mkoani Tabora.

Majaliwa alijitosa kwenye uwanja wa siasa mwaka 2010, alipopitishwa CCM kugombea Jimbo la Ruangwa ambalo liliachwa wazi na Selemani Ng’itu aliyefariki dunia Novemba 2009 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutokana na ugonjwa wa shinikizo la damu.

Katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 2010, Majaliwa alimwangusha mgombea wa Chama Cha Wananchi (CUF) Abubakar Kondo, baada ya kupata kura 27,671 sawa na asilimia 72.98 dhidi ya kura 9,024 sawa na asilimia 23.8 alizopata Abubakar.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alimteua kuwa Naibu Waziri akisimamia elimu.

Mbali na uwanja wa siasa, Majaliwa ni mwanamichezo mahiri hususan mpira wa miguu ambapo amechukua mafunzo ya ukocha ambapo ana leseni daraja A yenye uwezo wa kufundisha timu ya soka daraja lolote.

MAJALIWA ASHUKURU

Baada ya uteuzi huo Majaliwa alimshukuru,Dk Magufuli,wabunge, wapiga kura, familia pamoja na chama cha mapinduzi akidai kwamba amewiwa kupewa tena nafasi hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa weledi na kuleta maendeleo nchini.

Alisema hakutegemea kama atapewa tena nafasi hiyo hasa akizingatia kauli ya Dk Magufuli aliyoitoa hivi karibuni kwamba atalibadili baraza la mawaziri.

MAONI YA WABUNGE

Mbunge wa Tanga Mjini,Ummy Mwalimu,alisema amefurahi Rais John Magufuli alivyomuamini tena, Waziri Mkuu ,Kassim Majaliwa ,akidai kwamba ni  mnyenyekevu kwa Mawaziri wenzie, ana msaada na mchango mkubwa katika utendaji.

“Nina furaha kubwa sana ,nilikuwa nikimuombea mhe Majaliwa ,nilifanya naye kazi kwa miaka mitano nikiwa Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wazee na Watoto,yaani hata ukipata shida kwenye utendaji ni mtu ambaye ni rahisi  kufikika, nimefurahi kuliko maelezo,ni mtu mchapakazi ambaye muda wote ukimpigia simu ,yeye ni waziri mkuu lakini hajikwezi alikuwa akituita mawaziri wenzangu tufanye hiki tufanye kile “alisema Ummy

Naye Mbunge wa Kibakwe,George Simbachawene, alisema Majaliwa ni mtu wa pekee, ana hekima, mpole na anasikiliza shida, ana busara na hekima lakini pia ni mtu anayefanya kazi kwa weledi hivyo jina lake lilivyoletwa Rais Magufuli amewatendea haki watanzania.

“Tunajivunia kwakuwa nilikuwa nafanya naye kazi nikiwa Waziri lakini pia niliwahi kufanya naye kazi kabla hata hajawa waziri mkuu ,Majaliwa ni  msikivu unaweza ukawa umechanganyikiwa, una tension lakini ukifika kwake anakupokea ule mzigo, hakuachi uumie na mzigo mwenyewe anafanyia kazi alafu anakurudishia jambo lako ufanyie kazi “alisema Simbachawene

Alifafanua kuwa wabunge watakaoteuliwa na Rais kuwa mawaziri na kufanya kazi na Majaliwa watashuhudia ukarimu na utendaji wenye ushirikiano  na wakusaidiana na kusikiliza shida pale watakapokwama.

Alisema watanzania wengi wanamfahamu kwa namna anavyojituma katika shughuli za kiserikali lakini waamini zaidi kwamba ni mtendaji mzuri na ana karama ya kipekee,alimpongeza Rais kwa kuchuja vizuri na kuleta jina ambalo linafaa na ndio maana wabunge wamempitisha kwa asilimia 100.

Kwa upande wake,Mbunge wa Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, alisema ana uhakika watanzania na wabunge wote watakuwa wamefurahi kuona jina la Majaliwa limerudishwa tena kwani utendaji wake ulionekana kwa kila mtu.

Stella Manyanya ambaye katika serikali ya awamu ya tano alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji alisema “Wabunge wamefurahi sana ndio maana wametoa kura asilimia  100,Majaliwa ni mtendaji mzuri,mchapakazi, anashirikisha watu,hajawahi kuvunja maadili kwa namna yoyote na hana tamaa ndio maana ni kiongozi anayependwa na watu”

Mhandisi Manyanya alisema kama inavyojulika nchi imefanya vizuri huwezi kumuweka pembeni waziri  mkuu hivyo kuteuliwa kwake kunatoa taswira kwamba nchi inaenda kuwa bora zaidi ya miaka mitano iliyopita.

Aidha,Mbunge wa Ukonga,Jerry Silaa,alisema serikali hii inaenda kufanya kazi kubwa kuliko ya awali kwani viongozi wote waliokuwepo ambayo waliivusha nchi katika uchumi wa kati wamerudi ,hivyo kitendo cha rais kurudisha jina la Majaliwa kinaonesha ni jinsi gani anataka kazi iliyokuwa imefanyika iendelezwe kwa uweledi mkubwa.

Aliyekuwa Waziri wa Madini ,Dotto Biteko,alisema Majaliwa ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za serikali na miaka mitano iliyopita serikali imefanya vizuri kwa maana kwamba kuna mchango mkubwa wa Majaliwa hivyo ni jambo la kumpongeza na kumtakia heri  katika kuyatekeleza majukumu yake na kuiletea maendeleo nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here